Na Mwandishi Wetu, Moshi
WANAFUNZI watano wa Shule ya Sekondari Kiusa na moja wa Sekondari ya Regnald Mengi zilizopo katika Manispaa ya Moshi mkoani Kilimanjaro, wanashikiliwa na Jeshi la Polisi mkoani hapa kwa tuhuma za kukutwa wakivuta bhangi jambo ambalo ni kinyume cha sheria.
Kaimu Kamanda wa Polisi mkoani hapa, Yusuph Ilembo amethibitisha kukamatwa kwa wanafunzi hao na kuongeza kuwa walikamatwa Mei 16, 2012 majira ya saa 3 asubuhi katika eneo la pembezoni mwa Soko la Mitumba la Memorial Manispaa ya Moshi huku wakiwa wanavuta bhangi.
Akielezea mazingira ya tukio hilo kamanda Ilembo alisema wanafunzi hao walikamatwa baada ya kukutwa na msamaria mwema wakiwa wanavuta Bhangi na kutoa taarifa katika kituo cha polisi.
Kwa mujibu wa Kamanda Ilembo wanafunzi hao ambao walikutwa wakiwa wamevaa sare za shule wajiingiza kwenye tukio hilo la uvutaji Bhangi mara baada ya kurudishwa nyumbani na walimu wao kutokana na makosa ya utovu wa nidhamu.
Ilembo aliwataja wanafunzi hao kuwa ni Amidu Kasu (17), Isack Nzila (17) na John Kingwali (17), ambao ni wa kidato cha nne, Frank Ringo (15)na Kasmir Godfrey (16) wa kidato cha tatu ambapo wote ni wa shule ya sekondari ya Kiusa pamoja na Samuel Moses (15) wa kidato cha nne katika shule ya sekondari ya Regnald Mengi.
Alisema wanafunzi hao baada ya kukamatwa na kupekuliwa walikutwa na msokoto mmoja wa bhangi ambapo inasadikiwa misokoto mingine walikuwa tayari wameshaivuta.
Aidha kamanda Ilembo alisema kuwa kitendo cha wanafunzi hao kukutwa wakivuta bhangi ni kosa la jinai na kwamba upelelezi bado unaendelea na pindi utakapokamilika watafikishwa mahakamani ili kujibu shitaka linalo wakabili.
Hata hivyo, Ilembo aliwataka wazazi kujijengea tabia ya kufuatilia maendeleo ya watoto wao wawapo shuleni na kuhakikisha wanawakagua kila mara warudipo nyumbani ili kutokomeza tatizo la uvutaji bhangi kwa wanafunzi ambalo limeibuka na kushika kasi kwa sasa.
Tukio hilo limetokea siku chache mara baada ya mkurugenzi wa manispaa ya Moshi Bi. Bernadette Kinabo kueleza kuwa utumiaji wa madawa ya kulevya kwa wanafunzi wa shule za sekondari katika manispaa hiyo ni tatizo kubwa.
Bi. Kinabo alisema Halmashauri hiyo inaangalia uwezekano wa kukutana na wazazi, walimu na hata polisi ili kuweza kuweka mikakati ya kukabiliana na tatizo hilo ambalo ni kikwazo kikubwa katika kuinua kiwango cha taaluma.