SHUGHULI za uhamasishaji wa wananchi kunywa dawa za ugonjwa wa usubi, matende na mabusha Wilaya ya Morogoro zimekuwa na mwitikio mzuri baada ya wananchi 239,250 kujitokeza na kupatiwa dawa hizo.
Kwa mujibu wa taarifa za Mganga Mkuu wa wilaya hiyo, Dk. Debora Kabudi iliyotolewa mwishoni mwa wiki mjini hapa, watu 239,250 waliojitokeza katika tukio hilo wamepatiwa dawa ilhali matarajio ya awali ilikuwa ni watu 241,200 kupewa dawa hiyo.
Dk. Kabudi alisema idadi hiyo ni sawa na asilimia 80 ya walengwa na kuongeza kuwa wamepata mafanikio makubwa kimuitikio kwa wananchi wa eneo hilo.
Alibainisha kuwa mbali na idadi hiyo kupatiwa dawa za magonjwa usubi, matende na mabusha pia wengine 32,662 kati ya 52,171 waliolengwa walimeza dawa za ugonjwa wa kichocho ikiwa ni sawa na asilimia 63 ya walengwa.
Aidha katika taarifa hiyo, aliongeza kuwa kutokana na mwitikio huo idara ya afya imefanikiwa kuinua kiwango cha maendeleo kwa asilimia 90, huku utekelezaji kwa kazi zilizopangwa mwaka wa fedha 2010/2011 ukifikia asilimia 84.
Aliyataja mafanikio mengine kuwa ni pamoja na kuanza kukarabati baadhi ya vituo kupitia miradi na wafadhili mbalimbali na kununuliwa kwa dawa, vifaa anuai na kusambazwa katika vituo vya huduma.
Hata hivyo alisema idara yake inakabiliwa na changamoto kadhaa katika kutekeleza majukumu yake, ikiwemo uhaba wa wataalamu kutokana na wengi kukataa kufanya kazi kwenye maeneo yenye miundombinu mibovu na ukosefu wa nyumba za watumishi.
Alizitaja changamoto zingine ni ukosefu wa vyombo vya usafiri wa uhakika kwa wagonjwa, ukosefu wa dawa baada ya Bohari Kuu ya Dawa (MSD) kutoleta dawa kwa wakati hasa katika kipindi cha robo ya pili na ya tatu, pamoja na kuongezeka kwa vifo vya wajawazito.