Naibu Waziri wa Afya ataka waganga wakamatwe

Na Mwandishi Wetu
Morogoro
NAIBU Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Lucy Nkya ameiagiza Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro kuwachukulia hatua za kisheria watu waganga wanaobandika mabango kujitangaza wanatibu magonjwa sugu kumbe wanafanya utapeli.
Dk. Nkya alitoa kauli hiyo jana mjini hapa wakati wa semina ya Ukimwi kwa madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro na watendaji wa wilaya hiyo kwa lengo la kuwaweka mstari wa mbele kukemea maambukizi mapya ya janga hilo la Ukimwi.
Naibu Waziri huyo ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Morogoro Kusini Mashariki alisema waganga hao hawaruhusiwi kujitangaza na hata kuweka mabango eneo lolote kwani hawatambuliki kisheria.
Aliutaka uongozi wa halmashauri hiyo kuwachukulia hatua kali za kisheria, watakaobainika kujitangaza, na kungeza kuwa watu ni waongo, na wanawachukulia wananchi fedha zao wakati hawana uwezo wa kutibu.
“Wachukulieni hatua wote wanaojitangaza kuwa wanatibu magonjwa sugu ukiwemo ugonjwa wa Ukimwi na kisukari kwa kuwa wanasema uongo tu hawana dawa hizo,” alisema.
Aidha akizungumzia tiba inayotolewa katika Kijiji cha Samunge na Mchungaji wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Mchungaji Ambilikile Mwasapila, alisema kuwa tiba hiyo inaendana na imani ya mtu.
Alisema kuwa katika uchunguzi uliofanywa awali na Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii unaonesha kuwa tiba ya ‘babu’ inaweza kuzuia usiwe na mafuta kwenye mishipa ya damu, na kwamba wizara imeweka maabara katika eneo hilo ili kuendelea na uchunguzi zaidi.
Dk. Nkya aliyataja magonjwa mengine ambayo inadaiwa yameonekana kutibiwa na tiba ya ‘babu’ kuwa ni pamoja na kifua kikuu, kansa na kisukari na kwamba tiba hiyo inahitaji imani zaidi.