Jinamizi la wafuasi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), kukihama chama hicho limezidi kukiandama ambapo safari hii Kamanada wa vijana Kata ya Ilala jijini Dar es Salaam, Jaafar Juma ametangaza kuondoka na kundi la vijana na kujiunga na Chama Cha Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kwa madai ya kukerwa na uongozi wa Katibu Mkuu wa chama hicho, Wilson Mukama.
Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, Juma alisema amefikia hatua hiyo baada ya kuona kuwa Mukama ameshindwa kukisaidia chama na badala yake amekuwa mtu wa kusikiliza majungu, chuki na fitina dhidi ya makada wa chama hicho.
Juma ambaye pia ni mwenyekiti wa CCM kata ya Kariakoo jijini Dar es Salaam, alisema anaendelea kuwashawishi vijana katika maeneo anayoyaongoza kukihama chama hicho.
“Muda wowote nitavua gamba la CCM na kuvaa gwanda la Chadema kutokana na kuchoshwa na uongozi wa Mukama ambao umeshindwa kukijenga chama,” alisema.
Aliwatuhumu Mukama pamoja na Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye kwamba wanakipeleka chama mahali pabaya kwa madai kwamba kazi yao kubwa ni kusikiliza majungu na kuendeleza fitina ndani ya chama.
“Chama kimekosa mwelekeo kila kukicha wafuasi wake wanakihama na kujiunga na upinzani huku Mukama akishindwa kuchukua hatua zozote na mimi nipo tayari kuondoka na watu walio nyuma yangu,” alisema.
CHANZO: NIPASHE