Polisi wamtwanga risasi ‘jambazi’

Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, IGP-Said Mwema

Na Thomas Dominick wa Binda News-Musoma

MTU mmoja anayejulikana kwa jina la Duke Mkama (27) Mkazi wa Kijiji cha Katario, Tarafa ya Makongoro, Musoma Vijijini Mkoa wa Mara anayedaiwa kuwa jambazi wa kutumia silaha amepigwa risasi mguu wa kulia akijaribu kuwakimbia askari polisi waliokwenda kumkamata.

Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake jana, Kamanda wa Polisi wa Mkoa huo, Robert Boaz alisema kuwa tukio hilo lilitokea Mei 09 mwaka huu, mtuhumiwa huyo ameshiriki katika matukio mbalimbali ya unyang’anyi wa kutumia silaha na alikuwa anatafutwa tangu siku nyingi.

“Baada ya kupata taarifa kuwa mtuhumiwa huyo ameonekana katika kijiji hicho askari walienda kwa lengo la kumkamata ili kufikishwa chini ya sheria lakini alichomoa sime kwa lengo la kuzuia wasimkamate na alifanikiwa kukimbia ndipo askari walimpiga na risasi katika paja la kulia na kumkamata,”alisema Kamanda Boaz.

Kamanda Boaz alisema kuwa mtuhumiwa huyo kwa sasa yupo katika Hospitali ya Mkoa huo akiuguza majeraha yake na pindi atakapo pata nafuu atahojiwa na kufikishwa mahakamani ili kujibu tuhuma zinazomkabili.

“Kwa sasa amelazwa katika hospitali ya mkoa chini ya ulinzi tunasubiria apate nafuu ili tuanze kumuhoji na kuwatambua wenzake wengine ili tuwakamate na kuwafikisha mahakamani kwa ajili ya sheria ifuate mkondo wake,” alisema.

Kamanda Boaz ametoa onyo kwa wale wote wanaojihusisha na ujambazi wa kutumia silaha kuacha mara moja na kusalimisha silaha wanazozimiliki kwa tayari jeshi hilo limejipanga kuwakamata wote baada ya wananchi kuanza kupata mwamko wa kuwataja watuhumiwa hao.