Mawaziri EAC kujadili vigezo vya Sudan Kusini kujiunga na EAC

Wakuu wa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki wakiwa mkutanoni Arusha

*Maraisi wa EAC waagiza kuongezea mamlaka ya Mahakama ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EACJ) kushughulikia uhalifu dhidi ya binadamu

Na Nicodemus Ikonko, EANA-Arusha

WAKUU wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) Jumamosi walitoa maelekezo kwa Baraza la Mawaziri kuleta taarifa ya uhakiki wa vigezo vya kuruhusu kukubaliwa kwa maombi ya nchi ya Sudani Kusini kujiunga na Jumuiya hiyo.Uhakiki huo unatakiwa kuwa tayari ifikapo, Novemba mwaka huu. Muda huo umewekwa na kikao cha faragha cha wakuu hao kilichofanyika mjini Arusha, Tanzania.

Mkutano huo maalum ulihudhuriwa na Marais Mwai Kibaki wa Kenya, ambaye ni Mwenyekiti wa sasa wa Jumuiya hiyo, Yoweri Museveni wa Uganda,Paul Kagame wa Rwanda na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Burundi, Therence Sinunguruza.

Marais hao pia walielezea kusikitishwa kwao na hali ya mgogoro unaoendelea kati ya nchi mpya kabisa barani Afrika ya Sudani Kusini na Jamhuri ya Sudan, na kuwataka viongozi wa nchi hizo mbili kurejea katika meza ya mazungumzo ili kupata suluhisho la amani, alisema Katibu Mkuu wa EAC, Dk. Richard Sezibera alipokuwa anasoma taarifa ya pamoja mwishoni mwa kikao hicho.

Nakala ya taarifa iliyotolewa pia kwa Shirika Huru la Habari la Afrika Mashariki (EANA) imezipongeza juhudi zinazoendelea kufanywa na nchi za EAC katika kuleta suluhisho la amani la mgogoro huo, na kusisitiza kwamba zitaendelea kusaidia kutatua migogoro katika nchi zinazopakana na EAC kwa njia za amani.

Katika hatua nyingijne, viongozi hao wa EAC, wametoa maagizo ya kuongezea mamlaka ya Mahakama ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EACJ) kushughulikia pamoja na mambo mengine uhalifu dhidi ya binadamu.
Wameamuru kufanyia mabadiliko, sheria iliyounda EACJ na Barqaza la Mawaziri la EAC kulifikiria suala hilo kabla ya mwisho wa mwezi ujao, na kuripoti katika kikao maalum kitakachopangwa mara baada ya kupatikana reipoti hiyo.
Pendekezo la kuongezewa mamlaka EACJ limekuja ghafla kutokana na kuongezeka kwa shinikizo nchini Kenya la kukataa kesi ya Wakenya wanne wanaohusishawa na ghasia za uchaguzi mkuu wa mwaka 2007, wasishitakiwe katika Mahakama ya Kimataifa ya Makosa ya Jinai (ICC) iliyopo The Hague, Uholanzi.
Ghasia hizo ziliacha Wakenya 1,300 wakiwa wameuawa, wengine 3,500 kujeruhuiwa na watu wengine hadi 600,000 wakiwa hawana mahali pa kuishi.

Mkutano huo pia umempitisha raia wa Uganda, Jessica Eriyo (43) kuwa Naibu Katibu Mkuu mpya wa EAC kuchukua nafasi ya Beatrice Kiraso ,pia kutoka Uganda, ambaye amemaliza muda wake wa miaka tatu awamu ya pili na ya mwisho. Bibi Kiraso alikuwa Naibu Katibu Mkuu anayeshughulikia Shirikisho la Kisiasa.
Maraisi pia wamemuongezea muda wa kazi kwa miaka mitatu ya mwisho Naibu Katibu Mkuu mwingine wa Jumuiya hiyo kutoka Burundi, Jean –Claude Nsengiyumva.