Wataka mawaziri wafilisiwe

Katibu Mkuu wa UVCCM, Martin Shigela

Sasa kampeni inapigwa ili mali za mawaziri waliofutwa kazi zifilisiwa kama watakutwa na hatia mahakamani.
Huo ni wito wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM), wakitaka wote waliotajwa katika ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kuhusika na kufuja mali za umma wachukuliwe hatua za kisheria ikiwa ni pamoja na kufilisiwa mali zao.

Kauli hiyo ilitolewa na Katibu Mkuu wa UVCCM, Martin Shigela, wakati akiwahutubia wanachama wa chama hicho kutoka katika vyuo mbalimbali vya mjini Dodoma walioandamana kuunga mkono hatua ya Rais Jakaya Kikwete kulifanyia mabadiliko baraza la mawaziri.

Rais Kikwete alitangaza mabadiliko ya baraza la mawaziri Ijumaa iliyopita na kuwaapisha Jumatatu wiki hii.
“Kupitia katika vikao vyetu vya wilaya, halmashauri, jiji na manispaa, wote wanaohusika na hujuma na kufuja mali za umma wachukuliwe hatua, wafikishwe katika vyombo vya sheria na ikiwezekana wahukumiwe na mahakama zetu waweze kufilisiwa ili kurudisha zile mali,” alisema Shigela na kushangiliwa na wanavyuo hao.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Wazazi wa Chama hicho, Hamis Dadi, alimpongeza Rais Kikwete, kwa jinsi alivyochukulia mapendekezo ya wabunge wa CCM ambao waliazimia kuwa waliotajwa katika ripoti ya CAG hususan mawaziri wawajibishwe.

Dadi naye aliitaka serikali kufanya uchunguzi na kuwafikisha mahakamani bila kujali nafasi zao.
Alisema nchi ina hazina ya viongozi waadilifu, wenye busara, waaminifu na makini na kuongeza kuwa walioteuliwa kuwa mawaziri wana sifa hizo.

“Ninahakika (Rais Kikwete) analichukulia suala la hili kwa umakini na itafika wakati atachukua hatua zinazofaa,” alisema Dadi.

Katika mabadiliko hayo, Rais Kikwete aliwaacha nawaziri sita na manaibu mawaziri wawili.

Wengine walioguswa na ripoti ya CAG na ripoti za kamati za kudumu za Bunge za Hesabu za Serikali (PAC), Hesabu za Mashirika ya Umma (POAC), na Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC), ni aliyekuwa Tamisemi, George Mkuchika na aliyekuwa Kilimo, Chakula na Ushirika, Profesa Jumanne Maghembe. Hata hivyo, Rais Kikwete aliwahamisha Ofisi ya Rais (Utawala Bora) na Profesa Maghembe Wizara ya Maji.

Walioachwa ni Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Hadji Mponda; Waziri wa Uchukuzi, Omar Nundu; Waziri wa Fedha, Mustafa Mkulo; Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja; Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk. Cyril Chami na Waziri wa Maliasili na Utalii, Ezekiel Maige.

Manaibu mawaziri walioachwa ni Dk. Lucy Nkya (Afya na Ustawi wa Jamii) na Athuman Mfutakamba (Uchukuzi).

Mustafa Mkulo, alidaiwa kuhusika katika ubadhirifu wa Shirika Hodhi la Mali za Mashirika ya Umma (CHC). Alitajwa kuwa amepotea uaminifu na uadilifu kiasi cha kusema uongo bungeni ili kuficha maslahi binafsi katika ofisi za umma.

Dk. Chami, alitajwa kuhusika katika kumkingia kifua Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Viwango la Taifa (TBS), Charles Ekelege, kutokana na kusema uongo katika kazi ya ukaguzi wa magari nje ya nchi.

Ekelege anadaiwa kusema uongo kuwa kuna kampuni zimepewa kazi ya kukagua magari yanayokuja nchini nje ya nchi, ambayo yanalipwa mamilioni ya fedha, lakini kamati ya wabunge iliyokwenda nchi za Singapore na Hong Kong, hawakukuta kampuni hizo.

Dk. Mponda, anadaiwa kushindwa kusimamia matumizi bora ya fedha za umma kiasi cha kuruhusu nyumba yake kukarabatiwa kwa mamilioni ya fedha.

Mkuchika, anadaiwa kushindwa kusimamia fedha katika halmashauri mbalimbali nchini ambako ufisadi wa kuwango kikubwa umegundulika.

Ngeleja, anayetuhumiwa kwa kushindwa kusimamia sekta ya madini na umeme, kuweko kwa manunuzi makubwa ya mafuta ya kuendesha mitambo ya IPTL ambayo yameongezwa bei.

Maige, atauhumiwa kushindwa kudhibiti ubadhirifu katika wizara yake kama ulivyobainika katika ugawaji wa vitalu vya uwindaji wa kitalii na usafirishaji wa wanyama hai nje ya nchi.

Nundu, anatuhumiwa kuingilia mchakato wa kumpata mzabuni wa kujenga gati namba 12 na 13 katika Bandari ya Dar es Salaam.

Profesa Maghembe, anadaiwa kushindwa kudhibiti ununuzi wa pembejeo na ulipaji wa fedha za mdororo wa uchumi.

CHANZO: NIPASHE