Mbunge wa Temeke (CCM), Abbas Mtevu, na watu wawili akiwemo dereva wake wamenusurika kifo baada ya gari walilokuwa wakisafiria kupinduka katika kijiji cha Tabu Hotel kilometa nne kutoka makao makuu ya Wilaya ya Gairo mkoani Morogoro.
Ajali hiyo imetokea wakati Mtemvu akitokea Dodoma kuelekea jijini Dar es Salaam ambapo ghafla gari lake lilipata ajali.
Kaimu kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Joseph Rugia, alisema ajali hiyo aimetokea saa 11:00 jana alfajiri baada ya gari hilo lenye namba ya usajili T982 BKQ aina ya Toyota Land Cruser lilokuwa likiendeshwa na Hussen Rashid (30), mkazi wa Dar es Salaam lilopofika katika eneo hilo na kupinduka.
Alisema chanzo cha gari hilo kupinduka ni utelezi uliosababishwa na manyunyu ya mvua na hivyo kusababisha dereva ashindwe kulimudu na kwenda kugonga ngema ya ukuta na kupinduka.
Alisema Mtevu na dereva pamoja na mtu mwingine ambaye hajafahamika jina walijeruhiwa na kuokolewa na wasamaria wema wanaoishi katika eneo hilo na baadaye kukimbizwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Morogoro.
Mmoja wa mashuhuda, Gibson Malanda, Mkazi wa kijiji cha Tabu Hotel, alisema chanzo cha ajali hiyo ni mwendo kasi wa gari hilo uliosababisha mpira wa mbele kupasuka na baadaye kuyumba na kukosa mwelekeo kabla ya kupinduka.
“Wakati linakuja hilo gari la Mbunge mimi nilikuwa barabarani na lilikuwa na mwendo kasi, ghafla taili la mbele likapasuka dereva akafunga breki, lakini likamshinda na kuyumba na baadaye kupinduka.
Mganga Mfawidhi wa Hospitali hiyo, Dk. Marco Nkya, alisema hali zao zilikuwa nzuri na kwamba walipata michubuko katika sehemu za mikono na kupatiwa matibabu na baadaye kuruhusiwa kuendelea na safari yao ya jijini Dar es salaam kwa usafiri mwingine.
CHANZO: NIPASHE