Kamati Kuu cha Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) inakutana jana jijini Dar es Salaam, na moja ya ajenda ikielezwa ni kuendelea kuwabana mawaziri waliotuhumiwa kwa ufisadi katika kikao cha Bunge kilichomalizika wiki hii.
Hata hivyo, akiongea na NIPASHE Jumamosi akiwa ndani ya kikao hicho, Mkurugenzi wa Habari na Uenezi wa chama hicho, John Mnyika, alikanusha kuwepo kwa ajenda hiyo na badala yake alisema ajenda kuu walizojadili ni juu ya ratiba ya uchaguzi wa chama hicho kuanzia matawi hadi ngazi ya Taifa.
Alisema kikao hicho cha Kamati Kuu kilichofanyika katika hoteli ya Mbezi Garden ambacho kilitarajiwa kumalizika jana usiku wa manane ni maandalizi ya kikao cha Baraza Kuu litakalofanyika Aprili 29, mwaka huu.
“Kikao hiki ni cha kawaida, tumejadili mambo ya uchaguzi wa chama chetu na kama kuna hayo tutawaeleza, subiri kesho kwa sababu hatutakuwa na majibu mpaka tutakapomaliza nyakati za usiku sana,” alisema Mnyika.
Pamoja na hayo, habari toka ndani ya kikao hicho zinasema kuwa wajumbe hao wanajadili kwa kina njia ya kuendelea kuibomoa CCM pamoja na kuwabana mawaziri wanane ambao wanahusishwa na kashfa ya matumizi mabaya ya fedha za serikali katika Wizara zao.
“Moja ya kitu ambacho wanakijadili ni kuangalia mafanikio yaliyopatikana katika kuibomoa CCM pamoja na kutoa baraka ya kufanya shinikizo la nguvu ya umma nchini kote kuhakikisha mawaziri ving’anganizi wanaotuhumiwa kwa ufisadi wanajiuzulu,” kilisema chanzo hicho.
Katika taarifa ya chama hicho iliyotolewa juzi ilieleza kikao hicho kitapokea taarifa ya hali ya siasa na kufanya maamuzi muhimu kuhusu mwelekeo wa chama na taifa.
CHANZO: NIPASHE