Lugha ya Kiingereza ambayo ni rasmi kwa shughuli za Bunge la Afrika Mashariki jana ilikuwa kikwazo kwa baadhi ya wagombea waliokuwa wanaomba nafasi za kuiwakilisha nchi katika chombo hicho cha Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Dalili za lugha hiyo kuwa kikwazo kwa baadhi ya wagombea zilianza kuonekana awali baada ya baadhi ya wabunge kutaka Kiswahili kitumke kujieleza, ingawa hoja hiyo ilikataliwa kwa kuwa kanuni zinahitaji Kingereza kitumike.
Kutokana na hali hiyo, baadhi ya wagombea walionekana wakijitutumua kusaka maneno ya kujieleza ndani ya Bunge wakati wa kuomba kura, kiasi cha wengine kushindwa hata kuelewa vema maswali waliyokuwa wanaulizwa na wabunge.
Kutokana na kubabaika huko baadhi ya wabunge walilazimika kurudia maswali yao kwa baadhi ya wagombea ambao hata hivyo hawakujua walichoulizwa.
Mbali na kutaka Kiswahili kitumike, baadhi ya wabunge walitaka kila mgombea kutumia dakika tatu badala ya tano kujieleza.
Shughuli ya kuwahoji wagombea hao ilianza mara baada ya kipindi cha maswali na majibu 10: 30 asubuhi kwa Spika kutoa ufafanuzi wa namna uchaguzi huo utakavyofanyika.
Wagombea hao 34 walihojiwa hadi saa 10:20 jioni zoezi la kupiga kura lilipoanza.
Spika alitumia muda mwingi kujibu hoja zilizotolewa na wabunge wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) waliokuwa wakitaka chama chao kipewe nafasi moja ya ubunge kutokana na wingi wao bungeni.
Vile vile, Spika Makinda alitumia muda mrefu kuwaonya wabunge kuchagua wagombea kwa kuweka mbele maslahi ya taifa na wasiongozwe na ushabiki.
Aliwaeleza wabunge kuwa lazima wawe makini na wachague wawakilishi wenye uwezo mkubwa kwani wabunge hao ndio wanakwenda kuwakilisha nchi.
“Hawa tunaowachagua leo ndio wanakwenda kutuwakilisha kama nchi, kwa hiyo lazima tuangalie sifa na uwezo wa wagombea tunaowapeleka kutuwakilisha na tusipofanya hivyo itakula kwetu, waheshimiwa wabunge naomba muwe makini kwelikweli,” alionya Makinda.
MWAKYEMBE ATOA ANGALIZO
Kabla ya wagombea kuanza kuhojiwa, Naibu Waziri wa Ujenzi, Dk. Harrison Mwakyembe, alisimama kuomba mwongozo wa Spika huku akiwatahadharisha wabunge kuhusu wagombea gani wanapaswa kuchaguliwa kwenye uchaguzi huo.
Dk. Mwakyembe alisema hadhi ya Tanzania katika Bunge hilo la Afrika Mashariki imeshuka kutokana na kuchagua wawakilishi wasio na ubora kulinganisha na nchi zingine zilizo kwenye Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Alimweleza Spika kuwa kuliko wagombea wajieleze kwa dakika tano ni kheri wakazungumza kwa dakika tatu ili upatikane muda wa kutosha kuwahoji maswali matatu ili kupima uwezo wao wa kielimu.
“Mheshimiwa Spika wagombea wengine ni mahiri wa kukariri mambo, wanaweza kuja hapo wakazungumza, wakajieleza vizuri tukawachagua kumbe hawana kitu, ni heri tutumie muda kuwauliza maswali matatu yawe ya lazima tujue uwezo wao,” alisema.
Kadhalika, Mwakyembe alisema kuwa amesikia kupitia vyombo vya habari kuwa baadhi ya wagombea wamekuwa wakitembeza rushwa ili kushawishi kuchaguliwa.
Alionya hali hiyo ni ya hatari sana na inaweza kuathiri uwakilisha wa nchi katika chombo hicho cha kutunga sheria cha Afrika Mashariki.
“Naomba tuwaulize maswali matatu kama wengine hamtakuwa na maswali tuachieni sisi walimu tutawauliza hayo maswali ili tujue uwezo wao,” alisema na kushangiliwa.
Spika Makinda alikubaliana na ushauri wa Dk. Mwakyembe na kusema wagombea watajieleza kwa dakika tatu na si tano kama ilivyopangwa awali na kisha wataulizwa maswali matatu.
Hoja ya Dk. Mwakyemba kuwa Bunge limechafuka kwa rushwa, imekuja siku moja baada ya Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, kusema kuwa wagombea wengi wamewahonga wabunge ili wawachague.
Mbowe alisema baadhi ya wabunge wamehongwa hadi Sh. milioni mbili ili wawapigie debe wagombea kwa wenzao ili wawachague.
Alisema ana ushahidi wa namna wabunge walivyohongwa kwani hata wabunge wa Chama chake walifuatwa na kushawishiwa wachukue rushwa ili wawachague wagombea hao.
KUNDI LA WANAWAKE.
Kundi la kwanza kuhojiwa ni kundi la wanawake, lenye mchanganyiko wa wagombea wote wa vyama vya siasa vyenye usajili wa kudumu. Katika kundi hili, wabunge walitakiwa kupiga kura mbili.
Wa kwanza kuhojiwa katika kundi hilo alikuwa Shyrose Bhanji (CCM), ambaye alielezea uzoefu wake katika taasisi mbalimbali alizofanyakazi.
Mwingine ni Dk. Kokubanza Kinyondo na Angelah Kiziga (CCM), aliyegombea ubunge kwa tiketi ya CCM Kawe katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010 na kushindwa na mgombea wa Chadema, Halima Mdee.
Wengine katika kundi hilo walikuwa Janeth Mbene ambaye aliwahi kuteuliwa na Rais Jakaya Kikwete kuwa mbunge wa Bunge la Jamuhuri ya Muungano, Janeth Mmari, Fancy Haji Nkuhi (CCM) na Rose Mwalusamba (CUF), ambaye wakati wa kujieleza aliamua kutangaza kujitoa hata kabla hajaulizwa maswali.
Licha ya kujitoa, Katibu wa Bunge, Thomas Kashililah, aliwatangazia wabunge kuwa jina lake litabaki kwenye orodha ya wanaostahili kupigiwa kura. Alisema wagombea wote walikuwa wana nafasi ya kujitoa siku moja kabla ya uchaguzi hivyo jina lake litabaki kama lilivyowekwa kwa ajili ya kupigiwa kura.
WAGOMBEA WA ZANZIBAR
Kundi hili lilikuwa na wagombea tisa, ambapo wabunge walitakiwa kupiga kura mbili ambalo lina mchanganyiko wanawake na wanaume.
Wagombea walikuwa ni Dk. Said Ghalib Bilal, Dk. Haji Mwita, Dk. Khatib Hamad Hamad, Makame Khamis Jabir, Zuberi Ali Maulid, Abdalah Mwinyi ambaye ni mtoto wa Rais wa awamu ya pili, Nasoro Mohamed, Sofia Rijali Ali, Mariam Usi Yahya wote kutoka CCM.
KUNDI LA UPINZANI
Katika kundi hilo kulikuwa na wagombea saba ambapo pia wabunge walitakiwa kupiga kura mbili na lilikuwa na wanawake na wanaume.
Wagombea walikuwa ni Juju Martin Danda (NCCR- Mageuzi); Kessy Nderakindo (NCCR- Mageuzi); Antony Komu (Chadema); Dk. Fortunatus Masha (UDP); Mrindoko Mika Elifuraha (TLP); Polisya Mwaiseje (NCCR Mageuzi);Twaha Issa Tasilima (CUF) na John Lifa Chipaka (Tadea).
KUNDI LA TANZANIA BARA
Katika kundi hili kulikuwa wagombea 10 na wabunge walitakiwa kupiga kura tatu na kundi hili halikuwa na mwanamke hata mmoja.
Wagombea walikuwa Gamba Mrisho (CCM); Siraju Kaboyonga (CCM); Adam Kimbisa (CCM); Kingu Elibarik (CCM); Malecela William John (CCM); Edmund Mndolwa (CCM); Murunya Benard Msomi (CCM); Makongoro Nyerere (CCM), na Dk. Evans Rweikiza (CCM).
MATUKIO WAKATI WA KUJIELEZA
Hata hivyo, pamoja na Spika Makinda kuwakataza wabunge kutowapigia makofi wagombea, wagombea wengi walikuwa wakipigiwa makofi na wabunge wakati wanaingia na kutoka kuomba kura.
Aidha, mgombea Siraju Kaboyonga aliletwa na ukumbini na mpambe wa Bunge, kwa kutumia baiskeli ya kubebea wagonjwa.
Kaboyonga ambaye aliwahi kuwa mbunge wa Tabora Mjini kwenye Bunge la Tisa, alilazimika kutumia kiti hicho hadi alipomaliza kujieleza na kuulizwa maswali.
Baada ya kumaliza kujieleza, Kaboyonga alieleza kilichomsibu hadi kukaa kwenye hicho kuwa alipata ajali nje ya Bunge wakati akielekea kwenye uchaguzi huo, ingawa taarifa za awali zilieleza kuwa alikuwa kwenye hali hiyo tangu alipokuwa kwenye uteuzi wa CCM, Karimjee Dar es Salaam.
CHANZO: NIPASHE