TAWLA kusaidia wanawake, watoto kisheria

Na Tiganya Vincent,
MAELEZO-Dar es Salam

Chama cha Wanasheria Wanawake Tanzania (TAWLA) kimeahidi kuendelea kutoa msaada wa kisheria kwa wanawake na watoto wengi wanaokandamizwa pindi wanapokuwakidai haki zao za msingi ili kujenga jamii inayozingatia haki na usawa kwa jamii yote.

Kauli hiyo ilitolewa jana jijini Dar es Salaam na Mwenyekiti wa TAWLA Marie Kashonda wakati akiongea na waandishi wa habari juu ya mafanikio waliopata katika kipindi cha miaka 21 ya huduma za msaada wa kisheria kwa wanawake na watoto nchini.

Alisema kuwa kimsingi wamefanikiwa kuhakikisha kuwa wanawake wanashirikishwa katika masuala ya ardhi mara baada ya kuboresha Sheria ya Ardhi ambapo wengi wao wameweza kumiliki ardhi na kushiriki katika vikao vya mabaraza ya kata ya ardhi.

Kashonda aliongeza kuwa pia wamesaidia wanawake kupata haki zao zilizosbabishwa na ukatili au unyanyasi majumbani mwao (domestic violence).

Kwa mujibu wa Mwenyekiti huyo alisema kuwa hivi sasa wanaendelea na harakati ya kushiriki katika mchakato wa kuunda Katiba mpya ambayo itazingatia haki za wanawake na watoto zinaingizwa katika Katiba mpaya ili kuleta maendeleo yanayozingatia usawa wa kijinsia.

Alizitaja haki ambazo wanapigani ni pamoja na haki ya mwanamke kumili ardhi sawa na mwanaume, haki ya watoto wa kike kwenda shule na kutoolewa katika umri mdogo ili kuwakinga na kujiingiza katika matendo maovu.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa TAWLA Annamarie Marajina alisema kuwa Chama hicho kitaendelea kuwajengea uwezo wanachama wake ili waendelee kusaidia wanawake na watoto kisheria ili sheria zote zinazowakandamiza ziondolewe.

Alisema sanjari na usaidizi huo wataendelea na utafiti wa maeneo mbalimbali ambayo wanaona yana mapungufu ili waweze kutoa mapendekezo yatakasaidia kuboresha hali ya upatikanaji wa haki kwa kuzingatia usawa wa kijinsia na misingi ya utawala bora.

Mkurugenzi Mtendaji huyo alisema kuwa hadi hivi sasa TAWLA imefanikiwa kuwasaidia zaidi ya wanawake 10,000 nchini kote ambapo baadhi yao wamepata haki zao na wengine kesi zao zinaendelea.

Alisema kuwa lengo lao ni kuhakikisha kuwa wanaelimisha jamii na kuwasaidia wanawake na watoto ili umiliki wa ardhi uwe kwa wote na kwa manufaa ya jamii yote bila kujali tofauti ya kijinsia.

Annamarie alisema kuwa wanapoadhimisha miaka 21 tangu TAWLA ilianzishwa wataendelea na jukumu lao kubwa la kuhakikisha kuwa wanawake na watoto napata haki zao za msingi .

TAWLA ilianzishwa mwaka 1989 na kusajiliwa rasmi mwaka 1990 ambapo hivi sasa inayo matawi katika mikoa ya Tanga, Dar es Salaam, Dodoma na Arusha.