Ubakaji: Madaktari waeleza namna ya kutunza ushahidi

Mkurugenzi Mtendaji, Ananilea Nkya

MADAKTARI wamewatahadharisha kwamba mtu anayebakwa kamwe asioge au kubadilisha nguo kwa sababu kufanya hivyo kunapoteza ushahidi muhimu wa kumtia hatiani kisheria mtu aliyebaka.

Wamesema mtu akibakwa anapaswa kwenda polisi haraka kupata fomu ya PF3 na awahishwe hospitali ya wilaya ambako ataweza kupatiwa matibabu ikiwa ni pamoja na dawa ya kuzuia maambukizi ya Virusi Vya UKIMWI (VVU)

Dawa ya kuzuia maambukizi ya (VVU) inayojulikana kama PEP inaweza kufanya kazi endapo tu mwathirika atapatiwa ndani ya saa 72 baada ya kubakwa na endapo kabla ya kubakwa alikuwa hana maambukizi.

Dk. Zuberi Mzige wa Hospitali ya Mwananyamala, katika Wilaya ya Kinondoni, Dar es Salaam amesema watoto, wasichana na wanawake wengi wanaofika hospitali baada ya kubakwa wanakuwa wamepoteza ushahidi kutokana na kuoga na kubadili nguo walizokuwa wamevaa wakati wakibakwa.

Aidha amesema wengi waliobakwa wanafika hospitalini wakiwa wamechelewa na hivyo kuwa katika hatari kubwa ya kupata maambukizi ya VVU.

Amesema kesi nyingi za ubakaji zimekuwa zikikosa ushahidi wa daktari kwa sababu aliyebakwa anatakiwa kupelekwa hospitalini akiwa vilevile na nguo zake na uchafu ule ule kwa sababu ushahidi wa polisi na daktari ya kuwa umebakwa ni pamoja na nguo ulizobakwa nazo tena bila kuzibadilisha.

Dk. Prisca Berege anayeshughulika na magonjwa ya watoto katika hospitali ya Mwananyamala amesema kuna tatizo kubwa la ubakaji hasa kwa watoto Dar es Salaam na kwamba hatua zisipochukuliwa taifa litapata madhara makubwa.

Akizungumza na wanahabari walioshiriki katika utafiti wa masuala ya ukatili wa kijinsia uliofanya na TAMWA wilaya ya Kinondoni Dakta Berege amesema kwa wastani kila siku hospitali hiyo inapokea watu watatu waliobakwa ambao ni wanawake na watoto.

Dk. Begere amesema vitendo vingi vya ubakaji vinaripotiwa hospitalini hapo nyakati za usiku hivyo amewaasa wazazi kuepuka kuwatuma watoto wao usiku.

Aidha amewataadharisha wasichana kujiepusha kwenda kwenye nyumba za wanaume hata kama wanawaamini na ni marafiki zao kwani baadhi yao wanaume wanakuwa na nia mbaya ya kubaka hata kama ni mchana.

Ametoa mfano wa binti mmoja ambaye hivi karibuni alibakwa mchana kweupe kwenye nyumba ya mwanaume aliyemwamini na kumthamini kama kaka yake na mwajiri wake. Mwanamme huyo alimwita msichana huyo nyumbani kwa kumdanganya kuwa kuna kazi wangekwenda kupanga kufanya.