Twiga Stars kujipima kwa Zimbabwe

Baadhi ya wachezaji wa Timu ya Taifa ya wanawake (Twiga Stars)

TIMU ya Taifa ya wanawake (Twiga Stars) itacheza na Zimbabwe katika mchezo wa kirafiki utakaofanyika Mei 12 mwaka huu kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Twiga Stars hivi iko katika ziara ya mechi za kirafiki katika mikoa ya Dodoma na Mwanza. Leo, Mei 8 mwaka huu itacheza na kombaini ya Mkoa wa Dodoma ya vijana wenye umri chini ya miaka 17 katika mchezo utakaofanyika Uwanja wa Jamhuri, mjini Dodoma.

Kesho Mei 9 mwaka huu itaondoka kwenda jijini Mwanza ambapo pia itacheza mechi moja ya kirafiki Mei 10 mwaka huu kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, na kurejea Dar es Salaam tayari kwa ajili ya mechi dhidi ya Zimbabwe.

Zimbabwe inatarajia kuwasili Mei 9 mwaka huu jioni kwa ndege ya South African Airways (SAA) ikiwa na msafara wa 25 na wataondoka Mei 14 mwaka huu alfajiri.

Wakati huo huo; Kamati ya Mashindano ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) inatarajia kukutana Mei 8 mwaka huu ambapo pamoja na mambo mengine itapanga vituo vya Ligi ya Taifa na tarehe ya kuanza ligi hiyo.

Mikoa nane imeomba kuwa wenyeji wa ligi hiyo itakayochezwa katika vituo vitatu. Mikoa hiyo kupitia kwenye vyama vyao vya mpira wa miguu ni
Mikoa iliyoomba vituo ni Dar es Salaam, Kigoma, Kilimanjaro, Lindi, Mara, Mbeya, Shinyanga na Singida.

Timu zinazoshiriki ligi hiyo ni mabingwa wa mikoa. Timu hizo ni Ashanti United ya Ilala (Dar es Salaam), Aston Villa (Singida), Bandari FC (Kagera), CDA (Dodoma), Flamingo SC (Arusha), Forest FC ya Siha (Kilimanjaro), JKT Kanembwa (Kigoma), Korogwe United ya Korogwe (Tanga), Kurugenzi ya Mafinga (Iringa), Lindi SC (Lindi) na Majimaji (Tabora).

Mighty Elephant (Ruvuma), Mkamba Rangers ya Kilombero (Morogoro), Mpanda Stars ya Mpanda (Rukwa), Mwadui FC (Shinyanga), Nangwa VTC (Manyara), Ndanda FC (Mtwara), Pamba SC (Mwanza), Polisi Mara (Mara), Red Coast ya Kinondoni (Dar es Salaam), Super Star ya Bagamoyo (Pwani), Tenende SC (Mbeya) na Tessema FC ya Temeke (Dar es Salaam).