Na Mwandishi Maalumu
RAIS wa Tanzania, Jakaya Kikwete amesema Tanzania haina tatizo na Muungano wa Kisiasa wa Afrika Mashariki ili mradi huo Muungano huo uanzishwe baada ya kutimizwa kwa hatua nyingine zote muhimu za ushirikiano baina ya nchi wanachama wa Jumuia ya Afrika Mashariki (EAC).
Aidha, Rais Kikwete amesema Tanzania haiwezi kuwa na tatizo na Muungano huo kwa sababu Taifa la Tanzania lenyewe ni matokeo ya muungano wa nchi mbili za Tanganyika na Zanzibar na ina uzoefu na miungano ya kisiasa.
Rais Kikwete alitoa ufafanuzi huo wakati alipokutana na kufanya mazungumzo na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Biashara Duniani la World Trade Organisation (WTO), Paschal Lamy kwenye Hoteli ya Sheraton, Addis Ababa, Ethiopia usiku wa jana, Alhamisi, Mei 10, 2012.
Wote wawili walikuwa mjini Addis Ababa kuhudhuria mkutano wa mwaka huu wa Jukwaa la Uchumi Duniani, Kanda ya Afrika (World Economic Forum on Africa-WEF-Africa) ambao umemalizika leo, Ijumaa, Mei 11, 2012 ukiwa umefanyika Ethiopia kwa mara ya kwanza.
Rais Kikwete alitoa ufafanuzi huo baada ya Bwana Lamy kutaka kujua maendeleo ya Jumuia ya Afrika Mashariki ambayo wanachama wake ni Tanzania, Kenya, Uganda, Burundi na Rwanda.
Rais Kikwete alimwambia Bwana Lamy: “Kama unavyojua, Tanzania ni muumini mkubwa wa ushirikiano na umoja wa Afrika. Tunahitaji kuungana ili kuongeza nguvu zetu na ndiyo maana nchi yetu ni muumini mkubwa wa Jumuia ya Afrika Mashariki na misingi ya uendeshaji wake.”
Aliongeza Rais Kikwete: “Aidha, tofauti na hisia za watu wengine, Tanzania haina tatizo kabisa na kuanzishwa kwa umoja wa kisiasa, yaani Muungano wa Kisiasa. Tunalipenda jambo hili, isipokuwa tunaamini kwa dhati kuwa ili muungano huo uwe imara na wenye utulivu wa kutosha ni muhimu kwanza kukamilisha hatua nyingine zote muhimu za ushirikiano baina ya nchi zetu. Tukikamilisha hatua hizo, naamini kuwa tutakuwa tumepata uzoefu wa kutosha wa ushirikiano na tutakuwa tayari kuwa na umoja wa kisiasa wenye nguvu kabisa.”
Aliongeza Mheshimiwa Rais Kikwete: “Tanzania kamwe haiwezi kuwa na tatizo na Muungano wa Kisiasa kwa sababu nchi yetu yenyewe ni matokeo ya kuungana kwa nchi mbili – Tanganyika na Zanzibar. Hivyo, kwa maana hiyo, Tanzania ina uzoefu wa miaka 48 wa kuishi katika Muungano wa Kisiasa. Huu ni uzoefu mkubwa.”
Rais Kikwete na ujumbe wake amerejea nchini jioni ya leo na kabla ya kuondoka mjini Addis Ababa, Rais Kikwete amekutana na kufanya mazungumzo na Mwenyekiti wa WEF, Profesa Klaus Schwab na Makamu Mwenyekiti, Bibi Josette Sheeran.