TGNP yawanoa wanaharakati toka mikoani juu ya mbinu za uraghbishi
TGNP imezindua warsha ya uraghbishi ya wiki moja kwa wanaharakati kutoka mikoa mbalimbali ikiwemo Dar es Salaam, ili kunoa uwezo wao wa kufanya kazi na jamii husika kuibua masuala nyeti katika jamii.
Mbali na hayo warsha hiyo inalenga washiriki kuangalia mafanikio na changamoto, kuchambua visababishi vya matatizo au mafanikio hayo kwa kina na kupanga mikakati ya kushughulikia kero hizo pamoja na wanajamii .
Warsha hiyo iliyoanza jana pia inalenga kuimarisha uelewa wa pamoja wa mtizamo ya kiitikadi kuhusu dhana za ukombozi wa wanawake kimapinduzi na makundi yaliyoko pembezoni na kuitekeleza kwa vitendo.
Warsha hiyo imejikita kumjengea uelewa wa pamoja kuhusu uraghbishi na mbinu shirikishi zinazotumika katika uraghbishi, kuongeza uelewa wa kampeni ya hiaki ya uchumi katika kudai kazi zenye heshima utu na kipato, uhifadhi wa kumbukumbu, mbinu za mawasiliano na uwezo wa kuvitumia katika Ujenzi wa Vuguvugu la ukombozi wa wanawake kimapinduzi katika ngazi ya kanda.
Wawezeshaji wa warsha hiyo ni Richard Mabala Mkurugenzi wa TAMASHA ambayo ni asasi ya kiraia iliyobobea katika kuwawezesha vijana na jamii kwa ujumle kutumia mbinu za uraghbishi kama chachu ya kuleta mabadiliko chanya katika jamii husika. Winston Chuchil Mkurugenzi Msaidizi wa TAMASHA ni mwezeshaji mwenza ambaye naye pia amebobea katika mbinu za uraghbishi.
Washiriki wa Warsha hiyo wametoka katika mikoa ya Shinyanga, Morogoro, Arusha, Dodoma, Mwanza, Mbeya, Dar es Salaam na Pwani wakiwakilisha asasi mbalimbali za kiraia ambazo zimekuwa mstari wa mbele katika kuleta mabadiliko chanya katika jamii za mikoa husika.
Baada ya warsha washiriki wakishirikiana wanajamii na TGNP wataendesha zoezi la uraghbishi katika mikoa husika ambapo watatumia mbinu mbalimbali za uraghbishi katika kuibua masuala nyeti yanayogusa jamii husika, kuyachambua kwa kina ili kupata kiini cha matatizo au mafanikio, hayo na kutafuta mbinu mbali mbali za kutafuta ufumbuzi wa matatizo hayo, mbinu zitakazotumika, nani atafanya nini kuanzia ngazi binafsi, jamii na taifa.