Na Ismail Ngayonga
MAELEZO, Dar es Salaam
WAFANYAKAZI katika Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali wametakiwa kuheshimu kanuni za fedha na kuweka sawa hesabu ili kutekeleza mikakati anuai iliyopo kiufasaha na ukamilifu.
Kauli hiyo imetolewa jana na Waziri wa Katiba na Sheria, Celina Kombani wakati alipokuwa akifungua Mkutano wa Baraza la Wafanyakazi wa Ofisi ya Mwanasheria wa Serikali uliofanyika katika Ukumbi wa Giraffe Jijini Dar es Salaam.
Waziri Kombani alisema ni wazi kuwa rasilimali fedha haitoshi, hivyo ni wajibu kwa wafanyakazi kuwa na vipaumbele vya matumizi ya rasilimali za Ofisi ili kuhakikisha mafanikio yanaonekana katika maeneo ya kazi.
Aliongeza kuwa Baraza la wafanyakazi linawajibu wa kutambua na kujadili vipaumbele vya Ofisi ili kuhakikisha kwamba fedha za kutosha zinatengwa kulingana na vipaumbele ili kuboresha huduma na kuondoa kero za wananchi wanaowatumikia.
“Wajumbe wa Baraza la Wafanyakazi mnapaswa kutoa mwongozo na ushauri katika kutatua matatizo yanayojitokeza katika utekelezaji wa mambo yaliyo ndani ya uwezo wenu,” alisema Waziri Kombani.
Kwa Mujibu wa Kombani alisema ni vema Menejimenti ishirikiane na Baraza la Wafanyakazi pamoja na Wafanyakazi kwa ujumla katika kujadili na kufikia maamuzi yanayohusu maslahi yao, utendaji wao wa kazi na maandalizi ya Bajeti.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chama Cha Wafanyakazi wa Serikali Kuu na Afya (TUGHE) katika tawi la Ofisi ya Mwanasheri Mkuu wa Serikali, Bw. Hamisi Msigala alisema tatizo la miundombinu mipya ya utumishi halijapatiwa ufumbuzi wa kudumu kwani kilio kilichopo ni ile hali ya kuonekana kuwa uzoefu kazini haupati thamani inayotakiwa.
Akitolea mfano alisema muundo mpya wa mtumishi wa kada ya ukarani amewekewa ukomo wa kiwango cha daraja E katika mshahara wake (TGS.E) na anapofikia hapo atabaki hata kwa miaka 20 mingine na vinginevyo abadili kazi.
Ni kweli utaalamu wa mtumishi aliyesoma hauwi sawa na asiyesoma. Lakini uzaofu na elimu kwa maoni yetu vyote ni muhimu katika sehemu za kazi na si elimu ya shuleni ikaonekana ndio mhimili na uzoefu si muhimu” alisema
Aidha Bw. Msigala alizitaja changamoto zilizopo katika Ofisi hiyo ni pamoja na tatizo la
muda mrefu la usafiri kwa watumishi, hivyo kuwafanya Wafanyakazi wa Ofisi hiyo kutegemea usafiri kutoka Ofisi jirani ya Wizara ya Mambo na Ushirikiano wa Kimataifa, ambapo hata hivyo kupelekea kero mbalimbali ikiwemo kuchelewa kurudi majumbani kwao.