JK apongeza wabunge kuwasulubu mawaziri

Mh. Jakaya Kikwete

Rais Jakaya Kikwete amesema hakusikitishwa wala kufedheheshwa na mjadala wa wabunge wakati wa Mkutano wa Saba wa Bunge uliotoa mapendekezo kwa mawaziri ambao wizara zao zimekumbwa na ubadhirifu wa fedha wawajibishwe na kwamba serikali imejipanga vizuri katika kutekeleza mapendekezo hayo ya wabunge.

Kadhalika, Rais Kikwete ametoa ruhusa kwa yeyote anayefikiri ameonewa katika ripoti ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), kwenda kukata rufaa mahakamani.

Akihutubia katika Maadhimisho ya Sikukuu ya Wafanyakazi Duniani yaliyofanyika kitaifa kwenye uwanja wa Mkwakwani, jijini Tanga jana, Rais Kikwete, ambaye alizungumzia mambo mbalimbali yanayoikabili serikali na taifa, alisema hakusikitishwa wala kufedheheshwa na mjadala huo kwa kuwa yaliyokuwa yakijadiliwa ni moja ya ahadi zake za kushughulikia ubadhirifu wa mali za umma.

“Mengi yamesemwa kabla na baada, lakini jamani ukweli ni kwamba mimi sikusikitishwa wala kufedheheshwa na mjadala huo na kinyume chake nimefurahi kuona kuwa mambo hayo yanajadiliwa kwa kina na uwazi,” alisema na kuwapongeza wabunge kwa mjadala huo.

Rais Kikwete alieleza msimamo wa serikali katika kushughulikia suala hilo kwa kuahidi kuchukua hatua stahiki kulingana na taarifa ya CAG ili kulinda nidhamu na matumizi mazuri ya fedha za umma.

Aidha Kikwete alitumia nafasi hiyo kuwakumbusha wananchi kwamba kinachofanyika hivi sasa ni utekelezaji wa ahadi zake alizotoa kipindi cha kampeni za urais, kwamba miongoni mwa mambo aliyoahidi kuyashughulikia ni ubadhirifu wa mali za umma.

Rais Kikwete alisema katika mkutano wake na mawaziri pamoja na CAG uliofanyika mjini Dodoma hivi karibuni, CAG alisoma ripoti yake na kuwataja mawaziri ambao wizara zao zimehusika na wizi wa fedha za umma.

Alisema katika mkutano mwingine aliofanya na wenyeviti wa halmashauri, wakurugenzi pamoja na watunza hazina, CAG alizitaja pia halmashauri zilizohusika na wizi huo.

“Baada ya mikutano hiyo na mawaziri pamoja na viongozi wa halmashauri, tulifanya mikutano mbalimbali kujadili nini kifanyike ili kuimarisha nidhamu ya matumizi ya fedha za umma,” alisema.

Alisema kazi ya serikali yake ni kuhakikisha taarifa na mapendekezo ya CAG yanafanyiwa kazi na kwamba hilo si suala la kujadiliwa tena na kwamba hatua ya kulipeleka kwenye Kamati Kuu ya Chama cha Mapinduzi (CC) suala hilo ni moja ya hatua za awali.

“Tumeanza na mawaziri tutachukua hatua dhidi ya wote waliogushwa katika ripoti ya CAG na kama kuna mtu anahisi ameonewa katika ripoti ya Mkaguzi Mkuu wa Serikali aende ana haki kwa mujibu wa Katiba kwenda mahakamani kukata rufaa” alisisitiza.

Alieleza kuwa huo ni mwanzo tu na kwamba serikali itaendelea kuwaumbua walafi na wabadhirifu wa mali za umma na kuhakikisha wanachukuliwa hatua haraka ili fedha na mali za umma zitumike kwa manufaa ya wananchi na si katika matumbo ya viongozi wachache wasio waadilifu.

Alieleza jinsi serikali ilivyojipanga kukabiliana na wabadhirifu wa mali ya umma kwamba ni pamoja na kuiongezea nguvu ofisi ya CAG kwa kuiboresha na kuipa uhuru zaidi ili ifanye kazi zake kwa uhuru, haki na bila ya kubanwa na mtu.

“Ibara ya 27 tumeifanyia marekebisho ambapo mtu atakayegundulika kuhusika na matumizi mabaya ya fedha za umma, atakabidhiwa kwa Takukuru ili afikishwe mahakamani huku uchunguzi ukiendelea”, alisema.

Alisema mambo mengine yaliyofanyiwa marekebisho ni upungufu wa wafanyakazi, vitendeakazi na mabadiliko ya sheria inayowapa nguvu ya kuchukua hatua ya kuwasilisha taarifa ya ubadhirifu polisi na katika Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) dhidi ya mhusika hata kabla ya kufikisha taarifa hizo bungeni.

“Tumeiongezea watumishi, pamoja na kuwapa mamlaka ya kuchukua hatua kwa watakaobainika kuwa na matumizi mabaya ya fedha za umma kuwakabidhi polisi na Takukuru na siyo kungoja tena mpaka taarifa za Bunge…hii ni kuiongezea meno,” alisema.

Alisema katika maboresho hayo, serikali imeajiri wakaguzi 378, kuongeza magari na kujenga ofisi kwa kila mkoa badala ya sasa ambapo wakaguzi wa mikoa ofisi zao zipo kwenye majengo ya wakuu wa mikoa jambo linalojenga shaka endapo ukaguzi utakuwa huru pindi ubadhirifu utafanyika kwenye ofisi hizo.

AZIAGIZA HALMASHAURI

Kwa upande mwingine, Rais Kikwete, aliziagiza wizara, halmashauri za wilaya, miji, majiji na idara za serikali zinazojitegemea kujenga mazoea ya kusoma taarifa za ukaguzi wa hesabu na kuyapa kipaumbele cha kutekeleza maelekezo yaliyomo ili kubaini wizi mapema na kuchukua hatua haraka.

“Tatizo jingine ni watu walioajiriwa katika halmashauri nyingi nchini hawana ujuzi wa kuandaa mahesabu, jambo ambalo serikali imejipanga na mpaka sasa watendaji wenye elimu na ujuzi wa mahesabu 795 wameajiriwa katika halmashauri na hivyo kupunguza tatizo la hati chafu,” alisema.

SENSA, KATIBA MPYA

Kadhalika, Rais Kikwete alizungumzia suala la sensa na Katiba mpya na kuwataka wananchi kujitokeza na kushiriki kikamilifu wakati ukifika ili kutimiza haki na pia kurahisisha harakati za mipango ya serikali ya kuleta maendeleo kwa kuwa na uhakika wa bajeti na mipango yake.

Akijibu risala ya wafanyakazi iliyosomwa na Katibu Mkuu wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi (Tucta), Nicholas Mgaya, Rais Kikwete alieleza kuwa serikali ipo pamoja katika harakati za kuboresha maisha ya wafanyakazi na kwamba itachukua hatua za utekelezaji kulingana na uwezo wake.

MFUMUKO WA BEI

Kwa upande mwingine, Rais Kikwete alisema mfumuko wa bei unaosababisha kupanda kwa gharama za maisha unasababishwa na kupanda kwa bei ya nishati ya mafuta katika nchi yanaponunuliwa mafuta hayo.

Alisema pia kutokuwa na mvua za uhakika katika kipindi cha karibuni, kumesababisha bei ya vyakula kuwa juu hususani sukari, mchele na unga, ambapo alizitaja baadhi ya hatua zilizochukuliwa kupunguza tatizo hili.

“Nilitoa ruhusa kwa wafanyabiashara binafsi kuagiza sukari toka nje na kuondoa ushuru wa forodha ili bei ishuke na pia nimeagiza zitafutwe hekta 25 kwa ajili ya kulima miwa ya kuzalisha sukari,” alisema.

Kwa upande wa bei ya mchele, Rais Kikwete, alisema serikali imeamua kuwa na kilimo cha mpunga katika mabonde yaliyopo na kwamba hekta 1000 zilizopo Kilombero zipatiwe pembejeo ili kupata mpunga wa kutosha.

KODI KATIKA MISHAHARA

Mbali na hayo, Rais Kikwete alisema serikali imesikia kilio cha wafanyakazi kuomba kupunguziwa makato ya kodi ya mapato katika mishahara pamoja na kuongezwa kwa kima cha chini cha mishahara.

“Serikali imesikia kilio chenu cha kupunguziwa gharama za kodi ya mapato katika mishahara na kuongezwa kwa kiwango cha kima cha chini cha mshahara. Nawaahidi kulifanyia kazi katika bajeti inayokuja,” alisema.

Awali akisoma risala ya wafanyakazi nchini, Katibu Mkuu wa Shirikisho la Wafanyakazi (Tucta), Nicholas Mgaya, pamoja na mambo mengine, alisema wafanyakazi wanasubiri kwa hamu tangazo la serikali kuhusu kima cha chini cha mshahara cha Sh. 315,000 kwa mwaka huu wa fedha wa 2012/2013 ambacho hata hivyo walidai kupitwa na muda sambamba na ule wa sekta binafsi.

Mgaya pia alizungumzia punguzo la kodi ya mishahara hadi asilimia 11 kama ilivyo katika nchi nyingine za Afrika Mashariki, kuitaka serikali kutangaza kuimarishwa utekelezaji wa sheria ya wahujumu uchumi na kwamba itambue na kuwahoji wote wenye mali zisizolingana na vipato vyao na watakaoshindwa kuthibitisha wachukuliwe hatua.

Pia aliitaka serikali kuweka miiko ya uongozi inayoeleweka na ipitishwe na Bunge na hatimaye kuingizwa kwenye Katiba ya nchi ili kiongozi atakayeingia madarakani atambue kwamba hatakiwi kwa namna yeyote ile kutumia madaraka yake kujilimbikizia mali.

CHANZO: NIPASHE