Na Shomari Binda, Wa Binda News-Bunda
TIMU ya wapiga debe wa stendi ya mjini Bunda (Town Stars Fc) wameibuka mabingwa wapya wa Kombe linanaloandaliwa kila mwaka na Mbunge wa Viti maalumu kupitia vijana (CCM), Ester Bulaya na kuibuka na kitita cha sh. laki tano pamoja na kombe baada ya kuifunga timu kongwe ya Amani Fc kwa mikwaju ya penati 4-2 baada ya timu hizo kushindwa kufungana katika muda wa kawaida wa mchezo huo uliofanyika katika Uwanja wa Sabasaba Mji Bunda.
Katika mchezo huo uliokuwa na ushindani mkubwa na kuhudhuliwa na mashabiki wengi katika uwanja huo ulizishuhudia timu zote zikimaliza dakika 90 za mchezo huo uliochezeshwa na mwamuzi wa Ligi Kuu, Amon Paulo kwa umakini mkubwa na kuamuliwa mikwaju ya penati ambayo iliiwezesha town stars kuibuka na ushindi huo.
Shujaa wa mchezo huo alikuwa kipa wa timu ya Town Stars, Nyaku Nyaku baada kuokoa michomo kadhaa ya washamuliaji wa timu ya Amani katika dakika za kawaia za mchezo huo kabla ya kuokoa penati 3 na kufanikiwa kwa kiasi kikubwa kuchangia ubingwa wa timu yake.
Licha ya mabingwa hao wapya kuchomoza na kitita hicho, washindi wa pili timu ya Amani Fc ilichomoza na kitita cha sh. laki mbili na nusu huku mshindi wa tatu timu ya Polisi Bunda ikiondoka katika mashindano hayo na zawadi ya sh. laki moja na nusu huku timu ya Mwembeni Fc ikiondoka na sh. laki moja baada ya kuwa timu yenye nidhamu.
Kwa upande wa mchezaji bora wa mashindano hayo yaliyoshirikisha jumla ya timu 22 Ramadani kitundu wa Amani alipata sh. elfu hamsini huku mfungaji bora, Sebastian Rapahael wa Balili Fc alizawadiwa pia zawadi ya shilingi elfu hamsini kutokana na kutupia kimiani mabao 7.
Akifunga mashindano hayo Mbunge wa viti maalumu kupitia vijana (CCM) Ester Bulaya alisema lengo la mashindano hayo ni kutaka kuibua vipaji na kuzalisha ajira kupitia michezo kwa kudai kuwa michezo ikihamasishwa na kuwa na mashindano ya mara kwa mara kutafawafanya vijana kujitambua uwezo wao na kujitafutia kipato.
Alisema kupitia mashindano hayo katika msimu wake wa kwanza vipaji mbalimbali viliibuliwa na mpaka leo kuna wachezaji wanaochezea timu kubwa akiwemo mchezaji mmoja ambaye anakipiga katika kikosi cha kwanmza cha timu ya yanga B huku wengine wakiichezea timu ya maafande wa Polisi Mara ambao kwa sasa wanajiandaa na fainali za ligi ya Taifa ngazi ya Taifa itakayoaanza Mei 26.
Bulaya alisema mashindano hayo yatakuwa yakifanyika kila wilaya ya Mkoa wa Mara na kueleza kuwa kipindi kinachokuja zawadi zaidi zitaboleshwa ili kuweza kuleta changamoto mbalimbali na ushindani katika mashindano hayo ambayo yatakuwa yakifanyika kila mwaka.