JK amteua Mkaguzi Mkuu ndani ya Serikali

Bw. Mohammed A. Mtonga

 

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Jakaya Kikwete amemteua Bw. Mohammed A. Mtonga (52) kuwa Mkaguzi Mkuu wa ndani wa Serikali.

Bw. Mtonga ni msomi mwenye Shahada ya Uzamili katika masuala ya Fedha (MSc in Corporate Finance) toka Chuo Kikuu cha Salford nchini uingereza.

Aidha Bw. Mtonga anayo Shahada ya Uhasibu ya CPA (T) inayotolewa na Bodi ya Taifa ya Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu (NBAA) na Stashada ya Juu ya Uhasibu (Advanced Diploma in Professional Accountancy) toka Chuo cha Jamii Nyegezi ambacho kwa sasa ni Chuo Kikuu cha Mt. Augustine cha Mwanza.

Kabla ya uteuzi huu, Bw. Mtonga amekuwa na utumishi wa miaka 32 katika Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi wa Heasabu ambapo amewahi kushika nyadhifa mbalimbali.

Nyadhifa alizowahi kushika Bw. Mtonga ni pamoja na Ofisa Masuuli na Mkaguzi wa Hesabu wa Kanda. Pia amewahi kuwa Mkaguzi wa Hesabu Mkazi katika mkoa wa Lindi, Wizara ya Nishati na Madini, Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa na Makao Makuu ya Jeshi (Ngome).

Uteuzi huu umeanza toka tarehe 06 Aprili, 2011.