Iddi Simba adai fidia bil.12

Ndg. Iddi Simba

Aliyekuwa Mwenyekiti wa mradi wa ujenzi wa Machinjio, Idd Simba, amefungua kesi ya kutaka kulipwa kiasi cha Sh bilioni 12 kwa madai ya kudhalilishwa katika vyombo vya habari.

Kesi hiyo ambayo imefunguliwa katika Mahakama Kuu dhidi ya gazeti la Mtanzania na kulitaka limlipe fedha hizo kama fidia.

Katika kesi hiyo iliyofunguliwa kupitia kwa wakili wake, Alex Mgongolwa, anadai kudhalilishwa na gazeti hilo katika maoni ya Mhariri yaliyochapishwa na gazeti hilo la Machi 30 mwaka huu.

Anadai kuwa gazeti hilo lilimuandika mteja wake kuwa ni mbadhirifu, mwizi, amehusika na kashfa ya UDA, kampuni hewa ya machinjio jijini Dar es Salaam hivyo akamatwe afungwe, habari alizodai kuwa hazikuwa na ukweli wowote.

Alieleza kuwa hakuna chombo chochote kilichowahi kumtia hatiani hivyo analitaka gazeti hilo limlipe Sh 12 bilioni ambazo ni gharama zote na kwamba gharama za kesi hiyo zilipwe na wadaiwa.

Anadai kuwa habari hizo zililenga kumchafua mteja wake kwani ni mtu safi anayeheshimika ndani na nje ya nchi, amefanya kazi nyingi za umma, ni mwanasiasa mstaafu na mfanyabiashara mwenye uelewa wa juu katika mambo mbalimbali.

Katika hati hiyo ya madai, pia amenukuu vifungu mbalimbali vilivyochapishwa katika maoni hayo ambavyo alidai kuwa vyote vililenga kumchafua.

“Huyu Idd Simba aliyekuwa mbunge wa Ilala na baadaye alikuwa miongoni mwa wagombea wa Chama cha Mapinduzi akiomba ateuliwe kuwa Rais wetu tusingepona. Huyu ni miongoni mwa viongozi walafi wasiotosheka ambao wako tayari kuona watu wanateseka huku wao wakistarehe na kuponda maisha,”ilisema sehemu ya maoni hayo.

“Idd Simba ambaye amehusishwa pia na kashfa ya UDA yuko nyuma ya kadhia hii, sisi tunashangaa kwanini hajakamatwa na kushtakiwa,”ilieleza sehemu ya maoni hayo ambayo yamo pia kwenye hati ya madai.

Hata hivyo, alidai fidia hiyo italipwa na mhariri wa gazeti hilo na kumuomba radhi mteja wake kupitia ukurasa wa mbele.

Alidai kuwa habari hizo zilikuwa za uongo na zenye lengo la kumchafua mteja wake mbele ya jamii kwani gazeti hilo lilichapishwa na kusambazwa mikoa mbalimbali nchini.

CHANZO: NIPASHE JUMAPILI