Ofisi ya Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), Kamishina Robert Manumba, imekumbatia jalada la watuhumiwa waliodai kuwa Naibu Waziri wa Ujenzi, Dk Harrison Mwakyembe, amelishwa sumu na kukataa kuelezea kinachoendelea dhidi ya suala hilo.
Habari za ndani kutoka Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP), zilieleza NIPASHE Jumamosi kuwa jalada hilo limerudishwa kwa Manumba tangu Machi 16, mwaka huu.
Alisema kuwa kinachoendelea mpaka sasa dhidi ya jalada hilo bado hakijafahamika kwani alirudishiwa likiwa na maelezo ambayo anatakiwa kuyafanyia kazi dhidi ya watuhumiwa waliodai kuwa Dk. Mwakyembe amelishwa sumu.
“Hilo jalada limerudishwa kwa Manumba na halipo kwa DPP kuna maagizo alitakiwa kuyafanyia kazi ,” alisema.
Hata hivyo, gazeti hili lilipomtafuta Kamishina Manumba kwa njia ya simu ili aweze kuzungumzia suala hilo alijibu kwa kifupi “sina la kuzungumzia juu ya suala” na kuamua kukata simu.
Awali inadaiwa kuwa DPP, Eliezer Feleshi, alilirudisha jalada hilo kwa Manumba.
Aidha, NIPASHE Jumamosi ilimtafuta Dk. Mwakyembe ili aweze kuzungumzia suala hilo na kueleza kuwa suala hilo halijui na hafahamu kinachoendelea.
Hivi karibuni Manumba akijibu maswali ya waandishi wa habari alisema, uchunguzi uliofanywa na ofisi yake kupitia taarifa kutoka Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, ugonjwa unamsumbua Dk. Mwakyembe hautokani na kulishwa sumu.
Dk. Mwakyembe aliwahi kusema jeshi la polisi limejiingiza kwenye suala ambalo kwa takribani mwaka mzima uliopita, halijawahi kuwa na dhamira ya dhati ya kulielewa au kulichunguza, bali kulifanyia mzaha kupitia magazetini.
Alisema msimamo wa polisi umemkera hasa kutokana na hali aliyonayo ya ugonjwa, akibainisha kuwa umeingilia mchakato wa matibabu yake na uchunguzi wa kina kuhusu kiini cha kuugua.
Alisema inashangaza kuona polisi kupitia kwa Manumba, inaelezea hali ya afya yake na kuhitimisha `kienyejienyeji’ kuwa hakulishwa sumu ila anaumwa ugonjwa wa ngozi bila kufafanua ugonjwa huo umesababishwa na nini.
Dk.Mwakyembe alisema anapata taabu kuamini kama Manumba na maofisa wenzake waliisoma taarifa halisi ya matatibabu yake au walisoma taarifa nyingine.
Alisema kama viongozi hao wa polisi waliisoma taarifa hiyo wenyewe au walisomewa, kwa nini alichokisema Manumba kwa wandishi wa habari hakifanani na picha iliyo kwenye taarifa halisi ya hospitali ya Apollo anakotibiwa nchini India.
CHANZO: NIPASHE