VITENDO vya ubadhirifu wa mali za umma,ufisadi na wizi kwa baadhi ya watumishi na viongozi ni moja ya sababu inayoifanya serikali kukosa mapato na hivyo kushindwa kupandisha mishahara ya wafanyakazi.
Hayo yalibainishwa na Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro Bw. Leonidas Gama wakati akizungumza na wafanyakazi Mkoani humo katika siku ya wafanyakazi iliyofanyika katika viwanja vya chuo cha ushirika na stadi za biashara Moshi na kuongozwa na kaulimbiu isemayo Mishahara duni,Kodi Kubwa na Mfumuko wa Bei ni Pigo kwa wafanyakazi.
Bw. Gama alisema “kimsingi ni kwamba mishahara ya wafanyakazi ni midogo na haitoshi lakini inasababishwa na sababu mbalimbali ikiwa ni pamoja na baadhi ya watendaji na viongozi kutokuwa waaminifu hivyo kujihusisha na vitendo vya rushwa na wizi wa mali za umma”.
Aliongeza kuwa Vitendo vya baadhi ya viongozi na watumishi kujiingiza kwenye rushwa na wizi wa mali za umma vimechangia kwa kiasi kikubwa serikali kukosa mapato na hivyo kushindwa kupandisha mishahara ya wafanyakazi.
Kutokuwajibika kwa baadhi ya wafanyakazi na viongozi kikamilifu katika kutekeleza wajibu wao.
“Baadhi ya viongozi kutowajibika ipasavyo,kujiingiza kwenye wizi, Rushwa, ubadhirifu, ufisadi vinachangia kwa kiasi kikubwa serikali kukosa uwezo wa kutoa mishahara mikubwa kwa wafanyakazi,sasa tubadilike tuwajibike ipasavyo ili kukuza uwezo wa serikali kimapato na kuiwezesha kutoa mishahara inayokidhi haja za wafanyakazi”alisema Bw. Gama.
Alisema sababu nyingine inayochangia mishahara duni kwa wafanyakazi ni kudorora kwa uchumi wa dunia kuanzia mwaka 2009 pamoja na kupanda kwa bei ya mafuta duniani.
Akiongelea suala la mfumuko wa Bei Bw. Gama alisema linasababishwa na kuendelea kuwepo kwa biashara za magendo ambapo watumishi wa serikali wanahusika.
“Suala la mfumuko wa bei kwakweli ni tatizo na hili pia linasababishwa na sababu mbalimbali ikiwemo kuendelea kukithiri kwa biashara za magendo,na katika hili watumishi wanahusika kwani katika mipaka ni sisi watumishi tuko lakini pia uzalishaji mdogo katika viwanda vyetu na mazao pia ni tatizo”alisema Bw. Gama.
Alisema ufike wakati sasa wafanyakazi wote na wakulima wakuze uzalishaji na kuwajibika ipasavyo katika nafasi zao kwani bila kutokomeza ufisadi na wizi katika nyanja zote uchumi wa nchi hauwezi kukua.
“Ni wazi kuwa bila kuboresha uzalishaji katika nyanja zote,pato la nchi halitaweza kuongezekana kuongezeka kwa mishahara ya wafanyakazi itakuwa ngumu,ni lazima tukemee ufisadi kwa nguvu zote kwani ufisadi si katika ngazi za juu tu hata katika maofisi yetu ya wilaya mkoa na kwingineko”alisema.
Awali akisoma taarifa ya wafanyakazi katibu wa chama cha walimu mkoani Kilimanjaro (CWT)Bw. Nathaniel Mwandete alisema mishahara duni isiyokidhi mahitaji ya msingi kwa mwezi ni miongoni mwa changamoto mbalimbali zinazowakabili wafanyakazi na kuwafanya kuishi katika mazingira magumu ya kimaisha.
“Kitendo cha kuwalipa wafanyakzi kiasi kidogo cha mishahara kisichokidhi mahitaji ya msngi ya wafanyakazikwa mwezi kinachochea wafanyakazi kutafuta njia nyingine za kujiongezea kipato ili kujaribu kuziba mapungufu katika mahitaji yao ya msingi ya kimaisha na hivyo kusababisha tija na ufanisi mahala pa kazi kuwa katika kiwango cha chini na kuchangia kurudisha nyuma maendeleo ya nchi na taifa kwa ujumla”alisema Bw. Mwandete.
Maadhimisho ya siku ya wafanyakazi duniani huadhimishwa na wafanyakazi wote duniani ikiwa ni kumbukumbu ya kuwakumbuka wafanyakazi wenzao waliojitoa mhanga na kupoteza maisha yao kwa ajili ya kupigania haki,maslahi na hali bora za kazi na kwa mkoa wa Kilimanjaro maadhimisho hayo yalipambwa na wafanyakazi,kampuni na taasisi imbalimbali ikiwemo kampuni ya mafuta ya Panoni ambayo ndiyo kampuni pekee ya mafuta iliyoshiriki maadhimisho hao kwa mara ya kwanza.