UVCCM Arusha wasema waliomtuhumu Millya ni mamluki

Aliyekuwa Mwenyekiti wa UVCCM Mkoa wa Arusha, James Millya

Na Mwandishi Wetu, Arusha

JUMUIYA ya Umoja wa Vijana wa CCM mkoani Arusha umesema baadhi ya wanachama waliojitokeza na kumtuhumu aliyekuwa Mwenyekiti wa Umoja huo Mkoa wa Arusha, James Millya kwamba ametoweka na fedha za SACCOS sh. milioni mbili si wanachama na hawajui chochote ndani ya umoja huo.

Akizungumza na mtandao huu jana Katibu wa UVCCM Arusha Abdallah Mpokwa amesema waliojitokeza katika vyombo vya habari ikiwa ni siku chache baada ya Millya kuhamia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), na kudai kiongozi huyo ameondoka na fedha za UVCCM ni mamluki kwani walisha timuliwa ndani ya umoja huo muda mrefu.

Kiongozi huyo mtendaji wa umoja huo Arusha amepinga UVCCM kuwa na SACCOS kama walivyodai mamluki hao, ameshangazwa na watu hao wamezungumza kama akina nani ilhali Jumuiya haiwatambui.

Siku chache baada ya Millya kuihama CCM, walijitokeza Mrisho Gambo (Mjumbe Baraza Kuu CCM Taifa), Kennedy Mpumilwa (Mjumbe UVCCM Wilaya ya Arumeru) na mwenzao Salome Hatibu wakimtuhumu Millya kutoweka na fedha na kutokabidhi ofisi.

“Mimi ninachosema haya matamko yanatolewa na watu tusiowatambua katika
Umoja wetu, huyu Gambo alifukuzwa katika kikao chetu tulichofanya
longido na hatumtabui sasa anatoa matamko kama nani,” alisema Mpokwa.

Hata hivyo amepinga suala la Millya kutakiwa kukabidhi ofisi mara
alipoondoka na kujiunga na CHADEMA, ambapo alisema Millya, kisheria hakuwa na ofisi zaidi ya kuhusika katika ufunguzi wa vikao na mikutano.

Akifafanua suala la SACCOS Katibu huyo alisema hakuna SACCOS yoyote inayoendeshwa na ofisi hiyo hivyo anawashangaa watu walioibuka na kudai kuna kitu kama hicho ndani ya Jumuiya hiyo mkoani Arusha. Aidha ameongeza kuwa kujiengua kwa Millya hakuja punguza chochote ndani ya UVCCM Arusha na kila mmoja ana haki ya kuingia na kutoka ilimradi asivunje wala kukiuka taratibu ndani ya UVCCM.