Tanzania yapata uwakilishi katika Bunge la Marekani

Balozi Mwanaidi Sinare Maajar akiwa na Dan Boren, Mbunge wa Bunge la Marekani kutoka Oklahoma. (Picha zote kwa hisani ya Ubalozi wa Tanzania nchini Marekani)

Balozi Maajar akiwa katika picha ya pamoja na Mbunge Dan Boren,

Na Mwandishi Wetu, Washington DC

NCHI ya Tanzania sasa imepata uwakilishi katika Bunge la Marekani baada ya kujitokeza mbunge mwenye mapenzi mema na Tanzania na kuanzisha Kamati ndogo (Caucus) ya wabunge wakiitetea Tanzania ndani ya Bunge hilo.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Balozi wa Tanzania nchini Marekani na Mexico, Mwanaidi Sinare Maajar, Mei 9, 2012 alimpokuwa akifanya mazungumzo na Mbunge wa Marekani kutoka Jimbo la Oklahoma, Dan Boren alisema tayari amehamasisha na kupata wabunge marafiki wa Tanzania watakaoisemea juu ya masuala anuai.

Katika mazungumzo hayo Mbunge Boren ambaye ni kutoka Chama Tawala cha Democrat alimueleza Balozi Maajar kuwa amehamasisha na hatimaye kuanzisha kundi la wabunge wenye mapenzi na Tanzania, ambayo ni kamati ndogo ya kuisemea Tanzania kwenye Bunge la Marekani.

Aidha Boren aliongeza kuwa ameasisi kundi hilo akishirikiana na wabunge wenzake kadhaa wa chama chake na wengine kutoka Chama cha Republican baada ya kufurahishwa kwao na juhudi za Serikali ya Rais Jakaya Mrisho Kikwete katika kuimarisha demokrasia, utawala bora pamoja na juhudi za kimaendeleo katika sekta za uchumi, nishati, kilimo na hifadhi ya mazingira.

Katika ziara hiyo kwa Ubalozi wa Tanzania, Boren akiambatana na Bi. Hilary
Moffett, Mkurugenzi wa Sheria Bungeni, alimhakikishia, Balozi Maajar
utayari wake wa kuisaidia Tanzania katika juhudi zake hizo.

Hata hivyo alieleza kwamba Tanzania ina changamoto nyingi sana mbele yake na
hivyo kuwepo kwa sauti mpya ya kuisemea katika Bunge la Marekani ni jambo
ambalo analiona litakuwa na manufaa makubwa kwa nchi.

Sambamba na hilo, Boren alibainisha Tanzania imekuwa ni moja ya nchi ambazo Serikali ya Marekani inaziangalia kwa umakini kama mfano wa nchi bora na hivyo ameona ni vyema naye akaunga mkono juhudi hizo za Serikali ya Rais Barack Obama.

Kwa upande wake, Balozi Sinare Maajar alifurahishwa na kufarijika na ujio wa Boren Ubalozini na kumueleza kwamba atashirikiana naye bega kwa bega na kuahidi kwamba muda wowote atakapohitajika kukutana na kamati hiyo ya Bw. Boren yupo tayari.

Maajar alimshukuru, Boren kwa mwaliko wake kutembelea Jimbo la
Oklahoma ili Tanzania ipate kueleweka zaidi na hivyo kufungua pazia la
ushirikiano katika sekta mbali mbali za Uchumi, Kilimo, Nishati na Utalii.