Na Mwandishi Wetu
VIONGOZI wa makanisa wanapaswa kubuni mbinu za kubaini waumini walio katika ndoa ambao wanadanganya na kufunga ndoa nyingine kwa siri, hali inayohatarisha watoto kukosa matunzo na malezi ya baba na mama.
Mbinu hizo zinaweza kuwa ni pamoja na madhehebu kutengeneza mfumo wa kompyuta na simu za mikononi utakaowezesha makanisa kupata taarifa za watu waliofunga ndoa na wanaotarajiwa kufunga ndoa kwenye makanisa yao na madhehebu mengine pia.
Kadhalika wanaweza kutumia barua kutaarifu makanisa ya madhehebu yote nchini na wakuu wa wilaya kuhusu watu wanaokusudia kufunga ndoa kuepuka kumfungisha ndoa mtu mmoja mara mbili.
Makanisa yanashauriwa kubadili mfumo wanaoutumia sasa wa kutoa tangazo la ndoa kwenye makanisa ya watarajiwa tu badala yake yatangazwe pia katika makanisa mengine.
Vile vile madhehebu yanapaswa kubuni mipango endelevu itakayowavutia vijana wa kike na wa kiume kujifunza mbinu za kuepuka vishawishi vinavyowapelekea kuingia kwenye ndoa za kitapeli ambazo hazidumu.
Kupitia mipango hiyo madhehebu ya dini pia yanaweza kuandaa mafunzo endelevu ya kuwajengea wanandoa uelewa kuhusu wajibu wa baba na mama katika ustawi wa watoto kiroho na kijamii.
Hatua hii itapunguza wimbi la watoto na wanawake kutelekezwa hivyo kuwaweka katika hatari ya kujiingiza kwenye vitendo viovu vinavyoweza kusababisha kuambukizwa virusi vya UKIMWI, wizi na madawa ya kulevya.
TAMWA tunatoa tahadhari hii kutokana na baadhi ya wanawake wanaofika ofisini kwetu kuomba ushauri wa kisheria kuhusu waume zao kutelekeza familia baada ya kufunga ndoa nyingine kwa siri.
Elizabeth Mhangwa, Mratibu wa Kituo cha Usuluhishi (CRC) kilichopo TAMWA amesema kati ya Oktoba 2011 na mwishoni mwa mwezi wa nne mwaka huu kuwa kila mwezi wanawake watatu hadi watano waliofunga ndoa za Kikristo walifika wakilalamikia waume zao kufunga ndoa nyingine kwa siri.
Ametoa mfano wa mwanamke aliyefunga ndoa na mume wake katika kanisa Katoliki la Saint Maximilian lililopo Mwenge jijini Dar es Salaam na baada ya miaka michache akafunga tena ndoa nyingine katika kanisa la Efatha Mwenge.
Kwa imani za Kikristo ndoa ni ya mke mmoja na mume mmoja na wanandoa wanapaswa kuishi maisha yao yote.
Hata hivyo kesi ambazo zimeshughulikiwa na Kituo hicho cha Usuluhishi zinaonyesha kuwa ndoa nyingi hasa mijini zinavunjika kutokana na ulevi, usaliti, vitendo vya ukatili na kutelekeza familia.
TAMWA inaamini kuwa madhehebu ya dini yakijipanga kimkakati yanaweza kuepusha wanandoa kufanya ulaghai wa kutelekeza familia zao na kufunga ndoa nyingine kwa siri ambako kunasababisha madhara makubwa kwa watoto na kuvuruga amani katika jamii.