VITENDO vya baadhi ya wazazi katika wilaya ya Mwanga mkoani Kilimanjaro kuwaficha ndani watoto wenye ulemavu, vimeelezewa kuwa tatizo kubwa ambalo linaweza kukwamisha zoezi la sensa ya watu na makazi linalotarajiwa kufanyika Agost 26 mwaka huu.
Vitendo hivyo ambavyo vinachangiwa na mila na desturi potofu vimekuwa vikisababisha watoto wenye ulemavu kukosa haki zao za kimsingi ikiwemo elimu.
Hayo yamebainishwa na Ofisa Elimu Maalumu wilaya ya Mwanga Bi. Ester Kaaya wakati wa warsha ya elimu jumuishi kwa walimu wa shule za msingi wilayani humo ambapo alisema vitendo vya wazazi kuwaficha watoto wenye ulemavu bado ni changamoto kubwa wilayani humo.
Alisema kutokana na mila potofu juu ya watoto wenye ulemavu zilizojengeka miongoni mwa jamii wilayani humo zoezi la sense ya watu na makazi kwa kundi hilo halitafanikiwa kama ilivyokusudiwa.
“kutokana na wazazi wenye watoto wenye ulemavu kuwaficha watoto wao majumbani kwa kuogopa wasionekane na watu, hii itamnyima haki mtoto huyo kuhesabiwa na hivyo kukwamisha zoezi la uhesabuji watu na makazi hapa nchini,” alisema Bi. Kaaya.
Aidha alisema ili kuweza kufanikiwa katika zoezi hilo serikali haina budi kuwashirikisha viongozi kuanzia ngazi ya vitongoji,vijiji na hata kata kuanzia hatua za mwanzo kutokana na kwamba ndiyo wanaozifahamu nyumba zenye watoto wnye ulemavu.
Awali akizungumza katika warsha hiyo Ofisa elimu ya msingi wilayani Mwanga, Said Mderu alikiri kuwepo kwa Tatizo la watoto wenye ulemavu kufichwa na kwamba kuna haja ya jamii kuelimishwa zaidi ili kuondokana na tatizo hilo.
“kitendo cha mzazi kumficha mtoto ndani kutokana na ulemavu wake ni suala ambalo linapaswa kukemewa vikali kwani halifai katika jamii na si la kufumbiwa macho ni lazima lipigwe vita ili makundi haya yaweze kupata haki zao,” alisema.
Kwa upande wake mwenyekiti wa jumuiya ya watu wenye ulemavu wailayani humo, Gustav Mkekanule ameiomba tume iliyoundwa ya kuratibu zoezi la ukusanyaji wa maoni ya katiba mpya kuhakikisha kuwa inawafikia na watu wenye ulemavu ili nao waweze kutoa maoni yao ambayo wanataka yawepo kwenye katiba mpya.
Aliwataka walemavu wote nchini kujitokeza katika zoezi la utoaji wa maoni ya uundwaji wa katiba mpya hatua ambayo itawezesha kupatikana kwa katiba yenye kukidhi matakwa ya watu wote wakiwemo na walemavu.
Baadhi ya washiriki wa warsha hiyo walisema vitendo vya wazazi kuwaficha watoto wenye ulemavu havipaswi kufumbiwa macho tena na kuiomba serikali kuwachukulia hatua kali watu watakaobainika kufanya vitendo hivyo ambavyo ni vya kikatili na kuhakikisha makundi hayo yanapata haki zote za kimsingi ikiwemo elimu.