Jumla ya Shilingi bilioni 71 zatumika kununua karafuu Unguja na Pemba,

Dr Shein akiongea na wananchi wakulima wa karafuu(hawapo pichani)

Na mwandishi wetu

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein ametoa wito kwa wananchi wa Zanzibar hasa wakulima wa zao la karafuu kutoweka fedha zao majumbani na badala yake waweke kwenye mabenki yaliopo nchini kwa ajili ya usalama wa fedha zao.
Dk. Shein aliyasema hayo mara baada ya kutoa zawadi ya vyeti maalum kwa wanunuzi bora wazalendo wa zao la karafuu msimu huu wa mwaka 2011-2012, hafla iliyofanyika huko katika uwanja wa Jamuhuri, Wete Pemba.
Katika maelezo yake, Dk. Shein alisema kuwa ni vyema wakulima baada ya kuuza karafuu zao waweke fedha zao benki badala ya majumbani kwani inasemekana fedha nyingi walizozipata wananchi katika kuuza karafuu wameiweka majumbani.
Alisema kuwa ni jambo la busara kuweka fedha zao katika benki yoyote wanayoitaka wenyewe ikiwemo benki yao ya PBZ na hata benki nyenginezo kwa ajili ya usalama wa fedha zao na hata wao wenyewe.
Amesema kuwa bilioni 71 zimetumika katika kununua karafuu Unguja na Pemba, hali ambayo imewapelekea wananchi walio wengi kufaidika na fedha hizo kutokana na kuuza karafuu zao katika vituo vya ZSTC. Alisema kuwa sheria ya karafuu itatengenezwa upya ili iweze kukidhi haja pamoja na mazingira yaliopo hivi sasa.
Rais Dk. Shein aliwapongeza wananchi kwa kushirikiana na serikali katika kuhakikisha zao hilo wanawauzia Shirika la ZSTC na kueleza kuwa lengo la Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, ni kuwa na bajeti itakayokuwa haina tegemezi kutoka upande wowote.
Aidha, Dk. Shein alilitaka Shirika la ZSTC kuhakikisha linatafuta mbinu za kuviimarisha vituo vya kununulia karafuu kwa kuhakikisha vinatoa huduma muhimu zikiwemo vyoo, samani, maji, umeme na huduma nyenginezo.
Pamoja na hayo, Dk. Shein aliwaeleza wananchi na wakulima wa zao la karafuu kuwa Serikali itafanya juhudi ya kuhakikisha kuwa barabara kadhaa hasa zile zinazoelekea katika maeneo yanayozalisha karafuu kwa wingi zinatengezwa japo kwa kiwango cha kifusi ili iwe rahisi kusafirisha zao hilo wakati wa mvua na hata wa jua.
Dk. Shein alisema kuwa serikali itaanzisha mfuko wa kuendeleza zao la karafuu na kuupitia upya utaratibu wa kuwapa fidia wananchi pamoja na kuhakikisha kwwamba mapungufu yote yaliokuwepo kabla ya kusita utaratibu huo yanafayiwa kazi.
Pia, Dk. Shein aliupongeza Mkoa wa Kaskazini Pemba kwa kuongeza idadi kubwa ya zao la karafuu ambalo zimenunuliwa na ZSTC mwaka huu na kufikia tani 2285 ambapo mwaka jana karafuu zilizonunuliwa katika Mkoa huo zilikuwa tani 25 tu.
Dk. Shein alimpongeza Waziri ya Biashara pamoja na watendaji wake kwa hatua iliyofikiwa ya mafanikio pamoja na kupongeza Kikosi kazi maalum, vikosi vya ulinzi na usalama pamoja na wananchi wenyewe ambao pia walichangia kupambana na magendo.
Sambamba na hayo, Dk. Shein alieleza kuwa mbali ya zao la karafuu pia, sekta ya utalii nayo imefanikiwa kutokana na wageni wegi kuja kutembelea Zanzibar na kusisitiza kuwa mikopo iliyokopeshwa Zanzibar uwezo wa kuilipa yote upo na Zanzibar hivi sasa inakopesheka na hakuna aliyepata hasara huku serikali ikiwa imepata fedha ambazo zitatumika kwa ajili ya kuimarisha maendeleo nchini.
Wauzaji waliopewa vyeti hivyo maalum ni kutokana na kuuza zao hilo kwa ZSTC ni Bwana Hamad Said Hamad,Said Ali Juma, Hussein Khamis Jabu na Mohammed Issa Salim ambapo Mkoa Bora ni Mkoa wa Kusini Pemba na Wilaya Bora ni Wilaya ya Wete.
Na kwa upande wa Shehia, Shehia bora ya kwanza ni Shehia ya Selem, ikifuatiwa na Shehia ya Finya, Mtambile na Ziwani.
Wakati huo huo, Dk. Shein ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri kuu ya CCM Taifa aliweka jiwe la msingi Tawi la CCM Kinyasini na kuwataka wana CCM kujitolea kuimarisha kazi za chama ikiwa ni pamoja na kuchangia ujenzi wa Matawi.
Aidha, Dk.Shein aliwasihi wana CCM kujua kwamba Wazanzibari wote ni wamoja hivyo itikadi za vyama zisiwagombanishe jambo la muhimu ni kuelewa kuwa Serikali ni moja lakini kila mmoja anachama chake na kusisitiza kuwa katika serikali hamna upinzani na kuwataka Wana CCM kutobweteka na badala yake waendelee kukimarisha chama hicho.
Pia, aliweka jiwe la msingi katika Afisi ya la CCM Jimbo la Tumbe na kupata maelezo juu ya ujenzi wa tawi hilo ambalo aliahidi kuunga mkono kumalizia ujenzi wake ambapo katika ujenzi wa Tawi la Kinyasini, Dk. Shein aliahidi kutoa msaada wake kwa kuliezeka tawi hilo pamoja na kutia madirisha na mlango wa nyuma wa mbele na kutia rangi