Na Mwandishi Wetu, Same
ALIYEKUWA Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Tawi la USa River, Msafiri Mbwambo (36) aliyeuwawa kikatili na watu wasiojulikana amezikwa kijijini Mbwambo wilayani Same.
Akitoa salamu za rambirambi msibani hapo wakati wa mazishi, Mbunge wa Arumeru Mashariki, Joshua Nassari amewaomba wananchi wenye mapenzi mema kuendelea kumuomba Mungu ili wanaodaiwa kuhusika na tukio hilo wapatikane mara moja.
“Mimi sina cha kusema naendelea na mfungo wangu wa siku mbili na kunywa uji tu jioni hadi leo namaliza mfungo huu, ila nanyi niungeni mkono, ili sauti ya wengi ni sauti ya Mungu,” alisema.
Amewataka wakazi wa kijiji hicho kumwachia Mungu na kutolipiza
kisasi kwa aliyefanya hivyo, ili Jeshi la Polisi lifanye kazi yake na hatimaye wahusika kutiwa nguvuni.
Kwa upande wake Mbunge wa Musoma Mjini, Vicent Nyerere, alisema marehemu alikubali kufa kwa sababu ya kutetea haki za watu na hivyo Mungu atampokea na hasa kwa njia ya sala za waliobaki duniani.
Akiendesha ibada ya mazishi, Mchungaji wa Kanisa la Sabato la kijijini hapo, Charles Chagama, alisema dunia kwa sasa inatisha kutokana na binadamu kufanya makosa ya kikatili kama ilivyotokea kwa marehemu.
“Mimi kwangu akija mgeni kama nina kuku na sina mchinjaji niko
tayari kumwomba mtu akanunue samaki nimpikie mgeni ale, ila kifo
hicho Mungu atashughulika na wahusika,” alisema.
Alisema kuwa kila anayeuwa lazima atagharamia gharama ya mauaji anayofanya na hivyo alimtaka kila muumini aombe na kufunga ili wauai wa marehemu apatikane haraka na atiwe hatiani. Akisoma risala ya marehemu mmoja wa familia hiyo, Simon Ngwatu, alisema marehemu alizaliwa mwaka 1974 na kumaliza Shule ya Msingi Kigango Mbwambo mwaka 1989, kisha alifanya kazi za uongozi ndani ya kanisa na baadaye ufundi Ujenzi.
Alisema Marehemu aliuwawa kwa kuchinjwa hapo Aprili 27 mwaka huu, Usa River, Wilayani Arumeru na ameacha mke na watoto watatu.