Mwakyembe awaka

Dr. Harrison Mwakyembe

Siku chache baada ya kuanza kutumikia wadhifa wa Waziri wa Uchukuzi, Dk. Harrison Mwakyembe, amesema kuwa chanzo kikuu cha matatizo ya Shirika la Reli la Tanzania na Zambia (Tazara), ni uongozi mbovu.

Akizungumza na wafanyakazi wa Tazara makao makuu ya shirika hilo jana, Dk. Mwakyembe, aliwatangazia kwamba atahakikisha anatafuta muarobaini wa kumaliza matatizo yote sugu yanayolikabili bila kuogopa lolote, ikiwezekana hata kubadili mfumo wa kuendesha shirika hilo.

“Matatizo yanayoikumba Tazara ni uongozi mbovu. Hakuna Mtanzania wala Mzambia. Tupeni muda tuuhoji uongozi. Tutatafuta muarobaini wake. Mimi siogopi hata ikiwezekana kutenganisha operesheni za shirika. Hatuwezi kuendelea na makosa yale yale kila mwaka,” alisema Dk. Mwakyembe.

Katika mkutano huo ulioitishwa na Chama cha Wafanyakazi wa Reli Tanzania (Trawu) Kanda ya Dar es Salaam, ulikuwa mahususi kwa ajili ya kumweleza Waziri huyo ambaye aliongozana na Naibu wake, Dk. Charles Tizeba, matatizo sugu ya wafanyakazi na shirika hilo.

Dk. Mwakyembe, alisema miaka 30 iliyopita, jina la Tazara lilikuwa ‘huduma iliyotukuka’ ambayo alisema ilikuwa ikitolewa kwa wakati kiasi cha watu wanaohimizwa kutekeleza mambo kwa wakati kuwabatiza jina la “Tazara”.

Hata hivyo, alisema hali imekuwa tofauti kwa sasa na kuhoji zilikokwenda sifa hizo za Tazara na ‘mdudu’ gani aliyeingia katikati na kujibiwa na umati wa wafanyakazi waliofurika katika mkutano huo kwa kupaza sauti :“Ni hao hao”, wakimaanisha viongozi wa shirika hilo.

“Hata mimi huyo mdudu nimemuona. Nitamuondoaje? Nipeni muda. Hakuna Kiswahili tena, tutairejeshea Tazara heshima yake,” alisema Dk. Mwakyembe.

Alisema kuna haja ya kutenganisha baadhi ya mambo katika uendeshaji wa shirika hilo kati ya Tanzania na Zambia na kwamba, mchakato wa kufikia azma hiyo upo kabla ya kupeleka kwa Rais.

Dk. Mwakyembe alisema tatizo la Tazara mbali na uongozi, pia ni la kimfumo na kwamba, jambo kubwa lililomgusa ambalo atalifanyia kazi haraka, ni madai ya mabehewa ya treni ya shirika hilo baada ya kununuliwa yanapelekwa nje ya nchi baadaye yanaletwa nchini yakiwa chakavu.

Alisema kwa jinsi hali ilivyo mbaya Tazara, ni aibu kwa Rais kutembelea shirika hilo.

Aliwataka wafanyakazi wa Tazara kutoa taarifa kwake iwapo watasikia harufu ya mafisadi ambayo alisema kila anaposikia huhisi kutaka kutapika.

Katika kuonyesha kuwa yuko makini na hilo, alitoa namba yake ya simu ya mkononi na ya naibu wake na kuwapa wafanyakazi hao ili wawatafute iwapo watasikia harufu ya ufisadi na mafisadi katika Tazara.

Alisema kila atakayemuangalia mikononi, atashuhudia namna alivyopatwa na dhoruba ya maradhi ya ngozi yaliyomsibu, lakini alisema hilo limekwishapita, kwani amepona, hivyo ataendelea na kasi ile ile ambayo hata hivyo, hakuitaja.

Katika mkutano huo, Dk. Mwakyembe, alifanya kazi ya ziada kuwatuliza wafanyakazi hao walioanza kumzomea Naibu Mkurugenzi Mkuu wa Tazara, Damas Ndumbaro, alipojaribu kujibu swali la waziri huyo kama wafanyakazi walikwishalipwa mshahara wa Machi, mwaka huu au la.

Akiwatuliza wafanyakazi hao, Dk. Mwakyembe, alisema Ndumbaro ni mwanafunzi wake, hivyo akasema: “Naomba msimzomee.”

Kabla ya kukumbana na mkasa huo, Ndumbaro alisema kuwa hundi ya mwisho ya fedha za mishahara ya wafanyakazi ya Machi, mwaka huu, aliisaini Alhamisi wiki iliyopita na kumweleza Waziri Mwakyembe kuwa yuko tayari kumpa nakala ya hundi hiyo.

Baada ya kusema hayo, Ndumbaro, alianza kumwita Meneja wa Fedha wa Tazara ili alete mkutanoni hapo nakala ya hundi hiyo, lakini jitihada zake hizo hazikufanikiwa, kwani meneja huyo hakujitokeza.

Haikufahamika mara moja sababu za meneja huyo kutojitokeza mkutanoni hapo kuitikia wito wa bosi wake huyo.

Kutokana na hali hiyo, Dk. Mwakyembe, alimwamuru kwenda yeye mwenyewe (Ndumabaro) ofisini kwake kuileta nakala ya hundi hiyo ili aionyeshe mkutanoni hapo kuthibitisha madai yake.

Ndumbaro alitii amri hiyo na Waziri Mwakyembe, Dk. Tizeba na wafanyakazi walimsubiri kwa dakika kadhaa, lakini hakurejea mkutanoni.

Waziri Mwakyembe alipoona Ndumbaro anakawia kurejea mkutanoni, alijaribu kumpigia simu yake ya mkononi, lakini haikupatikana. Kutokana na hilo, Dk. Mwakyembe aliamua kumaliza mkutano huo.

Dakika chache, Ndumbaro, alirejea na kumkuta Waziri Mwakyembe akiwa tayari amekwishapanda gari lake kwa ajili ya kuondoka eneo hilo.

Dk. Mwakyembe alipomuona Ndumbaro, alishuka kwenye gari lake na kwenda kuangalia nakala za hundi hiyo na baada ya hapo aliaga na kuondoka eneo hilo.

Baada ya Dk. Mwakyembe kuondoka, Ndumbaro aliendelea kuwaonyesha waandishi wa habari na watu wengine nakala ya hundi hiyo.

Baadaye, aliwataka waandishi wa habari kuzungumza nao ofisini kwake, ambako alisema tatizo la Tazara siyo la mtu mmoja bali ni mfumo.

“Hakuna uongozi mzuri duniani kama mfumo ni mbovu. Uzuri wa kiongozi unatokana na mfumo mzuri,” alisema Ndumbaro.

Kutokana na hilo, alisema hawezi kujiuzulu kwa kuwa anayepaswa kuchukua hatua hiyo ni yule anayefanya kosa binafsi na kwamba hakuna mtu mwenye ushahidi kama anahusika na ubadhirifu wowote dhidi ya shirika hilo.

Awali, Katibu Mkuu wa Trawu, Erasto Kihwele, alimweleza Waziri Mwakyembe kuwa miongoni mwa matatizo yanayolalamikiwa na wafanyakazi, ni pamoja na kukosekana kwa mishahara toka Machi, mwaka huu, jambo ambalo alisema limewafanya wafanyakazi kuwa katika hali ngumu kimaisha.

Matatizo mengine, aliyataja kuwa ni Tazara kwa muda mrefu kushindwa kujiendesha kwa sababu ya ukosefu wa mafuta na kuiomba serikali kupitia Wizara ya Uchukuzi na Wizara ya Fedha kutoa udhamini kwa shirika hilo wa Sh. bilioni 8.5 ili kununua mafuta na vitendea kazi kwa miezi sita.

Kihwele alisema pia kuwa madai mengine ya wafanyakazi ni kutaka mkurugenzi mkuu na naibu wake wa Tazara waondolewe madarakani na kusisitiza kuwa fedha hizo zisitolewe hadi hapo viongozi hao watakapoondolewa kwenye nafasi zao.

Aliyataja matatizo mengine kuwa ni udhaifu wa Bodi ya Wakurugenzi wa Tazara na kuiomba serikali kuchukua hatua dhidi ya usimamizi mbovu wa bodi hiyo na kuundwa upya, ambayo pia ilidaiwa kuwa ni ya muda mrefu na imeshuhudia maovu yote ya Tazara yakitendeka pasipo kuchukua hatua.

Pia serikali ihakikishe soko la ndani linarejeshwa kwa ukamilifu kama vile mbao, mahindi, saruji, molasses, na karatasi za mgololo; kubana matumizi kwa kupunguza vikao vya bodi na kusitisha safari za viongozi wa Tazara zisizokuwa na tija.

Naye Dk. Tizeba alisema Tazara iko mahututi baada ya Kampuni ya Reli Tanzania (TRL) kuwa marehemu na kusema hata utaratibu uliopo wa makusanyo yote ya fedha za mapato ya Tazara kupelekwa kwanza Zambia na baadaye ndio yagawiwe nchini inabidi uangaliwe upya kwa kuwa hauna tija na umepitwa na wakati.

Aliahidi malalamiko ya wafanyakazi wa Tazara kwamba yatashughulikiwa, ikiwa ni pamoja na kuishirikisha Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) katika maeneo yote ya shirika hilo yanayodaiwa yana harufu ya ufisadi, yakiwamo yanayohusu mafuta, mabehewa na mizani.

CHANZO: NIPASHE