Maximo aibuka Brazil, atoa ushauri kuhusu timu ya Taifa Tanzania

Aliyekuwa kocha Mkuu wa Timu ya Taifa Star, Marcio Maximo

Na Anna Nkinda – Sao Paul, Brazil

VILABU vya soka nchini vimeshauriwa kuwa na timu nzuri kuanzia ngazi ya watoto wenye umri wa miaka nane, vijana na kuendelea ili kupata timu bora ya Taifa.

Wito huo umetolewa jana na aliyekuwa kocha mkuu wa timu ya Taifa Star Marcio Maximo wakati akiongea na waandishi wa habari mjini Sao Paul.
Maximo alisema kuwa timu nyingi ambazo ni bora na zinafanya vizuri katika mchezo wa soka zimekuwa zikiwaandaa watoto wenye vipaji vya mchezo huo wangali wadogo ili waweze kuwa wachezaji wazuri hapo baadaye.

Kuhusiana na uvumi ulioenea kuwa anataka kwenda kufundisha timu za Taifa Stars, Azam na Yanga alisema kuwa siyo kweli na wala hajawasiliana na timu hizo na hawezi kwenda kufundisha kwani hivi sasa anamkataba wa kufundisha timu ya Democrata iliyopo nchini humo.

“Timu ya Taifa Star inakocha mzuri ambaye ninamuheshimu na ninaukubali ufundishaji wake hivyo basi kupitia kocha huyo ninaamini watanzania watazidi kuendelea katika soka na kufika mbali zaidi”, alisema.

Maximo alimalizia kwa kusema kuwa anamawasiliano mazuri na watanzania na anawapenda ndiyo maana kila mahali anapopita anajivuna na kusema kuwa Tanzania ni nchi yake ya pili.

Hivi sasa Maximo ni kocha wa timu ya Democrata iliyopo nchini humo ambapo wiki ijayo inatarajia kuanza mashindano ya taifa yatakayopelekea kupata wachezaji bora watakaoshiriki mashindano ya kombe la Dunia yanayotarajia kufanyika mwaka 2014 nchini Brazil.