Mikopo ya siri yaziliza familia Tanzania

Mkurugenzi Mtendaji wa TAMWA, Ananilea Nkya

Na Mwandishi Wetu

WANANDOA wanapaswa kuepuka kuingia mikopo ya siri ikiwa ni pamoja na kuweka rehani mali za familia ili kuepusha familia kupoteza mali zake endapo aliyekopa atashindwa kulipa deni hilo.

Kauli hiyo imetolewa leo jijini Dar es Salaam katika taarifa ya Mkurugenzi Mtendaji wa Chama cha Wanahabari Wanawake (TAMWA), Ananilea Nkya huku akishauri ni vema familia kufahamishana na kukubaliana wanapoamua kuchukua mkopo na kuweka rehani nyumba au mali nyingine ya familia ili inapotokea mkopaji kufariki, kupoteza ajira au kuugua iwe rahisi wanafamilia kufuatilia na kulipa deni hilo.

Nkya ametoa changamoto hiyo kufuatia malalamiko ya mfululizo yaliyozifikia ofisi hizo, toka kwa baadhi ya akinamama ambao walifika kuomba msaada baada ya mali za familia kutaifishwa ghafya na kampuni zilizotoa mikopo baada ya mkopo kushindwa kurejesha.

Alisema kwa mujibu wa malalamiko yaliowafikia hivi sasa baadhi ya wanandoa, wanaume na wanawake wamekuwa wakichukua mikopo kwenye benki, makampuni na vikundi vinavyotoa mikopo na kuweka rehani kwa siri mali za familia bila kufahamisha wanafamilia.

Alisema inapotokea kushindwa kulipa deni mali zilizowekwa rehani huchukuliwa na kuuzwa kisheria kufidia deni, jambo linalosababisha familia hasa watoto kubaki wakitaabika kwa kukosa makazi na haki nyingine za msingi.

“Tunatoa angalizo hili kufuatia wanawake 12 waliofika katika ofisi zetu kati ya mwezi Oktoba mwaka jana na mwishoni mwa mwezi Machi mwaka huu wakilalamika kwamba familia zao zinakabiliwa na matatizo baada ya waume zao kuweka nyumba ya familia rehani kwa siri,” alisema.

Aliongeza kuwa mmoja wa wanawake hao alidai kuwa mahakama iliamuru nyumba yao iuzwe ili kufidia deni alilokuwa amekopa mume wake kwenye kampuni moja kabla ya kufariki kwa ajali.

“Mama huyo ambaye walikuwa pamoja na watoto wao katika ajali iliyomuua mume wake, alipata matatizo ya kiafya kwa miaka kadhaa ambayo yalimfanya ashindwe kufuatilia kesi mahakamani iliyohusu deni la mumewe na hivyo mahakama ikaamuru nyumba yao iuzwe,” alisema Nkya.

Aliongeza kuwa mama huyo alisema kwamba ingawa watoto walikuwa ni vijana ambao wangeweza kufuatilia hilo deni la baba yao walishindwa kufanya hivyo kwa sababu hawakuwa na mkataba wala kumbukumbu zozote za marejesho ya mkopo aliokuwa amechukua baba yao.

“Hivyo tunawashauri wanandoa kuwa wawe wazi kwa familia wanapoamua kuchukua mikopo iwe ni katika benki, makampuni au kwa mtu binafsi kwa kuhakikisha kwamba familia inakuwa inatambua na zinakuwa na taarifa kamili za maandishi kuhusu mikataba na marejesho ya mikopo hiyo,” alihimiza Mkurugenzi huyo Mtendaji wa TAMWA.