Na Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar
WIZARA ya Afya imeeleza hatua zilizofikiwa na zinazoendelea kuchukuliwa katika kutekeleza azma ya kuifanya hospitali kuu ya Mnazi Mmoja kuwa hospitali ya rufaa.
Maelezo hayo yametolewa leo na uongozi wa Wizara ya Afya katikaa mkutano kati ya uongozi huo na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein, katika kuangalia utekelezaji wa kazi za Wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2011-2012 pamoja na vipaumbele na malengo kwa mwaka 2012-2013.
Katika mkutano huo uliofanyika Ikulu mjini Zanzibar ambapo pia, Makamu wa Kwanza wa Rais Maalim Seif Sharif Hamad alihudhuria, Wizara hiyo ya Afya ilieleza kuwa miongoni mwa hatua hizo ni pamoja na ujenzi wa Dental Unit mpya ya kisasa kwa msaada wa Shirika lisilo la kiserikali la Marekani ‘Miracle Corners of the World’.
Uongozi huo ulieleza kuwa hatua nyengine ni pamoja na kuifanyia ukarabati mkubwa kwa msaada wa ICAP Maabara ya hospitali ya MnaziMmoja.
Akitoa maelezo kwa niaba ya Wizara hiyo, Katibu Mkuu wake Dk. Mohammed Saleh Jiddawi alisema kuwa hospitali hiyo ya Mnazi Mmoja imeimarisha huduma za watoto wachanga kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha Haukland cha Norway pamoja na vifaa kadhaa vya kisasa.
Alisema kuwa hatua hiyo imepunguza kwa kiasi kikubwa vifo vya watoto wachanga vilivyokuwa vikitokea hapo siku za nyuma. Uongozi huo ulieleza kuwa kitengo cha wagonjwa mahututi kimetiwa vifaa na mkataba wa ‘Mtambo wa Oxygen’ umeshatiwa saini na ‘Tanzania Oxygen’ na tayari asilimia 20 zimeshalipwa.
Aidha, ulieleza kuwa kambi za Madaktari Bingwa zinaendelea ambapo madaktari kutoka Hispania wanafanya upasuaji wa saratani za mgongo na ubongo ambapo tayari wameshafanya pasuaji zipatazo 30 za ubongo na 150 za Uti wa mgongo tena kwa mafanikio makubwa.
Ilieleza kuwa madaktari bingwa wa Kidachi tayari nao wameshafanya pasuaji 365 za plastiki na Waturuki wameshafanya pasuaji 50 za mifupa ambapo jumla ya pasuaji zilizofanywa na Madaktari kutoka nje ni 595.
Uongozi huo ulieleza kuwa pasuaji hizo kwa kawaida kila moja gharama zake ni dola 2000, ambapo serikali ingebidi itumie zaidi ya dola milioni moja kwa ajili ya kuwasafirisha nje wagonjwa hao mbali ya usambufu wa safari zenyewe.
Pamoja na hayo, uongozi huo ulieleza kuwa licha ya upungufu wa madaktari na wauguzi Wizara imekuwa ikifanya juhudi ya kuziba pengo hilo kwa kusomesha vijana katika Chuo cha Afya Mbweni na hata nje ya Zanzibar.
Wizara hiyo ilieleza kuwa hivi karibuni Wizara imepata madaktari watatno na daktari bingwa mmoja (Paedaitrician) na Daktari Msaidizi (AMO) mmoja na wauguzi wanane wa ngazi ya Degree.
Sambamba na hayo uongozi huo ulieleza kuwa katika kuelekeza kwenye kuifanya hospitali ya MnaziMmoja kuwa hospitali ya rufaa imeshafanya mazungumzo na Norway na imeonesha nia ya kuwaunga mkono.
Wizara ilieleza kuwa Mtaalamu kutoka Norway ameshafanya uchambuzi yakinifu na tayari na tayari imeshachagua Daktari Masaidizi (AMO) mmoja na wauguzi wawili kwenda nchini humo kujifunza mambo yanayohusiana na moyo.
Wizara hiyo pamoja na mambo mengineyo yakiwemo kuhusiana na bajeti yake pamoja na vipaumbele na malengo iliyojiwekea pia, ilieleza azma yake ya kukamilisha kituo cha Kwamtipura na Mpendae kwa lengo la kuipunguzia mzigo hospitali kuu ya MnaziMmoja.
Kwa upande wake Dk. Shein alitoa pongezi kwa juhudi zake hizo za kuiimarisha hospitali hiyo ya MnaziMmoja kwani jambo hilo alikuwa akilisisitiza kwa muda mrefu tokea alipoingia madarakani akiwa na lengo la kuwarahisishia na kuwapatia wananchi huduma bora za afya hapa Zanzibar.
Mkutano huo ni miongoni mwa taratibu alizoziweka Dk. Shein katika uongozi wake za kukutana na Watendaji Wakuu na Viongozi wa Wizara zote wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kwa kila muda wa miezi mitatu kwa ajili ya kuangalia utekelezaji wa kazi za Wizara hizo kupitia Bajeti zake pamoja na kuangalia mpango wa utekelezaji wa malengo makuu ya ya Wizara na Uhusiano wake na Dira 2020 na MKUZA.