Elimu bora sio majengo pekee – John Mnyika

Mbunge wa Ubungo (CHADEMA), John Mnyika

ELIMU bora sio majengo pekee bali ni pamoja na walimu bora na mazingira bora ya kusomea na kujifunzia yenye vifaa vya kujifunzia na vitabu vya kiada na ziada.

Hivyo, harakati za kusimamia uwajibikaji wa serikali kuu, serikali za mitaa na mamlaka nyingine zinazohusika na sekta ya elimu hususani kwenye shule, vyuo na vyuo vikuu vya umma zinapaswa kuendelezwa.

Tuendelee kuhakikisha rasilimali zinazotengwa ikiwemo ruzuku ya elimu ya msingi na sekondari na mikopo ya elimu ya juu zinakuwa za kutosha, zinatolewa kwa wakati na zinatumika kwa malengo yaliyokusudiwa kwa kudhibiti mianya ya ufisadi.

Wakati, tukisimamia uwajibikaji huo wa serikali tutambue masuala matatu muhimu; mosi, jukumu la kuboresha mazingira ya elimu kwenye elimu rasmi ya darasani sio wa serikali pekee bali ni wajibu wa wote katika jamii.

Pili, izingatiwe kuwa sehemu kubwa ya wananchi hawajapata elimu rasmi hivyo ni muhimu kuwa na mifumo ya elimu kwa njia nyingine mitaani na vijijini ili kuchochea zaidi maendeleo.

Tatu, hata kwa wenye elimu rasmi inafahamika kuwa elimu haina mwisho hivyo kila mmoja ana wajibu wa kujisomea ili kuendeleza uhuru wa kifikra.

Katika muktadha wa masuala hayo matatu, niliungana na Asasi ya Maendeleo Ubungo (Ubungo Development Initiative-UDI) kuzindua Programu ya Taarifa inayohusisha kukusanya vitabu vya kiada na vya ziada kutoka wa watu mbalimbali na taasisi mbalimbali na kuvisambaza katika taasisi za elimu kwa ajili ya wanafunzi kusoma na maeneo maalumu kwa ajili ya wananchi kujisomea.

“Toa kitabu kisomwe” kupitia ofisi ya Ubungo Development Initiative (UDI) iliyopo Kimara Kona au wasiliana na UDI kupitia Afisa Taarifa (0768503331 au 0715745874) au barua pepe ubungo2005@yahoo.com kutoa kitabu husika.

Mwanafalsafa mmoja aliwahi kusema kwamba ukimpa mtu samaki umemlisha kwa siku moja lakini ukimfundisha kuvua umemlisha kwa maisha yake yote. Nikisisitiza mantiki ya msemo huo naweza kusema pia kwamba ukimpa mtu chakula cha kawaida umemshibisha kwa muda mfupi lakini ukimpa chakula cha kifikra umemuwezesha kwa muda mrefu; huu ndio msingi utakaoongoza Programu ya Taarifa; “Toa kitabu kisomwe”.