Ruvuma ‘out’ Kili Taifa Cup

Nembo ya Kili Taifa Cup 2011

Na Asha Kigundula,
Arusha

TIMU ya soka ya Mkoa wa Ruvuma jana imeaga mashindano ya Kili Taifa Cup baada ya kupokea kipigo cha mabao 3-2 toka kwa timu ya Mkoa wa Mbeya Mapinduzi (Stars) mchezo uliofanyika kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid uliopo Jijini hapa.

Dakika ya 3 ya mchezo Gaudence Mwaikimba aliipatia Mbeya goli la kwanza kwa kupiga mpira wa shuti la mbali lililotinga wavuni.

Mchezaji Juma Mpola aliipatia Mbeya goli la pili baada ya kufanyiwa kazi nzuri na wachezaji Said Mtupa na Steven Mazanda naye kumalizia mpira wavuni.

Mpaka mapumziko Mbeya ilitoka kifua mbele kwa magoli 2-0, katika kipindi cha pili Ruvuma ilifanya mashambulizi kadhaa na dakika ya 49 ilipata goli kupitia kwa mchezaji Ally Bilali baada ya kupata pasi toka kwa Kassim Kilungo.

Mwaikimba aliipatia Mbeya goli la tatu baada ya kuipangua safu ya ulinzi ya Ruvuma na kupiga shuti kali lililomshinda Kipa wa Ruvuma Hamad Waziri.

Dakika moja kabla ya mchezo kumalizika ruvuma Ally Bilali aliipatia timu yake goli la pili lililofungwa kwa njia ya Penati baada ya mchezaji wa Mbeya Jumanne Elfadhili alimkwatua mchezaji Ally Bilali katika eneo la hatari.

Mashindano haya yamedhaminiwa na Kampuni ya Bia Tanzania (TBL) kupitia kinywaji chake cha Kilimanjaro Premium Lager na masuala ya habari kuratibiwa na Kampuni ya Executive Solutions.