Rufani ya African Lyon kujadiliwa Mei 2, TFF yaipongeza Simba



*TFF yaipongeza Simba kwa ushindi wa 3-0

Na Mwandishi Wetu

KAMATI ya Nidhamu ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) inatarajia kukutana Mei 2 mwaka huu kujadili rufani iliyowasilishwa mbele yake na klabu ya African Lyon.

Klabu hiyo ya Ligi Kuu inailalamikia TFF ikipinga uamuzi uliofanywa na Kamati yake ya Ligi juu ya kuvunjika kwa pambano la ligi hiyo kati ya Azam na Mtibwa Sugar lililochezwa hivi karibuni kwenye Uwanja wa Chamazi, Dar es Salaam.

Katika rufani yake, Lyon imedai uamuzi uliofanywa na Kamati ya Ligi ya TFF haikuwa sahihi, kwani haukuzingatia kanuni za ligi hiyo kuhusu timu inayogomea mchezo.

Kamati hiyo chini ya Kamishna Mstaafu wa Polisi, Alfred Tibaigana inatarajia kufanya kikao chake kuanzia 8 mchana.
Wakati huo huo; SHIRIKISHO la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) linatoa pongezi kwa timu ya Simba kwa ushindi wa mabao 3-0 ambao iliupata juzi (Aprili 29 mwaka huu) dhidi ya Al Ahly Shandy ya Sudan katika mechi ya Kombe la Shirikisho iliyochezwa Dar es Salaam.

Ushindi huo umetokana na ushirikiano uliopo kuanzia kwa wachezaji, benchi la ufundi, viongozi, wanachama wa klabu hiyo na Watanzania kwa ujumla.

Ni imani ya TFF kuwa Simba haijabweteka kwa ushindi huo na badala yake sasa inajipanga kwa ajili ya mechi ya marudiano itakayochezwa nchini Sudan ili kuondoa Al Ahly Shandy kwenye michuano hiyo na kusonga mbele.

TFF kama kawaida itaendelea kutoa ushirikiano kwa Simba ili kuhakikisha inafika mbali kwenye mashindano hayo, na ikiwezekana kuandikika historia ya kuwa timu ya kwanza ya Tanzania kutwaa Kombe la Shirikisho.

Wakatio huo huo; mikoa sita imeshaomba kuwa wenyeji wa Ligi ya Taifa itakayochezwa katika vituo vitatu tofauti. Ligi hiyo inayoshirikisha mabingwa wa mikoa inatarajia kuanza baadaye mwezi huu.

Kamati ya Mashindano ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) inatarajia kukutana wakati wowote kupitia maombi hayo kabla ya kufanya uamuzi wa vituo na tarehe ya kuanza ligi hiyo.

Mikoa iliyoomba vituo ni Dar es Salaam, Kigoma, Lindi, Mara, Shinyanga na Singida.