Na Mwandishi wetu
Morogoro
INSPEKTA Jenerali wa Polisi (IGP), Said Mwema amewataka watendaji wake kwa kushirikiana na Mamlaka ya Uthibiti wa Usafiri wa Majini na Nchi Kavu (SUMATRA) kubuni njia za kitaalamu kuthibiti ama kupunguza matukio ya ajali za barabarani nchini.
Inspekta Mwema alitoa tamko hilo mwishoni mwa wiki alipokuwa akifunga mkutano wa pamoja kati ya watendaji wa SUMATRA na Jeshi la Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani, ambapo alisema kuwa matarajio ya wananchi ni kuona mabadiliko chanya ya utoaji huduma katika kutatua matatizo yanayoikabili sekta ya usalama barabarani.
Mwema alisema kuwa sababu kubwa inayochangia ajali za barabarani ni makosa ya kibinadamu na huku akiyataja kutaja baadhi kuwa ni kuwa ni vitendo vya uzembe wa madereva, mwendo kasi uendeshaji hatari pamoja na ulevi.
Nyingine ni uzembe wa wasimamiaji wa sheria, na rushwa na kwamba yote yanatakiwa kuthibitiwa kwa kushirikiana na pande zote mbili ili kuhakikisha wimbi la ajali linapungua nchini.
Alisema kuwa kutokana na ongezeko la makosa ya ajali, taasisi hizo mbili na serikali zimekuwa zikilaumiwa na wananchi, na kuwataka wao kama viongozi kila mmoja kujiuliza namna ya kuboresha kikamilifu, usimamizi wa sheria za usalama barabarani na sheria za leseni za usafirishaji.
Aidha alizitaka tasisi hizo kutumia fursa ya leseni mpya ya udereva iliyopo sasa kuwabaini madereva bandia, pamoja na kuboresha uwezo wa madereva kupitia mafunzo ya vyuo vya udereva nchini.
Kwa upande wake Kamanda wa Kikosi cha usalama barabarani nchini (SACP) Mohamed Mpinga alisema kuwa wamefanya maazimio mbalimbali ili kuhakikisha wanathibiti ajali hizo na kuyataja baadhi kuwa ni, (SUMATRA) kuunganishwa katika mfumo wa utoaji leseni za madereva ili kuongeza uthibiti.
Madereva wa mabasi kupewa mafunzo kila baada ya muda kama ilivyo katika sekta za anga na maji ili kuihuisha taaluma, kutoa mafunzo kwa waendesha pikipiki kibiashara, pamoja na kutoa elimu kwa wamiliki na madereva wa mabasi kuhusu kanuni za ufundi na viwango vya huduma.
Kamanda Mpinga aliongeza kuwa ni polisi jamii kutumia ipasavyo kupata taarifa za wakosaji, kuimarisha ukaguzi wa mabasi katika vituo vya mwanzo wa safari, ili yenye matatizo yazuiliwe kabla ya kuanza safari na kuepuka ajali pamoja na usumbufu unaoweza kujitokeza kwa abiria njiani, na kufanya ukaguzi wa kushitukiza mara kwa mara katika njia kuu.