Ajali; Wawili wafa 28 wajeruhiwa Iringa

Gari lililpata ajali

Francis Godwin
Iringa

WATU wawili wamekufa papo hapo na wengine 28 kujeruhiwa vibaya baada ya fuso lenye namba za usajili T115 ANZ walilokuwa wakisafiria kwenda Mnadani Pawaga Iringa kupinduka.

Ajali hiyo imetokea majira ya saa 1 asubuhi leo katika Milima ya umasaini barabara kuu ya Iringa -Pawaga wakati wafanyabiashara hao zaidi ya 50 wakielekea mnadani huku chanzo cha ajali hiyo kikidaiwa kuwa ni uzembe wa dereva ambaye alikuwa akilazimisha kuendesha gari hilo pamoja na kuonyesha matatizo ya bleck kabla ya kuanza kushuka mteremko wa Milima ya umasaini.

Baadhi ya wafanyabiashara walionusurika katika ajali hiyo walimweleza mwandishi wa habari hizi aliyefika eneo la tukio kuwa lori hilo lilianza kusumbua na kufeli bleck, kabla ya kuanza kushuka mteremko huo hali iliyopelekea dereva na utingo wake kushuka na kujaribu kutengeneza bila mafanikio na kuamua kuliendesha bila bleck ili kuwawahisha wafanyabiashara hao mnadani huku wakidai kuwa litafika na kufanyiwa matengenezo mnadani.

Hata hivyo walisema baada ya kuliondoa lori hilo lilianza kushuka kwa kasi kubwa mteremko huo hali iliyopelekea wafanyabiashara kuanza kutaharuki ndani ya lori hilo na baadhi yao kujaribu kuruka kabla ya lori hilo kumshinda dereva huyo na kupinduka.

Abiria hao walisema kuwa dereva huyo alionyesha hofu zaidi baada ya kuona mbele yake kuna karavati la maji machafu na kuamua kulitoa lori hilo nje ya barabara na kupinduka huku likiwa tayari limemaliza mteremko huo likiwa katika mwendo kasi.

Kamanda wa polisi wa mkoa wa Iringa Evarist Mangalla, amethibitisha kutokea kwa ajali hiyo na kuwataja waliofariki kuwa ni Jokonia Kihape na Omari Maburuki wote ni wafanyabiashara.

Majeruhi wa ajali hiyo ni pamoja na Vicent Mtewele(20), Stella Nditu(36), John Magubika(45), Chusi Kalinga (22), Evance Ngonyani(31), Wenslaus Njovu(37)Edina Sanga(30), Yassin Alipha(30), Deo Benidict(40) na Ayoub Nzelu(23).

Wengine ni Allen Kisava(22), Erasto Lusungu(25), Emmanuel Mtunye(25), Anthony Kaguo (31), Mengi Kulwa(31), Ally Martine(55), Bony Mwakatebe, Antony Msingi(36), Anania Mkuye(52).

Majeruhi wa ajali hiyo wote wamelazwa katika hospitali ya mkoa wa Iringa huku baadhi yao wakiwa wameumia vibaya kichwani, miguu, mikono na mbavu.