SHIRIKA la Umoja wa Mataifa la Kudhibiti Matumizi ya Nishati ya Nyuklia (IAEA) limesema litaishinikiza Iran iwaruhusu wakaguzi kuingia kwenye kituo chake cha kijeshi, ambacho kinashukiwa kuwa na chumba maalum cha majaribio ya miripuko mikubwa ambayo inaweza kutumiwa kuunda silaha za nyuklia.
Iran ambayo imekana shutuma za nchi za magharibi kwamba inajaribu kuunda bomu la Atomiki, imekataa kuwaruhusu wakaguzi wa IAEA kukitembelea kituo cha kijeshi cha Parchin kilichoko kusini mashariki mwa mji mkuu, Tehran.
Suala hilo linategemewa kuzungumziwa katika mkutano baina ya IAEA na Iran, ambao unafanyika leo na kesho mjini Vienna, Austria. Katika ripoti yake ya mwezi Novemba, Shirika la IAEA lilisema kuwa mwaka 2000.
Iran ilijenga kituo cha majaribio ya miripuko mikubwa, na kusema hiyo ni ishara ya uwezekano wa kuunda bomu la nyuklia. IAEA imsema inazo picha za satelaiti kuthibitisha madai hayo.
-DW