Na Mwandishi Wetu
KAMATI ya Ligi ya TFF imewafungia mechi tatu na kuwapiga faini y ash. milioni mmoja kila mmoja wachezaji tisa wa timu ya Polisi Dodoma baada ya kumpiga mwamuzi Martin Saanya kwenye mechi dhidi ya Azam iliyochezwa Aprili 14 mwaka huu mjini Dodoma.
Wachezaji hao walioadhibiwa kwa mujibu wa kanuni ya 25(g)(iii) ni Noel Msekwa, Frank Sindato, Abdallah Matila, Bantu Admin, Salmin Kisi, Madope Mwingira, Sihaba Mkude, Kaliyasa Mashaka na Ibrahim Massawe.
Iwapo wachezaji hao watahama Polisi na kujiunga na timu nyingine, watahama na adhabu zao.
Vilevile timu ya Polisi Dodoma imepigwa faini ya sh. 500,000 kutokana na vurugu za washabiki wake katika mechi hiyo iliyochezwa Uwanja wa Jamhuri. Pia timu hiyo imepewa barua ya onyo kwa kuchelewa kufika uwanjani kwenye mechi dhidi yao na Yanga iliyochezwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Wakati huo huo; mechi ya kirafiki ya kimataifa kati ya timu ya Taifa ya wanawake (Twiga Stars) na Zimbabwe iliyokuwa ichezwe Aprili 28 mwaka huu kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam imefutwa.
Uamuzi huo umefanywa na Chama cha Mpira wa Miguu Zimbabwe (ZIFA) ambayo sasa imeamua kucheza mechi ya kirafiki na Zambia. Mechi hiyo itachezwa Aprili 28 mwaka huu jijini Harare.
Twiga Stars inaendelea na mazoezi chini ya kocha wake Charles Boniface Mkwasa katika kambi ya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) iliyoko Ruvu mkoani Pwani.
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) linaendelea na jitihada za kuitafutia mechi za kirafiki Twiga Stars kabla ya kucheza mechi ya mashindano dhidi ya Ethiopia ambayo itafanyika Mei 26 mwaka huu jijini Addis Ababa.