Wananchi Same watembea kilomita 50 kusaka huduma za afya

Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii Tanzania, Dk. Haji Mponda

Na Mwandishi Wetu-dev.kisakuzi.com, Same

WANANCHI wa Kata ya Mamba Myamba Wilaya ya Same mkoani Kilimanjaro, hulazimika kutembea umbali wa takribani kilometa 50 kutafuta huduma ya afya iliyopo Same Mjini kutokana na eneo lao kutokuwa na huduma hiyo.

Wakizungumza na mtandao huu baadhi yao wamesema ukosefu wa kituo cha afya imekuwa ni kero kubwa kwao kwani wananchi wengi hasa akinamama wajawazito hupoteza maisha wakati mwingine wakiwa njiani kuelekea hospitalini.

Kimaro Maine ni ambaye ni mkazi wa kata hiyo alisema wamekuwa wakitaabika kutafuta matibabu hasa wananchi wa kipato cha chini ambao hawana fedha za usafiri hadi Mjini Same ambako hutumia zaidi ya sh. 30,000 kutoka katika kata hiyo hali ambayo huwafanya wengi kupoteza maisha njiani.

Mwananchi huyo alitoa kero hiyo kwenye mkutano wa hadhara na Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Leonidas Gama aliyekuwa na ziara ya kukagua miradi ya maendeleo katika wilaya ya Same.

Alisema katika baadhi ya vijiji vya kata hiyo kuna zahanati lakini tatizo kubwa ni wahudumu ambapo wananchi hufika na kukosa huduma na kuamua kurudi nyumbani na kwa walio na uwezo kwenda hospitali ya wilaya iliyoko mjini Same.

“Katika vijiji vyetu na kata maafisa mifugo wapo na mifugo inaangaliwa vizuri na kwa umakini mkubwa, lakini cha kushangaza binadamu ambao ni muhimu kushinda hao mifugo tunataabika, hatuna wataalamu wa afya wala vituo vya afya, lakini pia vyombo vya usafiri kwenda katika hospitali hiyo ya mbali navyo ni shida na hali hii husababisha wagonjwa kubebwa na machela,” alisema Kimaro.

Waliiomba Serikali kuangalia uwezekano wa kuwajengea kituo cha afya na kuweka watumishi ili kuwaondolea adha hiyo ambayo ni kikwazo kikubwa katika maisha yao.

Akijibu kero hiyo Mkuu wa Mkoa, Gama alisema suala la ujenzi wa kituo cha afya liko mikononi mwa wananchi wenyewe hivyo ni jukumu lao kukaa chini na kujipanga kutafuta eneo na kuomba ramani katika halmashauri na watakaposhindwa ndipo waiombe serikali iwaunge mkono.

“Ndugu zangu wananchi msifike mahala mkasema mnaisubiri serikali ije iwajengee kituo cha afya au zahanati, hatua hizo zitachukua muda mrefu sana kwani mpaka ratiba ipangwe iwafikie ni mudamrefu na mtakuwa mnazidi kutaabika, cha msingi ninyi wenyewe jipangeni, tafuteni eneo na muombe ramani halmashauri na baada ya hapo anzeni ujenzi na mkifika mahali mkikwama mkituambia tunaweza kuwasaidia,” alisema Gama.