Wakati Bunge likitarajia kufanya uchaguzi wa wabunge wa Bunge la Afrika Mashariki kesho, Kambi rasmi ya Upinzani bungeni, imetishia kwenda Mahakama ya Afrika Mashariki kama kanuni na taratibu za uchaguzi huo hazitafuatwa.
Akizungumza na NIPASHE kwa njia ya simu kutoka Dodoma jana, Kiongozi wa Kambi hiyo, Freeman Mbowe, alisema tayari kambi hiyo imewasilisha malalamiko ya dosari kwenye uchaguzi huo kwa Katibu wa Bunge; ikipendekeza kwamba kanuni zirekebishwe ili kutoa viti zaidi vya wabunge kwa vyama vya upinzani badala ya kiti kimoja kinachotolewa hivi sasa.
Alisema: “Sisi tunaona kwamba uchaguzi unapelekwa sivyo, unafanyika kimakosa kwa sababu haiwezekani vyama vyote vya upinzani vyenye wabunge na visivyo na wabunge, vikapewa kiti kimoja; tunapendekeza angalau viwe vitatu au vikipungua kabisa viwe viwili.”
Mbowe, ambaye pia ni Mbunge wa Hai na Mwenyekiti wa Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Taifa, alisema Chama Cha Mapinduzi (CCM), kuendelea kupewa viti vinane kwenye Bunge hilo ni upendeleo ambao unaweza kuwavuruga Watanzania na Taifa kwa ujumla.
Hata hivyo, alisema anaamini kwamba suala hilo litatazamwa na kufanyiwa kazi na ofisi ya Bunge kabla ya uchaguzi huo ili Watanzania wapate haki ya kuwakilishwa kikamilifu kwenye chombo hicho.
“Tunaamini tutamaliza tofauti zetu hapa ndani kwa sababu tunajua hilo linawezekana kwa kukaa kwenye mazungumzo; hatutaki kwenda mahakamani lakini kama haki haitatendeka, hatutakuwa na namna (akimaanisha watakwenda mahakamani),” alisema Mbowe.
Mbowe ametoa kauli hiyo wakati tayari Katibu wa wabunge wa Chadema, John Mnyika, akitaka kurekebishwa kanuni za uchaguzi huo ili kuhakikisha uteuzi na uchaguzi unakuwa huru na haki kuepusha kasoro zilizojitokeza mwaka 2006 wakati wa Bunge la Tisa.
Alisema kufuatia tatizo hilo, amemwandikia barua Spika na Katibu wa Bunge, kumuomba wachukue hatua za haraka kurekebisha mchakato wa uchaguzi husika ikiwemo kuitisha kikao cha dharura cha kamati ya kanuni kwa ajili ya kuchukua hatua zinazostahili.
Alisema kwa mujibu wa msimamizi wa uchaguzi huo, chama kimoja kinatarajiwa kuwa na nafasi nane miongoni mwa nafasi tisa za wabunge wa Afrika Mashariki.
Mnyika alisema kulingana na uwiano wa idadi ya wabunge bungeni, CCM ilitakiwa kuwa na wabunge wasiozidi saba katika uchaguzi huo, Chadema mmoja na CUF mmoja.
CHANZO: NIPASHE