HALI YA UWAJIBIKAJI NCHINI; JE KATIBA MPYA ITALINDA RASILIMALI ZA TAIFA?

HALI YA UWAJIBIKAJI NCHINI; JE KATIBA MPYA ITALINDA RASILIMALI ZA TAIFA?

UTANGULIZI:

A) HALI YA UWAJIBIKAJI NCHINI
Tunapoangalia dhana mzima ya kuwajibikaji lazima tuangalie pande zote mbili kati ya viongozi kwa maana ya (watawala) na wananchi kwa maana ya (watawaliwa). Kwa lugha nyepesi kuwajibika ni kutimiza wajibu wako ipa. Viongozi wana wajibu wao kama watawala na wananchi wana wajibu wao kama watawaliwa.
Miongoni kwa mambo makuu ambayo mwananchi anawajibika kuyafanya ni kama kilipa kodi, kutii sheria za nchi, kudumisha amani. Kwa upande wa viongozi, wao wanapaswa kuwahudumia wananchi wao, kusimania hutekelezaji wa sheria za nchi, kuretea maendeleo wananchi na kulinda rasilimali za nchi.
Hili viongozi waweze kufanya kazi zao hupaswa kujiwekea miiko maadili na taratibu za kuendesha nchi. Taratibu hizi huwekwa kwenye Katiba na miongozo ya nchi husika. Tunapoangalia suala la uwajibikaji hasa kwa viongozi hapa nchini Tanzania tunaweza kusema viongozi wetu hawawajibiki ipasavyo.

Hii inaweza kubainishwa na ripoti zitolewazo kila mwaka na mdhibiti na mkaguzi mkuu wa hesabu za serikali na hasa ripoti ya sasa iliyotolewa mwezi uliopita pamoja na ripoti tatu za kamati ya bunge.

Katika ripoti hizi zimebaini matumizi mabovu ya rasilimali za nchi katika washirika ya serikali, Serikali za mitaa na serikali kuu. Ripoti zionyesha ulipaji wa mashahara hewa, upotevu wa rasilimali za nchi kwa kutoa misamaha ya kodi, kuingia mikataba mibovu na wakati mwingine mikataba huingiwa na makampuni hewa nk.

Hebu sasa tuangalie baadhi ya maeneo ambayo yameonyesha kuwa sugu katika suala zima la uwajibikaji hapa nchini Tanzania;

1. Ufuatiliaji wa maadili ya uongozi
Uwajibikaji kwa viongozi kutaja mali zao kabla ya kuwa viongozi na baada ya kuondoka katika uongozi limekuwa ni suala gumu. Viongozi walio wengi wamekuwa wagumu kuweka wazi mali zao.

2. Kulinda rasilimali za nchi
Uwajibikaji katika suala zima la kuwa na uwazi katika madini, mafuta na gesi hii ni pamoja na kuweka wazi mikataba na kuhakikisha rasililimali zinawanufaisha wananchi. Kumekuwa na ugumu sana katika suala hili kwani kumekuwa na migogoro mikubwa sana hususani katika uwepo wa uwazi wa rasilimali, mikataba na katika maeneo mengi rasilimali haziwanufaishi wananchi hivyo uwajibikaji katika suala hili umekuwa mgumu sana.

Mfano; Mkutano wa mwaka huu wa BARRICK GOLD MINE uliofanyika Torornto Nchini Kanada mnamo tarehe 3 Mei 2012 ulimzuia Mwanaharakati wa Haki za Binadamu Bw. Amani Mustapha Mhinda ambaye pia ni Mkurugenzi wa asasi ya kijamii HAKI MADINI, inayoshughulika na haki za binadamu katika maeneo ya machimbo ya madini.

Mhinda alikuwa amedhamiria kueleza wahudhuriaji wa Mkutano huu kuhusu umuhimu wa kujenga uwezo wa wachimbaji wadogo na jamii zinazoishi katika maeneo ya machimbo, ili ziweze kunufaika na rasilimali ya madini ya Tanzania, pamoja na kulinda na kutetea haki zao, ambayo pia ilikuwa ni agenda kuu ya HAKIMADINI yenye makao yake makuu mjini Arusha

Hata hivyo pamoja na kuwa na ajenda hiyo, Barrick Gold Mine na uongozi wake walimzuia kuingia katika eneo la mkutano huo ingawa alikuwa na uhalali wa kuhudhuria mkutano huo kutokana na matukio ya uvunjwaji wa haki za binadamu yanayofanywa na makampuni ya uchimbaji

Hatua ya kumzuia iliyochukuliwa na Barrick inaonesha wazi juhudi za kuficha uvunjwaji wa haki za binadamu unaofanywa na makampuni ya uchimbaji na wawekezaji wengine kwa jamii za kitanzania.

Mfano; Namna wananchi wa North Mara wanavyoishi katika mazingira magumu na walivyodhurika na mgodi wa Barrick Gold Mine. Mito na mabwa wanayotumia kwa ajili ya mahitaji yao kuchafuliwa na kemikali zinazotokana na mgodi huo. Hata hivyo suala hili bado ni tete. Uwajibikaji wa viongozi na tendaji wengine wa serikali ili kulinda haki za wananchi haupo na madai ya wananchi yanapuuzwa kwa makusudi.

3. Uwajibikaji kwa viongozi wa nchi
Suala hili limekuwa kikwazo sana kwani viongozi walio wengi hawawajibiki ipasavyo kwa wananchi kutokana na kujilimbikizia mali, kutotimiza ahadi (ahadi hewa). Kumekuwa na ufujaji mali za wananchi na kuwaacha wananchi walio wengi wakiwa masikini na wao wakijinufaisha. Mfano ; ni masuala ya ufisadi yaliyojitokeza na yanayoendelea kujitokeza kama Richmond na Radar.

Vile vile Mihimili mitatu (Dola, Mahakama, Bunge) kutoingiliana kikazi pia ni suala la kuonesha uwajibikaji kwani kila muhimili inabidi ufanye kazi yake bila kuingilia muhimili mwingine na si hivyo tu kufanya maamuzi yake bila kutegemea muhimili mwingine.
Hata hivyo mihimili hii imekuwa ikiingiliana, kutegemeana na hata muhimili mmoja kufanya kazi ya mwingine na mpaka kufanya maamuzi ya muhimili mwingine suala linaloonesha udhaifu mkubwa katika uwajibikaji.
i) Dola; kitendo cha serikali kufanya maamuzi ya bunge ni kuingilia kazi zake mfano; “Serikali ilitumia sh 544 bilioni bila kuidhinishwa na bunge, sh 1 bilioni zimelipwa mishahara kwa watumishi hewa na sh 3 bilioni zimetumika katika Balozi za Tanzania nje ya nchi ambazo ziko nje ya bajeti iliyoidhinishwa na Bunge”.
ii) Mahakama
Maamuzi ya mahakama yamekuwa yanaingiliwa na dola,kwa mfano mahakama kuu ilitoa maamuzi ya kuruhusu mgombea binafsi mara tatu lakini mara zote serikali imekuwa ikikataa kuyatekeleza. Pia kuna kesi ya muda mrefu ambayo mfanya biashara ajulikanaye kwa jina la bwana Vallambia aliyeishitaki serikali kwa kukataa kumlipa pesa kulingana na makubaliano ya kibiashara aliyofanya na serikali .Kwa mara zote amekuwa akishinda kesi laKini serikali haimpi haki yake hadi leo. Hiyo ni baadhi miongoni kwa kesi nyingi ambazo serikali imekuwa ikiingilia maamuzi yake.
iii) Bunge; rais amekuwa akitegemewa sana katika kufanya maamuzi hasa na bunge ambalo huwa na wajibu wa kufanya maamuzi juu ya jambo fulani, mfano suala la CAG kuwasilisha taarifa ya viongozi wasio wawajibikaji halikuhitaji kuthibitishwa na rais. Bunge lilipaswa kufanya kazi yake mpaka mwisho si mpaka raisi kutoa kauli yake kuthibitisha suala hilo.

Si kwamba serikali haifanyi juhudi binafsi katika suala la uwajibikaji, ushahidi wa juhudi hizo unajionesha katika ripoti mbali mbali za CAG za miaka iliyopita kwa kuangalia uwajibikaji nchini, hata hivyo kwa kutumia ripoti ya CAG ya mwaka huu mwaka 2012 kama iliyoandikwa na gazeti la Mwananchi la (April 13/ 2012) CAG aaniika ufisadi wa kutisha serikalini (Mwandishi: Daniel Mjema na Aidan Mhando)
Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Ludovick Utouh jana aliwasilisha ripoti yake bungeni inayoonesha kuendelea kuwapo kwa ufisadi wa kutisha serikali huku deni la taifa likiongezeka kutoka sh 10.5 trilioni mwaka juzi na kufikia sh 14.4 trilioni mwaka jana.
Serikali imetumia sh 544 bilioni bila kuidhinishwa na bunge, sh 1 bilioni zimelipwa mishahara kwa watumishi hewa na sh 3 bilioni zimetumika katika Balozi za Tanzania nje ya nchi nje ya bajeti iliyoidhinishwa na Bunge.
Deni la Taifa limeongezeka kutoka sh 10.5 trilioni mwaka wa fedha wa 2009/2010 hadi kufikia sh 14.4 trilioni mwaka 2010 sawa na ongezeko la asilimia 38.
Vile vile gazeti la Mwananchi la (Mei 07/ 2012)
CAG: Mawaziri wapya wakicheza watang’oka; asema atawakagua na kutoa ripoti katika vipindi vitatu, vigogo wengine “wapumulia mashine” (Mwandishi: Boniface Meena)
Mdhibiti mkuu wa Hesabu za Serikali, (CAG) Ludovick Utouh amewaonya mwaziri wapya na watendaji serikalini kuwa ripoti zake zina nguvu ya kusimamia uwajibikaji, hivyo basi wanapaswa kusimamia vyema wizara zao kuzuia ubadhirifu wa fedha za umma. Hii ni kauli iliyotolewa baada ya kuwangoa mawaziri sita katika wanane ambao wizara zao zilionekana kugubikwa na ufisadi wa mali za umma.

B) JE, KATIBA MPYA ITALINDA RASILIMALI ZA NCHI?
Wakati nchi yetu inapojipanga kuingia katika mchakato wa kuandika Katiba mpya kumekuwa na matarajio na misisimko mingi ya wananchi wakionyesha matarajio yao ya kundokana na hali ngumu ya maisha na maendeleo ya nchi kwa ujumla iwapo nchi itafanikiwa kuandika Katiba mpya. Tumeshuhudia taasisi mbalimbali zikitoa maneno yenye kuamasisha wananchi kushiriki katika zoezi hili wakitoa kauli mbiu yao yenye maneno yasemayo KATIBA MPYA NI JIBU.
Hamasa hii iliibua mjadala mkali wa makundi yaliyotofautiana kimantiki kwa kauli mbiu iliyotolewa wakidai kuwa KATIBA MPYA NI JAWABU na si JIBU. Tofauti hizi zililenga kujenga zaidi kuliko kubomoa.

Tofauti ya maneno haya mawili ambayo ni JIBU na JAWABU ilinalenga hasa kuufanya mchakato huu kufanyika kwa umakini na hatimaye kuzaa matokeo yanayotegemewa na watanzania yatakayotokana na matunda ya Katiba mpya. Kwa watanzaia walio wengi, hali ngumu ya maisha, ufisadi, kukosekana kwa ajira, kutowajibika kwa viongozi , rushwa na ufujaji wa rasilimali za taifa ni matokeo ya Katiba tuliyo nayo kutokidhi haja.
Hivyo basi mategemeo ya wananchi ni kuwa Katiba mpya itakuwa mkombozi wao kwa kuwa itaweka misingi imara ya kutatua kero hizi zote kwa maana nyingine itatoa jawabu.

Mjadala ulibaini kuwa wanaosema Katiba mpya ni jibu wanatoa majibu mafupi kwa maswali magumu kama ilivyo Katiba ya sasa. Pia wao wanaamini kuwa jibu linaweza kuwa sahihi au sio sahihi kwa kuwa huwa haliitaji kufikiri zaidi ukiringanisha na jawabu ambalo hupatikana baada ya kupitia njia ndefu inayoonyesha mtiririko mzima uliokufikisha kwenye jawabu.

Katiba ya sasa tuliyo nayo imekuwa ikitoa majibu kwa maana kuwa ilitumia njia fupi kupata majibu mazito. Watanzania wanataka Katiba yenye kutoa jawabu la matatizo, dukuduku na kuweka utaratibu sahihi wa kungoza nchi utakaotokana na ridhaa ya watu wenyewe.
Katiba ya kudumu ya mwaka 1977 imefanyiwa marekebisho mara kumi na nne na yote yalilenga hasa kuweka marekebisho yaliyosaidia kutunga sheria za kuwawezesha watawala kuweka mifumo na taratibu za kuwasaidia kutawala watanzania kwa maslahi yao na sio kutatua kero za watanzania. Pia baadhi ya marekebisho katika Katiba yetu yamefanyika ili kukidhi au kuridhia matakwa ya sheria za kimataifa.

NINI MAANA YA KATIBA?
Katika kujadili mada hii inabidi kujiuliza hasa Katiba ni kitu gani?

A) Kwanza, Katiba ni waraka wa kisiasa unaowawezesha wananchi kujitambua kama taifa.
B) Ni waraka wa kiutawala unaoeleza mgawanyo wa madaraka na majukumu ya vyombo mbalimbali vya dola.
C) Ni waraka wa kisheria unaoongoza shughuli zote kisheria ambao ndio chimbuko la sheria zote nchini.
D) Ni muafaka wa kitaifa juu ya namna ya kuendesha nchi.
Katiba inatakiwa kukidhi vigezo vyote vilivyo tajwa hapo juu. Katiba ya sasa imekuwa na upungufu wa kigezo cha mwisho ambacho ni Katiba kupata muafaka wa kitaifa.

Tunapoangalia tafsiri tatu za maana ya Katiba hapo juu, tunaona ulindwaji wa maslahi ya mihimili mikuu ya utawala wa nchi katikaKatiba. Mihimili hiyo ambayo ni; Dola, Mahakama na Bunge Maana zote tatu za mwanzo katika tafsiri ya maana ya Katiba zinaonyesha na kuitambua mihimili hiyo. Katika Katiba ya jamuhuri ya muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 tunashindwa kuona ni kwa namna gani mihimili hii imelinda maslahi ya kila muhimili kutoingilia muhimili mwingine. Tumeshuhudia mahamuzi ya mahakama yakiingiliwa na dola, na mfano mzuri ni wa kesi ya mgombea binafsi, kesi ya madai ya mfanya biashara maarufu mr. Vallambia ya tangu miaka ya 1990 dhidi ya serikali ambayo mfanya biashara mara zote amekuwa akishinda kesi hiyo bila mafanikio na nyingine nyingi.

MISINGI YA KATIBA;
Katika nchi zenye kufuata demokrasia misingi mkuu wa Katiba ni ule unaoweka mamlaka yote mikononi mwa wananchi na misingi mingine ni
a) Katiba kuwezesha wananchi wake kuridhiana kitaifa
b) Ushiriki wa wananchi ni lazima uwe wa kutoshereza ili kuwezesha umiliki wa wananchi wa Katiba husika.
c) Katiba kuwa ni ya kipekee kutokana na historia ya taifa husika
d) Katiba kutoruhusu ubaguzi wa aina yeyote miongoni mwa raia wake.
e) Katiba lazima itoe maono ya mbele ya taifa husika.
f) Na mwisho Katiba huwa ni sheria mama katika nchi ambapo hakuna sheria inayotungwa utaruhusiwa kukinzana nayo.

JE? KATIBA YA NCHI ITALINDA RASILIMALI ZA TAIFA?
Iwapo katika mchakato mzima wa uandikaji wa katiba mpya utazingatia misingi mikuu ya uandaaji wa Katiba mpya, pia watanzania wataweza kushiriki na kushirikishwa wakiwa ni washiriki waliojengwa uelewa hasa wa kujua mazuri na mapungufu waliyo katika Katiba ya sasa, na iwapo Tume itatekereza majukumu yake kwa haki na bila kuegemea upande wowote, Katiba mpya itakuwa ni suruhisho ya mambo yote. Imani tuliyo nayo katika Katiba hii tunayoandaa ni pana mno kwani suala la udhibiti wa rasilimali za nchi litakuwa ni suala dogo katika yale tunayoyategemea.
Kitu muhimu kinachotakiwa sasa ni kuakikisha utaratibu mzima wa kuandika Katiba mpya unafuatiriwa kwa umakini ili husiweze kukosewa au kupindishwa kwa maslahi ya kundi lolote lile.
Ni matarajio ya watanzania kuwa Katiba mpya itakuwa ndiyo dira na mwongozo mpya wa taifa ili kuongoa dukuduku za wananchi walizonazo.

SUALA LA UDHIBITI WA RASILIMALI PESA
Katika Katiba ya jamhuri ya muungano ya mwaka 1977 sura ya saba , sehemu ya pili namba 143 inazungumzia suala la mdhibiti na mkaguzi mkuu wa fedha za serikali . Mdhibiti huyu anapaswa kupewa madaraka ya kutosha katika katiba mpya kuwajibisha watendaji wa serikali ambao watabainika na kosa la matumizi mabaya ya rasilimali za nchi. Apewe mamlaka ya kuwafikisha watuhumiwa mbele ya sheria moja kwa moja.
Katiba mpya ingalie suala la benki kuu iliyopewa dhamana na kusimamia suala la udhibiti wa pesa, hasa mfumko wa bei, kudhibiti matumizi ya pesa za nje kununulia bidhaa hapa nchini na kuiruhusu benki kuu kununua na kuifadhi dhahabu ambayo kila kukicha pei yake imekuwa ikipanda katika soko la dunia ili kuongeza pato la taifa.

KUPUNGUZA NGUVU/ MADARAKA YA RAISI
Ili kuwezesha vyombo vingine kufanya kazi kwa kujitegemea kujiamini na kutoingiliwa kimaamuzi Katiba mpya inapaswa kumpunguzia madaraka mtendaji mkuu wa nchi. Suala hili litafanyika kwa nia njema hasa ya kuboresha utendaji wa vyombo hivi. Tumeona katika kipindi kilichopita mahamuzi wengi yakisubili uamuzi wa rais ili vyombo vingine viweze kufanya kazi zake.

MISAMAHA YA KODI
Moja ya vipengele ambayo vimekuwa vikipoteza pesa za nchi ni pamoja na misamaha ya kodi. Sheria kali zitungwe na utaratibu wa utoaji wa misamaha urekebishwe ili misamaha itolewe na chombo kilichoundwa kisheria na sio ofisa mmoja anayeweza kutoa misamaha kwa maslahi binafsi.

MIKATABA YA MADINI NA RASILIMALI NYINGINE ZA TAIFA
Kutokana na uzoefu tulio nao rasilimali nyingi za taifa zimepotea kutokana na mikataba mibovu iliyoingiwa na watendaji wa serikali bila kujali masilahi ya nchi Suala ili likirudi mikononi kwa wawakilishi wa wananchi ili mikataba yote bunge liweze kuiridhia kabla ya kusainiwa na wawekezaji
Masula yote yenye maslahi ya kitaifa yaweze kuchuliwa na yale yasio ya kitaifa yatachujwa kulingana na uzito wa hoja na kuachwa.

MAADILI YA TAIFA
Kila nchi huwa na maadili yake Lazima Katiba yetu ilitambue hili na kuliweka wazi katika vifungu vyake. Suala kama la rushwa na ulinzi wa rasilimali za nchi vyaweza kuwa ni sehemu ya maadili yetu. Mala na tamaduni zinazotutenganisha na kututofautisha na nchi nyingine pia zaweza kuchukuliwa kama sehemu ya maadili yetu