Na Mwandishi wetu.
WAKULIMA mkoani Kilimanjaro wameiomba serikali kuangalia uwezekano wa kuzuia usafirishaji mazao ya nafaka kwenda nje ya nchi ikiwa ni pamoja na kuongeza nguvu katika kudhibiti matumizi ya nafaka kutengenezea pombe hatua ambayo itasaidia kuwepo kwa chakula cha kutosha nchini na kupunguza tatizo la njaa ambalo limeanza kuwakabili baadhi ya wananchi mkoani humo.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti na gazeti hili wakulima hao walisema kwa sasa hali ya chakula katika mkoa wa kilimanjaro hususani maeneo ya ukanda wa chini bado ni mbaya kutokana na kuendelea kuwepo kwa ukame unaosababishwa na ukosefu wa mvua.
Walisema pamoja na mamlaka ya hali ya hewa kutangaza kuwepo kwa mvua nyingi katika kipindi hiki cha masika mvua hizo zilinyesha chache na kukatika hivyo kusababisha hasara kubwa kwa wakulima wengi waliopanda mapema kuwahi mvua za kwanza baada ya mazao kukauka .
Akizungumza Prf. Willy Makundi mmoja wa wakulima mkoani Kilimanjaro alisema kuna haja ya serikali kurudisha zuio la kuzuia mazao ya nafaka kusafirishwa kwenda nje ya Nchi hadi pale ambapo kutakuwa na uhakika wa upatikanaji wa chakula cha kutosha hapa nchini.
alisema hali ya chakula katika maeneo mengi mkoani Kilimanjaro si nzuri kutokana na kukosekana kwa mvua za kutosha kwa muda mrefu sasa hivyo ni vema serikali ikajipanga kukabiliana na tatizo hilo ambalo ni kubwa katika maeneo ya ukanda wa chini ambao wanategemea kilimo cha mvua.
“Pamoja na serikali kuondoa zuio na kuruhusu mazao ya nafaka ikiwemo mahindi kwenda nje ya nchi bado hali ya chakula hapa nchini si nzuri,maeneo mengi katika mkoa wetu wa Kilimanjaro kwa sasa yameanza kukumbwa na njaa na hakuna uhakika wa kupata mavuno kwa kipindi hiki kwani mvua zimekatika na mazao mengi yamekauka”alisema Prf. Makundi.
Alisema serikali ifike mahali sasa ijiandae kwa dharura na kuweka mipango madhubuti ya kukabiliana na tatizo la njaa katika mkoa wa Kilimanjaro hasa maeneo ya ukanda wa chini ambayo yameanza kuathirika na kuhitaji chakula cha msaada kutokana na kukosa mavuno kwa msimu ulichopita wa vuli.
Aidha alisema pamoja na serikali kurudisha zuio na kudhibiti utengenezaji wa pombe kwa kutumia nafaka pia ihamasishe wananchi kutumia vizuri chakula walichonacho ili kuwezqa kukabiliana na tatizo la njaa ambalo limmeanza kuyakumba baadhi ya maeneo.
Alisema kuna haja pia ya serikali kuhamasisha wakulima wa kilimo cha umwagiliaji kulima mazao ya chakula kama mahindi kutokana na kwamba wakulima wengi wa umwagiliaji hukimbilia kwenyekilimo cha mazao ya biashara kama Nyanya,Vitunguu,Karoti na pilipili hoho hivyo kushindwa kuwezesha kupatikana kwa uhakika wa chakula.
“Serikali inakila sababu ya kurudisha zuio la usafirishaji mazao ya nafaka kwenda nje kwani kwa sasa hali ni mbaya katika baadhi ya maeneo hapa nchini,lakini pia Nchini kenya,Somali na sudani ya kusini pia hali ni mbaya,na serikali isipojipanga vizuri nasi Tanzania tutaanza
kulia njaa na kutafuta misaada siku si nyingi”alisema.
Akizungumzia hali ya kilimo katika mkoa wa Kilimanjaro mwenyekiti wa wafanyabiashara wenyeviwanda na Kilimo mkoani Kilimanjaro (TCCIA)Bw. Patrick Boisafi alisema hali ya kilimo kwa sasa si nzuri kutokana na kuwepo kwa hali mbaya ya Hewa hivyo kuna haja ya watanzania wote kubadilika na kuyatunza mazingira ili kuwezesha mvua kunyesha kwa
wakati.
Hivi karibuni akielezea hali ya chakula kwa Rais wa jamuhuri ya muungano wa Tanzania Dkt.. Jakaya Mrisho Kikwete mkuu wa mkoa wa Kilimanjaro Bw. Leonidas Gama alisema mkoa wa Kilimanjaro unakabiliwa na upungufu wa chakula Tani 88,348 aina ya wanga na tani 9,809 za
protini.