Baba mahakamani kwa kutaka kuuwa kichanga

Na Mwandishi Wetu
Maswa

POLISI wilayani Maswa, Mkoa wa Shinyanga imemfikisha mahakamani, Baya Mlyagape (24) mkazi wa Kijiji cha Songambele Kata ya Ipililo kwa kosa la kutaka kumua mtoto mchanga mwenye umri wa miezi mitano.

Akisomewa mashitaka mbele ya Hakimu wa Wilaya ya Maswa, Thomson Mtani; ilielezwa kuwa mshitakiwa alitenda unyama huo Mei 5, 2011 majira ya saa nne usiku kwa kudai kuwa mtoto huyo alikuwa akilia usiku kucha jambo ambalo ilikuwa ni usumbufu. Inadaiwa mshtakiwa alimvunja mkono wa kulia mara mbili na kumkatakata na wembe kwenye ulimi mtoto huyo.

Mwendesha mashtaka huyo aliendelea kudai kuwa baada ya kutenda kosa hilo, mke wa mshitakiwa alipiga kelele kuomba msaada kwa majirani ili kumnusuru mtoto wake asiendelee kujeruhiwa na baada ya hapo aliamua kutoa taarifa katika Kituo cha Polisi ili sheria ichukue mkondo wake.

Mshitakiwa alikana kutenda kosa hilo mbele ya Hakimu, licha ya kutolewa kwa dhamana kwa mshitakiwa, upande wa mashitaka umepinga dhamana hiyo kwa mshitakiwa kwa kudai hali ya mtoto si nzuri na amelazwa katika Hospitali ya Wilaya ya Maswa. Hata hivyo mshitakiwa alirudishwa rumande hadi kesi itakapotajwa tena.