ASEMA YEYE NDIYE ALIYEAGIZA JENGO LINUNULIWE, TARATIBU ZILIFUATWA, ASEMA ALISHANGAA KUSIKIA AMESHTAKIWA
RAIS Mstaafu wa Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa jana alipanda kizimbani kumtetea Balozi wa zamani wa Tanzania nchini Italia, Profesa Costa Mahalu katika kesi ya uhujumu uchumi yanayomkabili, huku akimmwagia sifa kemkem za utumishi mwema.
Profesa Mahalu na mwenzake, Grace Martin aliyekuwa Ofisa Utawala wa Ubalozi huo, wanakabiliwa na kesi hiyo katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, wakidaiwa kuisababishia Serikali hasara ya Euro 2,065,827.60, kupitia mchakato wa ununuzi wa jengo la Ubalozi wa Tanzania Italia.
Hii ni mara ya kwanza katika historia ya Tanzania kwa Rais Mstaafu kupanda kizimbani kwa sababu yoyote ile. Mkapa ambaye wakati wa ununuzi wa jengo hilo alikuwa Rais, aliieleza Mahakama kuwa anatambua mchakato wa ununuzi huo na kwa kuwa yeye ndiye aliyetoa idhini ya ununuzi, mchakato wote ulikwenda vizuri.
Mkapa na msafara wake ulioongozwa na maofisa wa itifaki aliwasili mahakamani hapo saa 3:45 asubuhi. Akiwa amevalia suti ya rangi ya kijivu alielekea ndani ya Mahakama hiyo akiwa amezungukwa na wapambe wake akitabasamu baada ya kuwaona wanahabari.
Aliingia katika chumba maalumu cha mapumziko hadi saa 5:32 asubuhi muda ambao aliitwa kizimbani kutoa ushahidi wake. Kabla hajaanza kutoa ushahidi, alikula kiapo maalumu cha kutoa ushahidi wa ukweli na baadaye kuendelea hadi saa 7:31 mchana alipomaliza na kuondoka.
Mkapa alianza kutoa ushahidi katika kesi hiyo inayosikilizwa na Hakimu Mkazi Mfawidhi, Ilvin Mugeta, akiongozwa na mmoja wa mawakili wa Profesa Mahalu, Alex Mgongolwa kwa kueleza historia ya utumishi wake katika nafasi za kidiplomasia.
Mkapa alijibu maswali kwa kujiamini na kwa umakini mkubwa huku mara kadhaa akiwavunja mbavu wasikilizaji kwa jinsi alivyokuwa akiwajibu mawakili wa Serikali wakati mwingine mwenyewe alishindwa kujizuia kucheka.
Akielezea mchakato mzima wa ununuzi wa jengo hilo. Mkapa alidai kuwa Serikali yake ilifahamu ununuzi wake na taratibu za malipo baada ya kufahamishwa na Profesa Mahalu na kwamba lilinunuliwa kwa maagizo ya Serikali yake.
“Nilitambua muuzaji alipaswa alipwe malipo kwa kutumia akaunti mbili tofauti na Serikali ilitoa baraka. Mimi nilitaarifiwa na sikuzuia,” alidai Mkapa.
Kuhusu kuwepo kwa mikataba miwili katika ununuzi wa jengo hilo Mkapa alijibu: “Ninachoweza kukumbuka kwa hakika mimi ni kwamba niliambiwa kuwa kuna malipo katika akaunti mbili ‘separate’ (tofauti).
Alieleza kushangazwa na taarifa kwamba aliyekuwa Katibu Mkuu Kiongozi, Martin Lumbanga katika ushahidi wake alidai kuwa alikuwa hajui mchakato wa ununuzi wa jengo hilo.
Wakili Mgongolwa: Shahidi, alikuja hapa Shahidi wa kwanza wa mashtaka (PW1), Martin Lumbanga akasema kuwa hakuwa na taarifa za idhini ya Serikali katika ununuzi wa jengo hilo. Je, wewe unasemaje?
Mkapa: Ninashangaa ni kwa nini alisema hivyo.
Mgongolwa: Lakini wewe ukiwa Rais ulijua na ukabariki, inawezekana yeye asingeweza kujua?
Mkapa: Ndiyo.
Mkapa alidai kuwa katika mchakato wa ununuzi wa jengo hilo, mbali na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa kupitia kwa Balozi Mahalu, wizara nyingine ambazo zilihusika ni Ujenzi na Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi akidai kuwa zote zilituma wataalamu wake kufanya tathmini ya jengo hilo kabla ya ununuzi.
Akielezea maelezo yaliyoko katika kielelezo cha 6 cha ushahidi wa upande wa utetezi ambacho ni taarifa ya aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa bungeni wakati huo Jakaya Kikwete (sasa Rais) juu ya mchakato wa ununuzi wa jengo hilo Mkapa alisisitiza:
“Maneno hayo ni sahihi. Hayo ndiyo ninayoyajua mimi kuwa ndiyo yaliyotokea.”
Taarifa hiyo pamoja na mambo mengine, inaeleza kuwa jengo hilo lilinunuliwa kwa jumla ya Sh.2.9 bilioni na kwamba hati za umiliki wake zilishawasilishwa wizarani na kupelekwa kwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).
Mkapa alieleza kuwa hajawahi kupata malalamiko yoyote kutoka Italia kuhusu ukiukwaji wa sheria katika mchakato wa ununuzi wa jengo hilo na wala kwa mmiliki wa jengo hilo kudai kuwa alilipwa pungufu ya kiasi walichokubaliana.
Wakili Mgongolwa: Kikatiba Rais hukabidhiwa ripoti ya CAG. Je, una taarifa yoyote ya CAG kuhusu malalamiko juu ya ununuzi wa jengo hilo?
Mkapa: Sikuwahi kupata malalamiko hayo.
Wakili: Nini ufahamu wako kama Rais Mstaafu juu ya utumishi wa mshtakiwa ambaye ulimteua kuwa Balozi Italia?
Mkapa: Ninamfahamu kama ni msomi mzuri, mwadilifu na mfanyakazi mwaminifu na kiongozi wa haki.
Akizungumzia mawasiliano yake na Profesa Mahalu wakati akiwa Balozi, Mkapa alidai kuwa walikuwa wakiwasiliana ama kwa maandishi au kwa mdomo na kwamba hiyo ilitegemea usiri wa jambo husika, lakini akasisitiza kuwa wakati wa mchakato wa ununuzi wa jengo hilo waliwasiliana.
Baada ya kumaliza kutoa ushahidi wake, Mkapa aliulizwa maswali mbalimbali na mawakili wa Serikali, Vicent Haule na Ponsiano Lukosi kuhusu ununuzi wa jengo hilo, sehemu ya mahojiano hayo ilikuwa kama ifuatavyo:
Wakili Haule: Mheshimiwa katika Hansard (kielelezo namba 6 cha upande wa utetezi) uliyosoma imeandikwa jumla ya pesa zilizopelekwa kununua jengo hilo ni kiasi gani?
Mkapa: Sh.2.9bilioni.
Haule: Na zilizoandikwa kwenye hii risiti ambazo ulisema ulikuwa unazifahamu ni kiasi gani?
Mkapa: Nilichosema ni Euro 3milioni, mimi sijui exchange rate (gharama za ubadilishaji wa fedha) wakati huo ilikuwa ni kiasi gani hiyo si kazi yangu.
Haule: Nani aliagiza upelelezi wa ununuzi wa jengo hilo?
Mkapa: Mimi Sijui.
Haule: Uchunguzi wa malipo hayo ulifanyika lini ukiwa bado madarakani au baada ya kutoka madarakani?
Mkapa: Mimi sijui, nilikuja kusikia tu kuwa Balozi wako anashtakiwa.
Haule: Ulijua lini kuwa Balozi wako uliyekuwa umemteua wewe anashtakiwa?
Mkapa: Siku alipofikishwa mahakamani ndipo nilipoambiwa na kesho yake kweli nikamuona kwenye magazeti.
Haule: Ulisema ulipotaarifiwa kuhusu ununuzi huo ulibariki na hukuzuia, kwani ulipaswa kuzuia?
Mkapa: Ningeweza kuzuia na kuamuru hizo pesa zipelekwe kwingine kwa kuwa wakati huo tulikuwa na crisis (tatizo) ya fedha, lakini kwa kuwa niliona umuhimu wa ununuzi wa jengo hilo nikaagiza linunuliwe.
Haule: Umuhimu upi wa kulipa kupitia akaunti mbili?
Mkapa: Kupata Chancellery (ofisi ya ubalozi)
Haule: Baada ya kutoa maagizo hayo (kwa Profesa Mahalu) ni nani mwingine wizarani (Mambo ya Nje) uliyemwarifu kuhusu malipo hayo kwa akaunti mbili?
Mkapa: Kwani hiyo inahusiana na nini? Maagizo yangu mimi nilishatoa kwa balozi jengo linunuliwe, kama Rais nilikuwa ninaagiza tu.
Haule: Mheshimiwa, nakuuliza tena na nisingependa nawe uniulize swali. Ni kweli au si kweli kwamba hakuna mtu mwingine wizarani ambaye ulimpa taarifa hizo?
Mkapa: Sikumbuki mimi.
Lukosi: Mheshimiwa, Lumbanga akiwa Katibu Kiongozi ulikuwa ukimwamini?
Mkapa: Ndiyo.
Lukosi: Ni kwa kiasi gani ulimshirikisha katika ununuzi wa jengo hilo?
Mkapa: Specifically katika hilo sikumbuki lakini ki-principle nilishatoa maagizo kuwa kupata chancellery nunueni na yeye alikuwa akijua. Tulifanya hivyo India, Marekani na Uingereza.
Lukosi: Sasa Lumbanga alisema hajui ununuzi wa hili. Je, wewe unaona ni kitu cha kawaida?
Mkapa: Ndiyo maana nimesema nashangaa, maana haingewezekana kwamba mimi nika-communicate (nikafanya mawasiliano) na wizara moja tu na Lumbanga asijue.
Lukosi: Ulipata kujua au kuuliza ni kwa nini muuzaji alitaka alipwe kupitia akaunti mbili tofauti?
Mkapa: Sikuuliza, mimi nilichokuwa nataka ni Chancellery.
Lukosi: Unakumbuka kuna jengo jingine la ubalozi ambalo muuzaji alitaka alipwe kwa utaratibu huu wa kupitia akaunti mbili tofauti?
Mkapa: Siwezi kusema, nakumbuka lakini siwezi kusema kwa sababu mambo mengine ukiyasema, yanaweza kuharibu uhusiano na nchi husika.
Hakimu Mugeta: Kwa hiyo hayo mazingira huwa yapo?
Mkapa: Ndiyo.
Lukosi: Unawakumbuka watu wengine uliowahi kuwateua ambao wako mahakamani na yuko mwingine alishakuja kukuomba umtetee?
Mkapa: Ni lazima nilijibu hili? Alihoji Mkapa huku akicheka na kuwafanya wasikilizaji nao wacheke.
Lukosi: Kwa hiyo hii ni kesi ya kwanza kwako kuombwa kuja kutoa ushahidi?
Mkapa: Ndiyo.
Wakili: Nikiwaambia lengo la mwenye jengo kutaka mchakato wa uuzwaji kuwepo na mikataba miwili lilikuwa ni kukwepa kodi kwa Serikali yake utasemaje?
Mkapa: Hilo ni tatizo lake na nchi yake, mimi nilikuwa nataka nyumba na nimepata nyumba, nasema Al Hamdulillah, alisema Mkapa huku akicheka tena na kuwafanya wasikilizaji nao wavunjike mbavu.
Lukosi: Nikikwambia kuwa hizo pesa kulipwa kwa instalment (awamu), Profesa Mahalu alikuwa anataka azitumie kwa maslahi yake utasemaje?
Mkapa: Mimi nitashangaa sana, hasa nitakushangaa wewe, maana Profesa mimi namuamini. Alisema Mkapa na kuwachekesha wasikilizaji.
Mahojiano kati ya Mkapa na Wakili wa Profesa Mahalu, Mabere Marando katika kusawazisha maswali aliyoulizwa na mawakili wa Serikali yalikuwa kama ifuatavyo:
Kusoma zaidi habari hii bofya: www.mwananchi.co.tz