MTANDAO wa Jinsia Tanzania (TGNP) kupitia kikundi kazi chake cha uchambuzi wa bajeti (Budget Analysis Task Team) wakishirikiana na wanaharakati wengine kutoka ngazi ya jamii wamefanya uchambuzi wa muongozo wa mpango wa miaka mitano wa bajeti kwa mwaka wa fedha utakaoanza Julai mwaka 2011/2012 hadi 2015/16 . Uchambuzi huu umefanywa kwa mtazamo wa ukombozi wa wanawake kimapinduzi, wakiongozwa na kauli mbiu ya “Haki ya Uchumi: Rasilimali Ziwanufaishe Wanawake walioko Pembezoni”.
Uchambuzi huu umefanyika katika muktadha ambapo ndio kwanza nchi yetu imetoka katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2010 wa urais,wabunge na madiwani na bunge ni jipya pamoja na hali ya vuguvugu la kudai mabadiliko ya Katiba mpya ambayo imeonekana kuwa na changamoto nyingi kwa serikali kutokana na mapungufu yaliyoainishwa na wananchi. Kwa hiyo basi, mategemeo makubwa yalikuwa kuona msimamo wa serikali katika kutetea haki na usawa wa kila mwananchi, kwa kuelekeza rasilimali za kutosha ili kufanikisha mchakato huu wa mabadiliko ya katiba, ambao ndio mhimili kwa wapiga kura walio wengi, hasa wanawake walioko pembezoni ikiwa ni pamoja na makundi mengine ya watu wanaoishi na ulemavu aina zote, VVU na UKIMWI. Tumeshangaa kuona kuwa hakuna mikakati mahususi ya kuelekeza rasilimali katika eneo la katiba.
Vipaumbele vilivyoainishwa katika muongozo wa bajeti kwa mpango wa miaka mitano 2011/12-1025/16 vimeelekezwa zaidi kwenye; Kilimo, miundo mbinu, viwanda, uwekezaji katika rasilimali watu,mazingira endelevu,usimamizi wa ardhi, mipango miji na makazi,kuimarisha mahusiano kati ya sekta ya umma na binafsi na kuendeleza mafanikio katika sekta za kijamii.
Je vipaumbele hivi vimetokana na mpango wa uibuaji wa fursa na vikwazo kwa maendeleo (O & OD) ambao unatoa nafasi kwa walio wengi kuibua vipaumbele vyao wenyewe? Nani anafunaika zaidi, wawekezaji wakubwa au wawekezaji wadogo? Kwa upande wa kuwekeza katika rasilimali watu, ni kwavipi kila sekta iatongeza ajira kwa watu na ni ajira za namna gani?
Muongozo wa bajeti uliopangwa kwa mwaka 2011/2012 unatarajiwa kuwa Shilingi. milioni 11,970,356 ukilinganisha na milioni 11,609,557 mwaka 2010/2011 ambapo bajeti inazidi kuwa kubwa wakati huohuo mapato ya ndani yanazidi kushuka. Ikizingatiwa kuwa bajeti ya serikali ni tegemezi kwa kiasi kikubwa kwa wafadhili na deni la taifa linazidi kukua kutoka Shilingi 7.6 trilioni (2008/2009) hadi Sh10.5 trilioni (2009/2010) ambayo ni sawa na ongezeko la asilimia 38 (Ripoti ya Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali,2010), je ni kwa vipi serikali inapanga kuongeza ukubwa wa bajeti wakati deni inazidi kukua na mikopo na misaada ya wafadhili haitabiriki? Tunadai serikali ipunguze utegemezi wa bajeti kutoka kwa wafadhili kwa kuboresha ukusanyaji wa mapato ya ndani na kupunguza ukubwa wa serikali, yaani wizara, mawaziri na manaibu Waziri kufikia kiasi ambacho hakitaathiri sana ukubwa wa bajeti.
Muongozo wa bajeti unasisitiza uimarishaji na uendelezaji wa masuala ya uchumi mpana na siasa kwa kuweka mazingira mazuri ya uwekezaji, kuzuia mfumuko wa bei, kuendeleza sekta binafsi, kusimamia usawa katika bei ya mafuta kwa kuwekeza kupitia rasilimali watu. Sisi kama wanaharakati tulitarajia kuona muongozo huu wa bajeti unaweka kipaumbele katika kusimamia mgawanyo sawa wa rasilimali katika jamii, kurasimisha kazi zisizo na kipato zinazofanywa na wanawake na wanaume walioko pembezoni. Pamoja na masuala mengine, suala la ‘mabadiliko ya dhana’ yaani ‘paradigm shift’ na kuipa ‘fursa’ kipaumbele zaidi kuliko ‘mahitaji ya watu’ inatupa wasiwasi sana; tunadai kuwe na mdahalo mpana wa kitaifa juu ya mawazo haya, maana inaweza kuleta matokeo hasi kwa maendeleo ya uchumi wa taifa. Vilevile tunapinga suala la kuweka kipaumbele katika uuzaji wa bidhaa nje ya nchi kwa wawekezaji wakubwa wakati soko la ndani la bidhaa linakufa.
Tumeshangazwa na kushtushwa sana kuona kwamba pamoja na juhudi zote za serikali kuendeleza kilimo na kuwa na mkakati wa mapinduzi ya kijani “Kilimo Kwanza”, ukuaji wa kilimo unatarajiwa kukua na kufikia wastani wa 5.5% tu. Ukuaji huu hauendani kabisa na umuhimu wa kilimo kwa watanzania walio wengi. Halikadhalika pamoja na kilimo kuwekewa kipaumbele, mchango wa kilimo katika pato la taifa unatarajiwa kupungua kutoka asilimia 21.9 (2010) hadi 18.7 (2011) na hii itakuwa na athari kubwa kwa wakulima wadogo wadogo ambapo wengi wao wanategemea sana kilimo hasa jamii kubwa ikiwa ni wanawake.
Tunasikitishwa kuwa bado hakuna mkakati wa wazi au chanzo mbadala cha nishati kama vile gesi, upepo au makaa ya mawe kwa ajili ya kutatua changamoto iliyopo ya umeme. Miaka 50 baada ya uhuru tunadai kwamba kila Mtanzanaia ana haki ya umeme akiwa kijijini au mjini. Pia tulitarajia kuona bajeti ya serikali inaliimarisha shirika la umeme nchini (TANESCO) kwa kulijengea uwezo ili kuondokana na tatizo la ukodishaji mitambo ya uzalishaji umeme toka nje ya nchi, ambapo mara kwa mara mitambo hiyo imekua ikiligharimu taifa kutokana na kuwepo kwa udanganyifu katika manunuzi na ukodishwaji wake. Tunadai uwajibikaji kuanzia kwa Waziri hadi maafisa wengine wanaohusika na suala la nishati ya umeme hapa nchini.
Kwa upande wa sekta ya elimu, serikali kuendelea kubajeti wastani wa shilingi 1,500 kwa kila mwanafunzi kwa siku kwa ajili ya chakula kwa wanafunzi wa shule za msingi na sekondari haiendani kabisa na hali halisi ya mahitaji ya lishe na kupanda kwa maisha. Asilimia 40 ya ruzuku maalum [capitation grant] kwa wanafunzi hutolewa kwa ajili ya ununuzi wa vitabu lakini hali halisi iliyopo inaonyesha kwamba shule nyingi za msingi kufikia mwezi Disemba 2010 zimepokea kiasi kisichozidi jumla ya Shilingi 60, 000 hadi 300,000/= tu kwa ajili ya kununulia vitabu vya kiada na ziada kwa mwaka 2009/2010 (rejea report ya Mkaguzi mkuu wa Hesabu za Serikali ya mwaka 2010). Hali hii tunayoiona ni kwamba shule nyingi hazina vitabu na kila mtoto anaambiwa ajinunulie vitabu. Tunahoji pesa hizi nyingine za ruzuku maalum zinakwenda wapi?
Katika Sekta ya Afya muongozo haukueleza ni jinsi gani serikali itakabiliana na changamoto za uzazi salama. Tunakumbuka na kuunga mkono ahadi iliyotolewa na Wizara ya Afya na Maendeleo ya Jamii kwamba kila mama mjamzito atapewa vifaa vya kujifungulia bure (The Citizen, 6th My 2011) ,tunadai utekelezaji wa ahadi hiyo ya wizara. Kwa mantiki hiyo, tulitarajia kuona muongozo unaelekeza kutengwa kwa bajeti ya Afya inayoanzia asilimia 15 kama ilivoelekezwa katika azimio la Abuja pamoja na mikakati mahususi ya kuhakikisha eneo la afya linaboreshwa. Na je pia kuna vivutio gani vitatolewa kwa manesi wakunga wanaofanya kazi katika mazingira magumu?
Kutokana na yaliyojitokeza katika muongozo wa bajeti, sisi kama wanaharakati wa ukombozi wa wanawake kimapinduzi tunadai yafuatayo:
• Kutengwa kwa rasilimali za kutosha zitakazowezesha mchakato wa mabadiliko ya Katiba kufanyika kwa ufanisi zaidi.
• Ushiriki zaidi wa wananchi katika mchakato mzima wa kutengeneza Katiba mpya ili kuweza kuainisha vipaumbele vyao.
• Mikakati ya kuimarisha soko la bidhaa za ndani kwa kuimarisha barabara za vijijini zitakazosaidia kuchukua mazao ya wakulima wadogo wadogo ambao wengi wao ni wanawake ili kuinua pato la ndani la taifa na kuimarisha uchumi mkuu.
• Mikakati maalum ya kuongeza ajira, maisha endelevu na kipato kwa wote, wanawake na
wanaume, mijini na vijijini.
• Ushiriki wa wananchi katika michakato yote ya bajeti kuanzia mwanzo uboreshwe ili masuala yao yote muhimu yaweze kuingizwa na kupewa bajeti ya kutosha.
Mwongozo wa bajeti ni lazima ulenge namna uchumi wa nchi utakavyojenga maisha ya watu wake kwanza na si kuangalia tu wawekezaji wa ndani na nje ya nchi. Suala la ajira na maisha endelevu kwa wote liwekewe kipaumbele. Masharti yawekwe kwa wawekezaji ili kila mmoja (awe wa ndani au nje) aongeze idadi ya wafanyakazi kwa asilimia kadhaa kufuatana na sekta husika. Katika utekelezaji wa malengo ya MKUKUTA II lazima muongozo uzingatie masuala ambayo yataleta maendeleo kwa wananchi hasa wanawake walioko pembezoni na si kuangalia masuala ambayo yatawafanya wananchi kuwa watumwa katika nchi yao. Suala la mahusiano kati ya sekta ya umma na sekta binafsi (PPP) litazamwe kwa kina zaidi kuona nani anafaidika zaidi, wawekezaji au wananchi? Kwa hiyo tunadai mwongozo wa bajeti ambao utaboresha maisha ya jamii nzima hasa wanawake na wanaume walioko pembezoni.
Imetolewa na Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP)
na kusainiwa na; Usu Mallya, Mkurugenzi Mtendaji wa TGNP
25/05/2011