Ngorongoro Heroes kwenda Sudan Mei 2

Baadhi ya wachezaji wa Kikosi cha timu ya taifa ya vijana Ngorongoro Heroes

Na Mwandishi Wetu

TIMU ya Taifa ya vijana wenye umri chini ya miaka 20 (Ngorongoro Heroes) inatarajia kuondoka Mei 2 mwaka huu kwenda Sudan kwa ajili ya mechi dhidi ya Sudan itakayochezwa Mei 5 mwaka huu.

Msafara wa Ngorongoro Heroes utakaokuwa na watu 28 ukiongozwa na Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Athuman Kambi utaondoka saa 8.45 mchana kwa ndege ya Kenya Airways.

Ngorongoro Heroes itaagwa rasmi kwa kukabidhiwa Bendera ya Taifa kesho (Mei 2 mwaka huu) saa 5 kamili asubuhi kwenye ofisi za TFF zilizoko Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume.

Wengine katika msafara huo ni wachezaji na benchi la ufundi linaloongozwa na kocha Kim Poulsen. Mechi hiyo ya marudiano namba 16 itachezwa kwenye Uwanja wa Khartoum kuanzia saa 2 kamili usiku kwa saa za Sudan.

Iwapo Ngorongoro Heroes ambayo ilishinda mechi ya kwanza mabao 3-1 itafanikiwa kuitoa Sudan itacheza na Nigeria ambayo yenyewe imefuzu moja kwa moja kucheza raundi ya pili ya michuano hiyo.

Mechi ya kwanza itachezwa Julai 28 jijini Dar es Salaam wakati ya marudiano itafanyika Nigeria kati ya Agosti 10, 11 na 12 mwaka huu. Fainali za U20 kwa Afrika zitafanyika Machi mwakani nchini Algeria.

Wakati huo huo, mechi maalumu ya hisani kwa ajili ya kuchangia timu ya Taifa ya wanawake (Twiga Stars), kati ya timu hiyo na wasanii wa filamu maarufu kama Bongo Movie itachezwa sasa itachezwa Mei 6 mwaka huu badala ya Mei 4 mwaka huu.

Kwa mujibu wa kampuni ya Edge Entertainment iliyoandaa mechi hiyo, imesogezwa mbele kwa siku mbili kutoa fursa kwa watu wengi zaidi kujitokeza kuchangia Twiga Stars. Awali ilikuwa ichezwe Ijumaa ambayo ni siku ya kazi, hivyo imesogezwa hadi Jumapili ambayo ni siku ya mapumziko.

Mechi hiyo itachezwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kuanzia saa 10 jioni ambapo viingilio kwa viti vya rangi ya chungwa, kijani na bluu ni sh. 2,000, VIP C na B itakuwa sh. 5,000 wakati VIP A ni sh. 10,000.

Twiga Stars ambayo kwa sasa haina mdhamini na kambini katika kambi ya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) ya Ruvu mkoani Pwani kujiandaa kwa mechi ya mashindano ya Afrika kwa Wanawake (AWC) dhidi ya Ethiopia.

Timu hizo zitapambana Mei 26 mwaka huu jijini Addis Ababa na kurudiana Juni 16 mwaka huu Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. Mshindi atashiriki fainali za AWC zitakazofanyika Novemba mwaka huu nchini Equatorial Guinea.