Na Mwandishi Wetu
LIGI Kuu ya Vodacom imeingia raundi ya 25 ambapo kesho (Aprili 25 mwaka huu) Oljoro JKT itaikaribisha Yanga kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Sheikh Kaluta Amri Abeid jijini Arusha wakati JKT Ruvu itakuwa mwenyeji wa Ruvu Shooting kwenye Uwanja wa Chamazi, Dar es Salaam.
Raundi hiyo itakamilika kwa mechi nne; Aprili 28 mwaka huu Coastal Union itakuwa mwenyeji wa Kagera Sugar kwenye Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga huku Mtibwa Sugar ikiwa mgeni wa African Lyon kwenye Uwanja wa Chamazi.
Azam na Toto African zitacheza Chamazi, Aprili 30 mwaka huu wakati Mei 1 mwaka huu Villa Squad itaumana na Oljoro JKT kwenye Uwanja wa Chamazi.
Ligi hiyo itafunga msimu wa 2011/2012, Mei 5 mwaka huu ambapo timu zote 14 zitakuwa uwanjani. Simba vs Yanga (Uwanja wa Taifa), Oljoro JKT vs Polisi Dodoma (Sheikh Kaluta Amri Abeid, Arusha) na Ruvu Shooting vs Villa Squad (Mabatini, Mlandizi).
Mechi nyingine zitakuwa kati ya Coastal Union vs Toto African (Mkwakwani, Tanga), African Lyon vs JKT Ruvu (Manungu, Morogoro), Azam vs Kagera Sugar (Chamazi, Dar es Salaam) na Moro United vs Mtibwa Sugar (Jamhuri, Morogoro).
Wakati huo huo; mechi ya Ligi Kuu ya Vodacom kati ya Yanga na Polisi Dodoma iliyochezwa (Aprili 22 mwaka huu) kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam ilishuhudiwa na watazamaji 1,635 na kuingiza sh. 5,666,000.
Baada ya kuondoa gharama za awali za mchezo na asilimia 18 ya Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) ambayo ni sh. 864,305.08 kila klabu ilipata sh. 193,858.47, uwanja sh. 26,469.49.
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) sh. 26,469.49, Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA) sh. 108,687.80. Mfuko wa Maendeleo ya Mpira wa Miguu (FDF) sh. 13,234.75, Baraza la Michezo la Taifa (BMT) sh. 2,646.95 na asilimia 10 ya gharama za mechi ni sh. 26,469.49.
Gharama za awali za mechi zilikuwa nauli ya ndani kwa waamuzi sh. 10,000, nauli ya ndani kwa kamishna wa mchezo sh. 10,000. Mwamuzi wa akiba sh. 30,000, posho ya kujikimu kwa kamishna na waamuzi sh. 160,000, gharama ya tiketi sh. 1,500,000, usafi na ulinzi kwa uwanja sh. 1,500,000 na Wachina (Beijing Construction) sh. 1,000,000.
Kutokana na mechi hiyo kuingiza kiasi kidogo baadhi ya gharama zililipwa nusu au kutolipwa kabisa na kuacha madeni. Madeni hayo ni tiketi sh. 1,500,000, maandalizi ya uwanja (pitch marking) sh. 400,000, umeme sh. 300,000, usafi na ulinzi kwa uwanja sh. 850,000 na Wachina sh. 1,000,000.