Na Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein ameiagiza Wizara ya Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo kutoa taarifa kwa wananchi wa kisiwa cha Pemba juu ya hitlafu zilizosababisha kushindwa kuona vyema matangazo ya Shirika la Utangazaji (ZBC) televisheni na kufanya juhudi za haraka kurekebisha hali hiyo.
Hayo aliyasema leo wakati alipokutana na watendaji na viongozi wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo katika mkutano kati ya uongozi huo na Rais uliofanyika Ikulu mjini Zanzibar ambao una lengo la kuangalia utekelezaji wa robo tatu ya malengo makuu ya mpango kazi wa mwaka wa fedha 2011-2012 pamoja na vipaumbele na malengo kwa mwaka 2012-2013.
Katika mkutano huo ambapo Makamu wa Kwanza wa Rais Maalim Seif Sharif Hamad, pamoja na Katibu wa Baraza la Mapinduzi na Katibu Mkuu Kiongozi Dk. Abdulhamid Yahya Mzee, wameshiriki, Dk. Shein alieleza kuwa ipo haja ya kuwapa taarifa wananchi wa kisiwa hicho ili waelelewe tatizo lililotokezea na juhudi zinazochukuliwa katika kurekebisha hali hiyo.
Dk. Shein, alisema kuwa iwapo wananchi watapewa taarifa huku wakifahamishwa juhudi zinazochukuliwa ili kuweza kuona vyema matangazo ya Shirika lao hilo kwa upande wa televisheni itakuwa ni jambo la busara na wataweza kutambua kinachoendelea.
Pia, Dk. Shein aliunga mkono juhudi zinazochukuliwa na Wizara hiyo katika kulikarabati jengo kongwe la studio ya kurikodia muziki liliopo Rahaleo ambalo litawasaidia wasanii wa hapa nchini kurikodi sanaa zao, agizo ambalo linatokana na ziara yake aliyoifanya wakati akitembelea taasisi za Wizara hiyo mwaka jana.
Aidha, Dk. Shein alisisitiza haja kwa watendaji na viongozi wa serikali kuandaa ripoti juu ya safari zao za kikazi wanazokwenda ndani na nje ya Zanzibar ili ripoti hizo ziweze kusaidia katika utendaji wao wa kazi.
Pamoja na mambo mengineyo, Dk. Shein alieleza azma ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar za kuweka mtambo mpya wa kuchapisha vitabu vya bajeti, nyaraka za serikali pamoja na mtambo mkubwa kwa ajili ya kuchapishia magazeti.
Pia, Dk. Shein alitoa pongezi kwa uongozi wa Gazeti la Zanzibar Leo kwa kupanua huduma za magazeti na kueleza haja ya kuongeza kasi kwa kuchapisha machapisho mengi zaidi huku akieleza azma ya serikali ya kutafuta mtambo ili gazeti hilo liweze kuchapishwa hapa hapa Zanzibar.
Dk. Shein, alieleza haja ya kutengeneza filamu inayozungumzia maendeleo ya Zanzibar ili wananchi waweze kujua hatua za maendeleo zinazochukuliwa na serikali yao. Pamoja na hayo, uongozi wa Wizara hiyo, ulieleza kuwa tayari matengenezo ya studio ya kurushia matangazo kwa njia ya dijitali iko tayari na imeshaanza kutumika.
Wizara hiyo ilieleza kuwa juhudi zimekuwa zikifanyika katika kuhakikisha Zanzibar inaingia katika matangazo ya dijitali pale muda uliopangwa utakapofika.
Mapema Waziri wa Wizara hiyo, Said Ali Mbarouk, akisoma utangulizi wa utekelezaji huo pamoja na mambo mengineyo alisema kuwa Baraza la Kiswahili limefanya tafiti kwa wasanii waliofariki miongoni mwa hao ni marehemu Bwana Bakari Abeid, marehemu Iddi Abdalla Farhani na marehemu, Issa Haji Pandu (Issa Matona).
Aidha, uongozi huo ulieleza kuwa kwa upande wa wa wasanii wa vitabu Baraza limeandaa utaratibu wa kuwasajili wasanii wa vitabu na kutoa mafunzo kwa wasanii hao pamoja na walimu wa skuli ili kuwa na utaratibu wa kuvitumia vitabu hivyo. Pia, Wizara hiyo ilieleza juhudi zake za kuanza utaratibu wa kupasha habari kwa njia ya ishara ili kuwapatia fursa watu wenye mahitaji maalumu.
Pamoja na hayo Wizara hiyo ilieleza hatua inazozichukua katika kuimarisha ubora wa matangazo ili kuweza kuwavutia wasikilizaji, watazamaji na wafanyabiashara wa ndani na nje ya Zanzibar. Pia uliezo kukua kwa soko sanjari na mapato ya gazeti hilo.
Kwa upande wa Gazeti la Zanzibar Leo, uongozi huo ulieleza azma yake ya kuhakikisha gazeti hilo linawafikia wasomaji Zanzibar nzima na baadhi ya maeneo zaidi ya Tanzania Bara pamoja na kukuza uwezo wa waandishi wa habari wa magazeti na wafanyakazi wa ajili ya kuongeza ubora wa makala, habari na matukio yanayochapishwa gazetini.
Wizara hiyo pia, ilieleza mikakati yale iliyoiweka katika kukuza, kueneza na kuutangaza utalii wa Zanzibar Kitaifa na Kimataifa sanjari na kukuza idadi na ubora wa huduma za watalii. Uongozi huo pia ulieleza lengo lake la kuimarisha Makumbusho na mambo ya kale na kushajiisha jamii kuwa na mwamko wa kuyatembelea kwa ajili ya kufahamu umuhimu na matumizi yake.