Mwenyekiti wa Ulingo wa Wanawake nchini, Anna Abdallah, amesema hakuna mgombea ubunge asiyetoa rushwa katika chaguzi, hali ambayo inayosababishwa na mfumo wa uchaguzi uliopo.
Akizungumza katika semina ya wabunge iliyofanyika kwenye ukumbi wa Pius Msekwa mjini hapa jana, Abdallah ambaye ni Mbunge wa Viti Maalum (CCM), alisema kwa kupata utaratibu mpya wa kuwachagua wabunge, kutawezesha kuepuka masuala ya rushwa.
Alitolea mfano wa Mbunge wa Viti Maalum (Chadema), Cecilia Paresso, alivyopatikana na kwamba hakukuwa na rushwa kwa kuwa uteuzi huo umetokana na orodha ya majina iliyowasilishwa katika Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC).
“Mfumo wa sasa unawafanya wabunge kutoa rushwa, si kwa uchaguzi mkuu wala mdogo,” alisema Abdallah na kufafanua kuwa hakuna jambo ambalo litamsikitisha ikiwa Katiba Mpya itakuja na kasoro ambazo zinamfanya mwanamke kubaguliwa.
Pia alisema utaratibu mpya wa kuwapata wabunge utawajengea heshima wabunge wote tofauti na mfumo uliopo hivi sasa ambao mbunge wa viti maalum amekuwa akibaguliwa.
Alisema mfumo huo umekuwa ukimbagua mbunge wa viti maalum kupata nafasi ya uwaziri mkuu kwa kuwa katiba imeainisha kuwa waziri mkuu atatokana na mbunge kutoka jimboni.
Kadhalika, Abdallah alisema jambo ambalo limekuwa likimkera ni wanawake kutoteuliwa ndani ya vyama vya siasa kugombea nafasi mbalimbali za uongozi.
“Hakikisheni mnagombea kwa wingi katika chaguzi na sisi kama ulingo tutazungumza na viongozi wakuu wa vyama vya siasa,” alisema.
Akifungua semina hiyo, Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, Sophia Simba, alitoa wito kwa wabunge kutumia muda wao kwa kuwa makini ili kujenga msingi wa uelewa wa hatua mbalimbali za mabadiliko ya Katiba.
Alisema kwa kupata msingi huo, kutawawezesha kutoa michango yenye tija wakiwa kama jicho la kijinsia.
“Sote tunatambua kuwa masuala ya kikatiba ni ya kitaalamu na yanahitaji uelewa mzuri zaidi ili kutoa mchango wetu kwa jamii hususan wanawake, kwani sisi tukielewa vizuri basi tutawafikia jamii kwa kujiamini zaidi na hivyo kupata maoni yao kiurahisi,” alisema.
Wakichangia kwenye semina hiyo, wabunge hao wametaka wanawake nchini kuwaunga mkono kwa kuwapa kura wanawake wanaowania ubunge ili washinde nafasi wanazowania.
Mbunge wa Viti Maalum (Chadema), Mariam Msabaha, aliwataka wanawake kuwaunga mkono wagombea wanawake wanapogombea nafasi mbalimbali za uongozi.
Kwa upande wake, Mbunge wa Viti Maalum (CCM), Fatuma Mikidadi, alisema ingawa haki za mwanamke zimekuwa zikidaiwa tangu uhuru, lakini hadi sasa bado si yote yamekamilika.
CHANZO: NIPASHE